Kombe la EPL latua Tanzania kwa mara ya kwanza
Muktasari:
- Kombe la Ligi Kuu England limetua Tanzania kwa mara ya kwanza katika historia kwa lengo kunogesha na kuunganisha mashabiki wa soka Tanzania na dunia.
Dar es Salaam. Kombe la Ligi Kuu ya England (EPL) limewasili nchini kwa mara ya kwanza, likianza ziara yake ya Afrika Mashariki iliyoandaliwa na kampuni ya bia ya Guinness, mmoja wa wadhamini wa ligi hiyo.
Kombe hilo limewasili nchini leo Oktoba 9, 2026, kwa ajili ya sherehe za siku mbili zinazolenga kuwaunganisha mashabiki wa soka na utamaduni wa mchezo huo nchini.
Ziara hiyo inalenga kuwakutanisha mashabiki wa soka la Tanzania na moja ya alama zinazotambulika zaidi katika soka la kimataifa, huku ikitoa fursa ya kuonyesha utamaduni na mapenzi ya Watanzania kwa mchezo huo.
Akizungumzia ujio wa kombe hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Serengeti Breweries, Dk Obinna Anyalebechi, amesema Tanzania ina mamilioni ya mashabiki wanaofuatilia EPL, hivyo kulileta kombe hilo nchini ni fursa ya kuwapa uzoefu wa kipekee.
“Ligi Kuu ya Uingereza tayari ina nafasi kubwa katika mioyo na mazungumzo ya mamilioni ya mashabiki wa soka, wakiwemo Watanzania. Kinachofanya tukio hili kuwa tofauti ni kwamba sasa kombe lenyewe limefika hapa, likikutana na mashabiki mahali ambapo mapenzi yao kwa soka yanaishi,” amesema.
Amesema lengo ni kuandaa tukio litakalodhihirisha utamaduni wa Tanzania na kuonyesha namna soka la kimataifa linavyokutana na ubunifu na mapenzi ya Watanzania kwa mchezo huo.
Ujio wa kombe hilo unatarajiwa kuongeza hamasa kwa mashabiki wa soka nchini, wakiwemo wafuasi wa klabu za Simba na Yanga, ambazo zina idadi kubwa ya mashabiki wanaofuatilia pia ligi mbalimbali za kimataifa.
Mkurugenzi wa Masoko na Ubunifu wa Serengeti Breweries, Henry Esiaba, alisema ziara hiyo ni nafasi ya kuhusisha mashabiki katika tukio hilo kwa kuzingatia utamaduni wa soka nchini.
“Tanzania ina utamaduni mkubwa sana wa soka, na kulileta Kombe la Ligi Kuu ya Uingereza hapa kumetupa nafasi ya kuona mapenzi hayo kwa karibu,” amesema.
Ameongeza kuwa kampuni hiyo inataka mashabiki na simulizi zao kuwa sehemu muhimu ya tukio hilo, huku wakipata nafasi ya kusherehekea ujio wa kombe hilo na mchezo wa soka kwa ujumla.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Aaron Nyanda, amesema kuwasili kwa kombe hilo kunaonyesha uhusiano uliopo kati ya mashabiki wa Tanzania na soka la kimataifa.
Amesema mashabiki wa Tanzania wanafuatilia soka katika ngazi mbalimbali, kuanzia ligi za ndani hadi mashindano ya kimataifa, hivyo tukio hilo linatoa fursa ya kukutana na soka la kimataifa kwa namna tofauti.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema ujio wa kombe hilo una umuhimu zaidi ya burudani ya soka, kwa kuwa michezo ina nafasi ya kuwaunganisha watu, kukuza vipaji vya vijana na kuitangaza nchi.
“Michezo huwaleta watu pamoja, hutengeneza fursa kwa vijana na kutoa nafasi kwa nchi kuonyesha utamaduni na utambulisho wake. Kwa hiyo, kuwasili kwa Kombe la Ligi Kuu ya Uingereza si tukio kwa mashabiki wa soka pekee, bali pia ni fursa ya kuonyesha nafasi kubwa ambayo michezo inaendelea kuwa nayo katika jamii yetu,” amesema.
Baada ya kumaliza ziara yake Tanzania, kombe hilo linatarajiwa kuelekea Uganda kuanzia Oktoba 11 hadi 13, kabla ya kuhitimisha safari yake nchini Kenya.