Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dakika za jioni kabisa marefa wameamua kuharibu ligi


MBIO tamu za ubingwa zipo England. Arsenal yupo juu anakimbizana na Manchester City. Nini kinatokea? Arsenal angeweza kuwa amechukua ubingwa mapema tu lakini naye kuna wakati anajikuta anaambulia sare za kijinga tu. Inatokea pia kwa wapinzani Manchester City. Nao huwa wanaangusha pointi za kijinga tu.


Kwa mfano Arsenal aliangusha pointi kwa Wolves. Timu dhaifu ambayo inaburuza mkia pale England. Juzi Man City imepoteza pointi za kijinga ugenini dhidi ya West Ham ambayo nayo ipo kule maeneo ya mkiani. Hakuna kitu cha kushangaza. Waamuzi wa mechi kama hizi hawakuhitaji kwenda katika VAR kuthibitisha maamuzi yao. Mashabiki wakabaki kuzilaumu timu zao. Basi.

Pale Hispania Barcelona na Real Madrid wanawania ubingwa lakini wamekuwa wakiangusha pointi kwa timu za kawaida tu. Madrid majuzi tu amechapwa na Osasuna. Kwao ni kitu cha kawaida tu. Kama mmoja kati ya Barcelona au Madrid angekuwa haangushi pointi kijinga si ajabu sasa hivi mmoja wao angekuwa anaongoza kwa pointi zaidi ya 15 dhidi ya mwenzake.

Sisi tuna Simba na Yanga zinataka ubingwa. Tutaanza kuona mauzauza mengi kutoka kwa waamuzi. Ili mradi tu wakubwa wanakimbizana kule juu. Hatuamini wakubwa wanaweza kuteleza na kutoka sare au kufungwa. Katika ligi ya mabingwa Afrika tunaamini lolote linaweza kutokea lakini katika ligi hatuamini kama wakubwa wanaweza kutoka sare au kufungwa dhidi ya timu za kawaida.

Hatuamini kama Wolves na West Ham za huku zinaweza kutoa sare na wakubwa. Kwa mfano, sare ya Yanga na Mbeya City ugenini pale Mbeya lilikuwa jambo la ajabu katika mpira wetu. Mashabiki wakashinikiza lazima kocha afukuzwe. Sio hilo tu, kulikuwa na mambo mengi ambayo yaliandamana na pambano lile. Kama Yanga angeshinda kusingekuwa na tatizo lolote la msingi.

Ikaja mechi ya Simba na Dodoma Jiji pale Dodoma. Ilionekana ni jambo la ajabu sana Simba kutoka sare. Hata wachezaji wa Dodoma Jiji walishangilia mno na mashabiki wao kama vile pambano hilo lilikuwa linaamua hatima ya wao kubakia ligi kuu. Kumbe hata wachezaji wa hizi timu huwa hawaamini kama wanaweza kutoka sare na Simba au Yanga. Basi ndio hivyo hivyo hata waamuzi nao hawaamini kama hizi timu zinaweza kufungwa au kutoka sare.

Namungo walinyimwa penalti halali pale kwao Ruangwa katika pambano dhidi ya Yanga. Majuzi pia Singida Black Stars wakanyimwa penalti halali dhidi ya Simba wakiwa kwao Singida. Kama unabisha kuwa hazikuwa penalti halali subiri siku nyingine kama matukio hayo yakitokea katika malango yao. Mwamuzi anaweka penalti.

Tatizo nini? Kule kwa wazungu kuna weledi mkubwa. Lakini unaweza kuniambia Arsenal na Manchester City sio wapinzani wa jadi kama Simba na Yanga. Labda ndiyo maana waamuzi wanatoa maamuzi halali. Au labda utaniambia waamuzi wanasaidiwa na VAR. Sio kweli. Sisi huku waamuzi wanaamua kufanya maamuzi ya ovyo makusudi. Ndiyo, makusudi tu.

Waamuzi wetu wanajua wanachofanya. Tulianza ligi tukiwa shwari kabisa. Nusura niwasifie waamuzi wetu kwa weledi ambao walikuwa wanauonyesha hapo awali. Lakini sasa hivi wakubwa wetu wametolewa kule katika michuano ya Afrika na akili yao yote wameielekeza katika ubingwa wetu..ubingwa ambao kwao kwa kiasi kikubwa hauna maana kubwa sana. Wameshachukua mara nyingi. Na kama zawadi ya ubingwa sidhani kama ni kitu ambacho kinawasumbua.

Kinachowasumbua wakubwa ni ufahari tu. Simba anataka kumzuia Yanga asichukue ubingwa kwa mara ya tano mfululizo. Yanga anataka kuchukua kwa mara ya tano mfululizo. Vyovyote ilivyo kwangu siyo habari kubwa sana. Yanga kujenga uwanja wao kama walivyodhamiria ni habari kubwa kuliko kuchukua ubingwa wa ligi kuu kwa mara ya tano mfululizo.  Simba wana mambo mengi ya msingi kufanya kuliko kuwazuia Yanga kuchukua ubingwa. Kama watachukua kwa uwezo wao basi hakuna mbaya.

