Takukuru yabaini upungufu ujenzi wa viwanja vya mazoezi AFCON Dar
Muktasari:
- Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu za Afrika Mashariki, pamoja na Kenya na Uganda, zitakazokuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON 2027
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) Kinondoni, imebaini upungufu katika utekelezaji wa miradi 14 ya maendeleo, mmoja ukihusisha ujenzi viwanja vitatu vya mazoezi kwa ajili ya Fainali za Mataifa ya Aftina (AFCON) 2027 vinavyojengwa Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Novemba 11,2026 na Naibu Mkuu wa Takukuru Kinondoni, Elizabeth Mokiwa, alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026.
Elizabeth amesema katika kipindi tajwa wamefuatilia matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo 14 yenye thamani ya Sh81 bilioni.
Hata hivyo amesema mradi mmoja kati ya hiyo ni ule wenye thamani ya zaidi ya Sh51.6 bilioni katika sekta ya Michezo ambayo ni mradi wa ujenzi wa Viwanja vya Mazoezi vya Leaders Club, Gymkhana 2 na Farasi vitakavyotumika kwenye mashindano ya AFCON 2027.
"Katika kutekeleza jukumu tumebaini mapungufu kadhaa katika utekelezaji wa miradi hiyo na hivyo kufanya vikao kazi na watekelezaji wa miradi hiyo wakiwemo wakandarasi, washauri na wasimamizi wa miradi pamoja na Ofisi ya mthibiti ubora ili kuhakikisha miradi inakamilika ndani ya muda uliopangwa na kwa kuzingatia ubora,"amesema.
Hata hivyo amebainisha kwamba baadhi ya mapungufu yaliyobainika tayari yamefanyiwa kazi na mengine yanaendelea kufanyiwa kazi hadi sasa.
Mkuu huyo alipoulizwa ni mapungufu gani haswa wameyabaini katika viwanja hivyo, hakuwa tayari kutaja zaidi ya kusema wanapofuatilia miradi ni kuhakikisha inakamilika kwa wakati na matumizi ya fedha yanakuwa kama inavyotakiwa.
Pia amesema kwa kuwa ni miradi inayoendelea, mapungufu yanapoonekana huwa wanatoa maelekezo ya nini wahusika wanapaswa kufanywa kwenye eneo Gani na kwa wakati gani.
"Hivyo hayo marekebisho yapo ambayo yamesharekebishwa na yapo ambayo bado yanendelea," amesema Elizabeth.
Hali ya Uchunguzi wa mashtaka
Katika hatua nyingine Takukuru imeelezea hali ya
uchunguzi wa mashitaka katika kipindi hicho ilivyokuwa ambapo inaelezwa malalamiko 110 yalipokelewa na kati ya hayo malalamiko 47 yalihusu rushwa na malalamiko 63 hayakuhusu rushwa.
Elizabeth amesema malalamiko 47 yaliyohusu rushwa uchunguzi wake unaendelea na upo katika hatua mbalimbali huku malalamiko 63 ambayo hayakuhusu rushwa, walalamikaji walishauriwa.
Pia katika kipindi tajwa kesi 14 zinaendelea mahakamani, ambapo kati ya kesi hizo, kesi mpya 10 zilifunguliwa na kesi 12 zilitolewa maamuzi na Jamhuri ilishinda kesi 9
Mapato
Katika eneo la Mapato, Elizabeth amesema katika kipindi hicho, Takukuru ilifanikisha kukusanya Sh37 milioni za ushuru na adhabu kwa Mamiaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokana na uingizaji wa magendo wa madumu 510 ya mafuta ya kula ya ujazo wa lita 20 kupitia Pwani ya Kunduchi.
"Ofisi ya Takukuru Mkoa wa Kinondoni ilifanya ufuatiliaji katika eneo la Kunduchi na kukamata gari lililokuwa limesafirisha shehena hiyo.Uchunguzi ulibaini kuwa mwagizaji hakuwa na nyaraka halali za uingizaji wa bidhaa nchini wala uthibitisho wa kulipa kodi na ushuru stahiki.
"Kwa kushirikiana na TRA, Takukuru ilichukua hatua za kisheria dhidi ya mwagizaji pamoja na mmiliki wa gari. Aidha ushuru na adhabu ya jumia ya Shs37 milioni ulilipwa," amesema.
Hata hivyo Elizabeth amesema mafuta
baada ya mamlaka husika kujiridhisha kuwa yalikuwa salama kwa matumizi ya binadamu, mwagizaji aliruhusiwa kukamilisha taratibu za kuyachukua.
Kutokana na hilo Takukuru imesisitiza kuwa uingizaji wa bidhaa kwa njia za magendo husababisha Serikali kupoteza mapato ya kodi, huathiri ushindani wa haki katika biashara na unaweza kuhatarisha afya ya wananchi kutokana na bidhaa kukwepa ukaguzi wa mamlaka husika.
Imetoa wito kwa waagizaji wa mafuta ya kula na bidhaa nyingine kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uingizaji wa bidhaa nchini, pamoja na kulipa kodi na ushuru stahiki kwa TRA.
Pia Mkuu huyo amesisitiza wataendelea kushirikiana na TRA na taasisi nyingine za Serikali kudhibiti vitendo vya ukwepaji kodi na uingizaji wa bidhaa kwa njia za magendo ili kulinda uchumi wa Taifa.
Mikakati
Akielezea kuhusu mikakati yao katika kipindi Cha Oktoba hadi Desemba, Elizabeth amesema ni kuendelea kufuatiliwa matumizi ya fedha za serikali katika miradi ya maendeleo.
Jingine ni kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu kuzuia Rushwa kwenye miradi ya maendeleo na kuendelea kufuatiliwa utekelezaji wa mapendekezo ya programu ya Takukuru-Rafiki.