Pamba Jiji yazindukia Kirumba dakika za jioni
Muktasari:
- Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini, Mwanza, Pamba Jiji ilikuwa ya kwanza kupata bao la dakika ya nane lililofungwa na mshambuliaji, Abdoulaye Camara, kisha Maabad Maulid akaisawazishia Coastal dakika ya 13.
BAO la dakika ya 90+5, lililofungwa na beki wa kati wa Pamba Jiji, Abdulrahim Bausi, limetosha kuipa timu hiyo pointi tatu muhimu, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2, dhidi ya Coastal Union 'Wagosi wa Kaya' katika mechi ya Ligi Kuu.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini, Mwanza, Pamba Jiji ilikuwa ya kwanza kupata bao la dakika ya nane lililofungwa na mshambuliaji, Abdoulaye Camara, kisha Maabad Maulid akaisawazishia Coastal dakika ya 13.
Pamba Jiji ikajibu mapigo hayo na kufunga bao la pili dakika ya 38, lililofungwa na mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Deogratius Mafie na kuipeleka timu hiyo hadi dakika 45, za kipindi cha kwanza ikiwa kifua mbele dhidi ya Coastal Union.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Coastal Union ikasawazisha tena bao hilo dakika ya 54, kupitia kwa Maabad Maulid likiwa ni bao lake la pili katika mechi hiyo, ila likiwa ni la tano la Ligi Kuu Bara tangu kuanza kwa msimu huu wa 2026-2027.
Wakati mechi hiyo ikionekana inaisha kwa sare, beki wa kikosi hicho, Abdulrahim Bausi akaifungia Pamba Jiji bao la tatu na la ushindi dakika ya 90+5, ukiwa ni ushindi wa kwanza kwa timu hiyo baada ya kucheza mechi nne mfululizo bila ya ushindi.
Kwa matokeo hayo, yanaifanya Pamba Jiji imefikishe pointi tisa ikiwa nafasi ya 13, baada ya kushinda mechi mbili, sare tatu na kupoteza saba, huku Coastal Union ikishinda nne, sare mbili na kupoteza sita, ikiwa nafasi ya 10 na pointi 14.