Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rekodi zaibeba Taifa Stars kwa Madagascar

STARS Pict

Muktasari:

  • Mchezo huo unakuja baada ya Taifa Stars kuanza vibaya kampeni hiyo kwa kupoteza mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Guinea-Bissau, matokeo yanayoongeza umuhimu wa timu hiyo kutafuta mrejesho mzuri katika mchezo wa leo utakaoanza saa 10:00 jioni kwa majira ya Tanzania.

TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo itashuka dimbani kuumana na Madagascar, katika mchezo wa Kundi L wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, utakaopigwa kwenye Uwanja wa d’Honneur, Meknes nchini Morocco.

Mchezo huo unakuja baada ya Taifa Stars kuanza vibaya kampeni hiyo kwa kupoteza mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Guinea-Bissau, matokeo yanayoongeza umuhimu wa timu hiyo kutafuta mrejesho mzuri katika mchezo wa leo utakaoanza saa 10:00 jioni kwa majira ya Tanzania.

Hata hivyo, kabla ya kuingia uwanjani, Taifa Stars ina jambo moja la kujivunia katika historia ya michezo yake na Madagascar. Timu hizo zimekutana mara 10 katika mashindano rasmi, huku Stars ikishinda mara nne, sare tatu na kupoteza mara tatu.

Hiyo inaifanya Taifa Stars iingie kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi nzuri zaidi dhidi ya Madagascar, kwa kuwa imeshinda mchezo mmoja zaidi katika mikutano yao. Kwa upande wa mabao, Madagascar inaongoza ikiwa imefunga 17 dhidi ya 15 ya Stars.

Historia hiyo imejengwa katika vipindi tofauti. Katika Michezo ya Afrika mwaka 1965, Madagascar iliichapa Tanzania mabao 5-1, lakini Stars ikajibu siku mbili baadaye kwa ushindi wa mabao 2-1.

Mwaka 1967, Madagascar ilitawala michezo miwili ya kuwania kufuzu Olimpiki, ikiifunga Tanzania mabao 4-2 na 2-0. Lakini mambo yalibadilika katika miaka iliyofuata, hasa kwenye michezo ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

AFCO 01

Katika michezo mitatu ya kuwania Kombe la Dunia, Taifa Stars haijawahi kupoteza dhidi ya Madagascar. Mwaka 1992, timu hizo zilitoka sare ya 0-0, kabla ya kukutana tena mwaka 2021, ambapo Taifa Stars ilishinda 3-2 katika mchezo wa kwanza, huku mchezo wa marudiano ukimalizika kwa sare ya 1-1.

Michezo miwili ya karibuni nayo imegawanyika. Juni 2025, Madagascar ilishinda bao 1-0 katika mashindano ya Kusini mwa Afrika (COSAFA), kabla Stars haijajibu Agosti kwa ushindi wa mabao 2-1 katika Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Ingawa Madagascar imekuwa ikifunga mabao mengi zaidi katika historia yote ya mikutano hiyo, Tanzania ndiyo inayoshikilia idadi kubwa ya ushindi. Rekodi inasema wazi, imeshinda mara nne, Madagascar imeshinda mara tatu na mara tatu mchezo ukamalizika kwa sare.

Hilo linaipa Tanzania kumbukumbu nzuri kabla ya mchezo wa leo, lakini Stars italazimika kuonyesha tofauti hiyo ndani ya dakika 90.

Kipigo cha Guinea-Bissau kimeifanya timu hiyo kuhitaji mwitikio mzuri ili kurejesha hali ya kujiamini. Mazingira kama hayo pia yapo kwa Madagascar, ambayo imetoka kupoteza mabao 2-1 kutoka kwa Nigeria.

Kwa Madagascar, mchezo huu ni nafasi ya kusawazisha hesabu ya historia. Kwa Stars, ni fursa ya kuongeza ushindi wake wa tano na kuendeleza rekodi inayoiweka mbele katika mikutano yao rasmi.

Zaidi ya yote, matokeo ya aina yoyote hayataathiri Taifa Stars, kwani tayari inayo tiketi ya kushiriki AFCON 2027, kutokana na kuwa nchi mwenyeji, kama ilivyo kwa Kenya na Uganda.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, kocha wa Taifa Stars, Miguel Gamondi, amesema: “Hakuna muda mwingi wa kubadili mambo, hivyo tutaendelea na mfumo wetu na kujaribu kuboresha.

“Hata hivyo, adhani tupo kwenye njia sahihi ya kuboresha na kujenga timu hii kwa ajili ya Kombe la Mataifa ya Afrika lijalo.”