Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TFF yaingilia uchaguzi Simba, Magori na Mangungu wakutanishwa

TFF Pict

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Kiomoni Kiburu Kibamba, alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kamati yake kupokea malalamiko kuhusu utaratibu uliotumiwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Simba Sports Club Company katika kuandaa uchaguzi.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeamua kusimamia moja kwa moja mchakato wa uchaguzi wa Simba SC baada ya kubaini mapungufu katika ratiba iliyotolewa awali na klabu hiyo, hatua inayolenga kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa kuzingatia katiba, kanuni na taratibu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Kiomoni Kiburu Kibamba, alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kamati yake kupokea malalamiko kuhusu utaratibu uliotumiwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Simba Sports Club Company katika kuandaa uchaguzi.

Alisema kamati ilipokea barua mbili kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu wa TFF. Barua ya kwanza ilitoa taarifa ya kuanza kwa mchakato wa uchaguzi wa Simba, huku nyingine ikiwa na malalamiko kuhusu utaratibu uliotumiwa na bodi hiyo.

Kutokana na hali hiyo, kamati iliamua kuwasikiliza wahusika wa pande zote kabla ya kutoa maelekezo kuhusu namna uchaguzi utakavyoendeshwa.

Kibamba alisema walifanya mazungumzo na wawakilishi wa pande mbili, akiwamo Crescentius Magori aliyewakilisha upande wa mwekezaji na Murtaza Mangungu kwa upande wa wanachama.

Baada ya mazungumzo hayo, kamati ilisisitiza kuwa uchaguzi wa viongozi wa upande wa wanachama na mwekezaji lazima ukamilike kabla ya muda wao wa uongozi kumalizika Januari 29, 2027.

Viongozi hao walichaguliwa Januari 29, 2023, kwa kipindi cha miaka minne kwa mujibu wa Katiba ya Simba na kanuni za TFF.

“Iwe mvua iwe jua, uchaguzi lazima ufanyike. Kwa kuwa uchaguzi ulifanyika Januari 29, 2023, maana yake ukomo wa uongozi wao ni Januari 29, 2027,” alisema Kibamba.

Hata hivyo, alisema kamati imebaini mapungufu mawili katika ratiba ya uchaguzi iliyokuwa imetolewa na kamati iliyoundwa na Bodi ya Simba.

Alifafanua kuwa ratiba hiyo haikuweka utaratibu wa rufaa kwa wagombea ambao hawataridhishwa na maamuzi ya uteuzi, pamoja na masuala ya maadili ambayo ni sehemu muhimu ya mchakato wa uchaguzi.

Kutokana na mapungufu hayo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilihitaji siku mbili au tatu kufanya marekebisho kabla ya kutangaza rasmi ratiba iliyoboreshwa.

Kibamba alisema baada ya marekebisho hayo, zoezi la uchukuaji fomu za kugombea lilipangwa kuanza Ijumaa katika ofisi za Simba, huku kalenda kamili ya uchaguzi ikitangazwa rasmi.

Alisisitiza kuwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF ndiyo itakayoratibu na kusimamia moja kwa moja mchakato mzima kwa kushirikiana na menejimenti ya Simba.

Alisema hatua hiyo ina msingi wa kisheria kupitia Kanuni ya 14 ya Kanuni za Uchaguzi za Simba Sports Club za mwaka 2021, inayoiwezesha TFF kuingilia mchakato wa uchaguzi wa klabu wakati wowote ili kufuatilia uadilifu na kuhakikisha taratibu zinafuatwa.

“Kanuni ya 14 inasema TFF ina haki ya kuingilia mchakato wa uchaguzi wa klabu wakati wowote ili kufuatilia uadilifu na kuchunguza kama kanuni hizi, sheria na taratibu za klabu zinafuatwa,” alisema.

Aliongeza kuwa kanuni hiyo inaipa TFF mamlaka ya kufuta au kubatilisha mchakato wa uchaguzi endapo kutabainika ukiukwaji wa taratibu.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa kwa sasa uchaguzi wa Simba haujabatilishwa, bali utaendelea chini ya usimamizi wa TFF.

Aidha, alitaja Kanuni za Uchaguzi za TFF kuwa sehemu nyingine ya msingi wa mamlaka hayo, kwa kuwa zinaipa kamati jukumu la kuratibu na kusimamia michakato ya uchaguzi ya shirikisho, Bodi ya Ligi na wanachama wake, wakiwamo klabu za soka.

Kibamba alisema TFF itatumia mamlaka hayo kuhakikisha uchaguzi wa Simba unakamilika kwa kuzingatia ratiba itakayopangwa na kabla ya kumalizika kwa kipindi cha uongozi wa sasa.