THOMAS ULIMWENGU (1)
Thomas Ulimwengu ‘The Buffalo’
Muktasari:
Wakati mashabiki wa soka nchini wakikiri kipaji maridhawa cha mshambuliaji namba moja wa TP Mazembe na Taifa Stars, Mbwana Samatta, lakini hapana shaka, hakuna mchezaji wa Kitanzania anayewakosha wengi zaidi kwa sasa zaidi ya Thomas Ulimwengu.
CHUMBA namba 309, hoteli ya kifahari ya Malawi Sun, Kusini mwa Jiji la Blantyre, nchini Malawi, mwili wa kiume uliojaa vyema umejilaza kitandani. Mwili uliojengeka kisoka. Si mwili wa Didier Drogba. Si wa Yaya Toure. Si wa Seydou Doumbia, wala si Victor Wanyama.
Miongoni mwa miili michache ya Kiafrika Magharibi inayoweza kupatikana Tanzania. Haupati shida kujua ni kwa nini anawasumbua walinzi wengi wa timu kubwa za Taifa zinazokuja nchini. Ni Thomas Ulimwengu ‘The Buffalo’.
Wakati mashabiki wa soka nchini wakikiri kipaji maridhawa cha mshambuliaji namba moja wa TP Mazembe na Taifa Stars, Mbwana Samatta, lakini hapana shaka, hakuna mchezaji wa Kitanzania anayewakosha wengi zaidi kwa sasa zaidi ya Thomas Ulimwengu.
Ulimwengu ana mwili mkubwa, misuli minene. Ungetegemea mchezaji wa aina yake awe na kasi ndogo uwanjani, lakini cha kushangaza Ulimwengu ana kasi kubwa uwanjani hasa anapokwenda upande wa pembeni ambako amezoeshwa kucheza katika timu ya Taifa.
Wakati Mbwana ambaye ni rafiki yake mkubwa ndani na nje ya uwanja akiwa mfungaji zaidi, Ulimwengu amejikita katika kuyatengeneza na kuyafunga. Wiki moja iliyopita ilikuwa ni ya mfano wa kile anachoweza kukifanya ndani ya uwanja kwa sasa. Katika pambano dhidi ya timu ya taifa ya Malawi, Ulimwengu alipika kwa juhudi binafsi bao la Samatta, lakini hapo hapo akafunga bao la pili.
Wiki tatu zilizopita, Ulimwengu alifunga bao la kufutia machozi dhidi ya El Marreikh jijini Khartoum akiwa na jezi yake namba 28 ya TP Mazembe na wiki moja iliyofuata Ulimwengu alipika bao moja kati ya mawili ambayo Samatta alifunga katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya El Marreikh, Lubumbashi.
Huu ni mwendelezo wa kuibuka zaidi kwa Ulimwengu ambaye kabla ya kuondoka katika mipaka ya Tanzania alikuwa akikipiga katika klabu ya Moro United iliyokuwa imemnyakua kutoka katika kituo cha soka cha TFF, TSA.
Ulimwengu ni miongoni mwa wachezaji wachache mastaa wa kileo ambao mpaka sasa hawajagusa jezi za klabu mbili maarufu nchini, Simba na Yanga.
Utapata wapi muda wa kuongea kwa utulivu na Ulimwengu zaidi ya wakati huu akiwa na simu yake mkononi, rimoti mkononi, na tabasamu usoni? Kabla ya kila kitu naanza kumuuliza jinsi alivyotua Mazembe. Ni kitu ambacho kinawasumbua Watanzania wengi kujua jinsi gani aliibukia Mazembe.
“Wakati huo nilikuwa nacheza Athletic Football Club ya Sweden. Unakumbuka wakati ule nilikuwa nacheza Ulaya muda mwingi? Ile timu ilikuwa inakusanya vipaji mbalimbali kwa ajili ya kuviuza,” Anaanza kusimulia Ulimwengu kwa utulivu huku tukitazama filamu inayotisha ndani ya chumba chake.
“Meneja wangu anaitwa Roland (raia wa Ufaransa) akaambiwa na ile timu kuwa kwa sababu nisingeweza kupata kibali kutokana na umri wangu kuwa mdogo basi anitafutie timu kubwa Afrika ili nipate uzoefu halafu baadaye nirudi tena Ulaya,” anaongeza Ulimwengu.
“Uzuri wa Roland ni kwamba ana mawasiliano na klabu nyingi za Ulaya na Afrika. Ikawa rahisi kwake kuwasiliana na Moise Katumbi (tajiri wa Mazembe) ili nicheze pale. Nikafanya majaribio na kufaulu,” anasema Ulimwengu.
“Hata hivyo sikusaini mkataba wowote na Mazembe ingawa nilifaulu majaribio. Baada ya kumaliza majaribio tu Meneja wangu Roland akaniambia kuna ofa ya mimi kufanya majaribio Ujerumani katika klabu ya Hamburg. Kwa hiyo tukapanda ndege mpaka Hamburg kwa ajili ya kufanya majaribio,” anasema Ulimwengu.
“Wakati nikiwa Ujerumani huku nyuma ndiyo Mbwana akatua TP Mazembe akitokea Simba. Kwa hiyo hapo utagundua kuwa mimi nilifika Mazembe kabla yake ingawa Mbwana alitangulia kupata mkataba kwa sababu alipofika tu alisaini mkataba. Mimi nilifanya majaribio na kuondoka zangu kwenda Hamburg bila ya mkataba,” anasimulia Ulimwengu.
Napata wasaa mzuri wa kuzungumza na Ulimwengu hasa ukizingatia kuwa rafiki yake anayelala naye chumba kimoja, Samatta hayupo chumbani. Ni hapo ninapopata fursa ya kumuuliza kuhusu maisha ya Ujerumani.
Je ni nini kiliendelea wakati alipokwenda Hamburg? Je unafahamu kwamba wakati akiwa Hamburg alipata bahati ya kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza cha Hamburg? Ni wachezaji gani mahiri ambao alifanya nao mazoezi katika kikosi hicho? Kesho fuatilia mahojiano haya ya kusisimua kati ya Thomas Ulimwengu na mwandishi Edo Kumwembe yaliyofanyika jijini Blantyre hivi karibuni.