Tanzania yaanza na sare Kombe la Dunia, Kayanda akiwaka
Muktasari:
- Tanzania ilianza mechi hiyo ikitanguliwa kwa mabao mawili ndani ya dakika 15 za kipindi cha kwanza, baada ya Jefrey Urbina kuifungia Costa Rica bao la kwanza dakika ya nane, kabla ya Jorshuad Pilarte kuongeza la pili dakika ya 15.
TANZANIA imeanza safari ya Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 17, Qatar 2026, kwa kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Costa Rica katika mechi ya kwanza ya Kundi I, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Doha Aspire Zone, Pitch 1.
Tanzania ilianza mechi hiyo ikitanguliwa kwa mabao mawili ndani ya dakika 15 za kipindi cha kwanza, baada ya Jefrey Urbina kuifungia Costa Rica bao la kwanza dakika ya nane, kabla ya Jorshuad Pilarte kuongeza la pili dakika ya 15.
Hata hivyo, vijana wa Tanzania wakarejea kipindi cha pili wakiwa na nguvu mpya na kuanza kuisumbua ngome ya Costa Rica.
Juhudi hizo zilizaa matunda dakika ya 51 baada ya Faraji Kayanda kuifungia Tanzania bao la kwanza na kupunguza pengo la mabao.
Kayanda aliendelea kuwa mwiba kwa mabeki wa Costa Rica, akafunga bao la pili dakika ya 73 na kuisawazishia Tanzania, baada ya awali kukosa penalti dakika ya 55. Mabao hayo mawili yaliifanya Tanzania kurejea mchezoni.
Licha ya mabao hayo lakini mshambuliaji huyo anayekipiga Dodoma Jiji kama angekuwa makini na nafasi ambazo zilikuwa zimetengezwa angefunga zaidi ya mabao mawili na kuwa mchezaji wa pili kufunga hat-trick kwenye Kombe la Dunia baada ya Halidou Maïga (Mali) kufunga mabao matatu katika ushindi wa Mali wa 3-0 dhidi ya New Zealand, Novemba 20.
Takwimu zinaonyesha licha ya Tanzania kurudisha mabao mawili lakini ilikuwa bora kwenye mechi hiyo ikipiga
mashuti 22 dhidi ya tisa ya Costa Rica na kumiliki mpira kwa asilimia 59.8.
Mechi inayofuata kwa Tanzania ni dhidi ya Brazil Novemba 24, kabla ya kukamilisha michezo ya kundi hilo kwa kukutana na Jamhuri ya Ireland Novemba 27.