Nafasi mbili za kucheza ligi ya mabingwa wa Afrika wanazo. Sio kesi sana. Kulazimisha ubingwa kwa kiasi kilichopitiliza mpaka waamuzi wanaharibu mechi sio sawa. Hao kina Arsenal na Manchester City hawalazimishi kiasi cha kuitia ligi aibu. Waamuzi naona wameingia kazini kiasi tunalazimika kuulizana lile swali maarufu. Waamuzi wetu wanahongwa, wanakosea kwa bahati mbaya, wana mapenzi na timu hizo au hawajui sheria?

Hatujawahi kupata jibu sahihi lakini katika yote hayo ninachojua ni waamuzi wetu wanajua sheria. Wanajua wanachopaswa kufanya uwanjani. Wanaamua tu kuharibu. Waamuzi wetu ukikaa nao baa ukawauliza maswali mbalimbali kuhusu sheria mbalimbali za uwanjani huwa wanakueleza ukweli mtupu na wananyoosha maelezo. Ni tofauti na kile wanachoenda kufanya uwanjani.

Hapa ndio huwa hatuna ushahidi wa kile kinachoendelea nyuma ya pazia. Wanahongwa? Hatuna uhakika kwa sababu Takukuru hawapo bize na upande huu. Wana mapenzi binafsi na hizi timu? Hili jambo ni gumu. Kule kwa wazungu waamuzi huwa wanaweka wazi timu wanazoshabikia. Huwa hawapangwi kuchezesha mechi zinazohusu timu zao. Huku jambo hilo ni gumu kwa sababu nchi imegawanyika katika pande mbili. Mwamuzi lazima atakuwa Yanga au Simba.

Hatujali kama mwamuzi ambaye alikuwa na mapenzi na Yanga utotoni apendelee Yanga. Wala hatujali kama mwamuzi ambaye alikuwa ana mapenzi na Simba utotoni awe apendelee Simba. Tunataka haki na uwajibikaji. Kule kwa wenzetu hata kama mwamuzi sio shabiki wa Liverpool na katika hisia zake angependa Liverpool ishinde mechi bado hawezi kupendelea.

Kutoka hapa mpaka mwishoni mwa msimu usitegemee kuona mwamuzi akiweka penalti dhidi ya Simba au Yanga katika dakika tano za mwisho za mchezo. Hawezi. Hana ubavu huo. Kuna ambao tunahisi ambao wamechukua chao lakini kuna wengine ambao wanashindwa kuhimili presha ya majukwaa na watu wanaotazama mechi kutoka nyumbani. Wanaogopa lawama. Inawezekana hawajachukua chochote lakini wanaogopa kuudhi watu.

Hatuwezi kuwa na ligi ya namna hii ambayo tunatazamia wakubwa watapewa penalti laini huku wadogo wakinyimwa penalti zao za wazi. Hili jambo limekuwa likijirudia mara nyingi tu. Hata wachezaji wa timu ndogo huwa tunaziangalia sura zao kwa huzuni wakati wanalalamika. Tunajua wanaonewa. Ni basi tu tunajikaza.

Wakubwa wanapooneana wenyewe adhabu zinatolewa kwa haraka. Ni kama vile tulivyoona kwa mwamuzi msaidizi aliyekataa bao la Suleiman Mwalimu na pia nafasi ya kufunga ya Prince Dube. Jaribu kufikiria tu kuna mwamuzi amefungiwa kwa kuikataa tu nafasi ya kufunga na sio bao lenyewe. Ingetokea kwa mchezaji wa Namungo dhidi ya Simba au Yanga unadhani angefungiwa?

Tusiharibu mpira wetu. Nafahamu presha katika mchezo wa soka imekwenda juu zaidi kwa sababu ya maisha ya mitandao ya jamii. Hata hivyo tunapaswa kusimama imara na kusimamia haki. Dunia imekuwa kama kijiji. Kuna matukio ambayo tunayafanya na yanawafikia wenzetu kiasi cha kwamba tunaonekana kichekesho huku tukisifia ubora wa ligi yetu.

Ubingwa feki hauwezi kutusaidia katika kuunda timu imara ambazo zitakuwa zinapambana na akina Al Ahly. Tunahitaji uwanja wa haki ambao utawafanya wakubwa wapambane kuimarisha vikosi vyao. Unanunua wachezaji wa bei mbaya, mishahara mikubwa, kocha mkubwa mwenye mshahara mkubwa na bado unawaona waamuzi. Inasaidia nini?