TAIFA Stars imeingia katika kipindi cha maswali mengi kuhusu uwezo na maandalizi ya kikosi hicho kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, huku wadau wa soka wakibainisha changamoto mbalimbali zinazotakiwa kufanyiwa kazi licha ya Tanzania kufuzu moja kwa moja kwa mashindano hayo kwa kuwa mwenyeji.
Stars ambayo itashiriki AFCON 2027 itakayofanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027 kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda, imeanza kuonyesha mwenendo unaoibua mjadala baada ya kucheza michezo miwili ya kufuzu, ikifungwa mabao 2-0 na Guinea-Bissau, Septemba 25, 2026, kisha kupata sare ya bao 1-1 na Madagascar, Septemba 29, 2026.
Matokeo hayo yamewafanya baadhi ya wadau kuangalia zaidi tatizo lililopo ndani ya kikosi kuliko matokeo yenyewe, huku maeneo ya ushambuliaji, muunganiko wa wachezaji, ubora wa kikosi na maandalizi ya muda mrefu yakitajwa kuwa sehemu ya changamoto.
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua, amesema moja ya matatizo makubwa yanayoonekana ni matumizi mabaya ya nafasi za kufunga, akitaka timu kutumia muda uliopo kufanya maboresho kabla ya AFCON.
“Ni kweli timu bado inahitaji maboresho zaidi ili tuendane na ushindani mkubwa tutakaokutana nao mbeleni. Mechi hizi mbili ziwe sehemu ya kujiandaa vizuri na kufanyia kazi tatizo kubwa la utumiaji wa nafasi za kufunga,” alisema Chambua.
Chambua pia amegusia eneo la golikipa, akisema Yona Amosi alionekana kuwa na mchecheto katika mchezo dhidi ya Madagascar, hasa wakati wa kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma.
Mbali na matumizi ya nafasi, Chambua amesema Stars bado inakosa muunganiko mzuri wa kiuchezaji, jambo linaloathiri utulivu wa timu.
Kwa mtazamo wake, changamoto hiyo inahitaji kufanyiwa kazi kwa pamoja na kocha mkuu, Miguel Gamondi pamoja na wachezaji katika nafasi zao.
Naye nyota wa zamani wa Stars, Said Maulid ‘SMG’, anaona sababu nyingine ya mwenendo huo inaweza kuwa wachezaji kucheza wakiona tayari Tanzania imefuzu AFCON kutokana na uenyeji.
“Nafikiri tungekuwa hatujafuzu moja kwa moja tusingeona kiwango hiki kinachoendelea kuonyeshwa au hata mabadiliko pia ya mara kwa mara yanayofanywa na benchi la ufundi,” alisema SMG.
Hata hivyo, SMG anaamini bado Stars ina ushindani na amependekeza kurejea kwa Mbwana Samatta ili kutoa uzoefu na motisha kwa wachezaji vijana.
Mchambuzi wa soka, Edward Kumwembe ‘Edo’, amesema kiwango cha timu hakiwezi kutenganishwa na ubora na mazingira ya wachezaji wanaounda kikosi.
Kwa mujibu wake, Tanzania inaweza kupiga hatua zaidi iwapo wachezaji wengi watapata nafasi ya kucheza katika ligi zenye ushindani mkubwa, hasa Ulaya.
“Tanzania inaweza kupiga hatua kubwa zaidi katika soka pale tu wachezaji wengi watakapopata fursa ya kwenda kucheza soka katika klabu mbalimbali kubwa hasa barani Ulaya,” alisema Edo.
Edo ametumia mfano wa AFCON iliyopita, akisema Tanzania ilikutana na mataifa yaliyokuwa na wachezaji wanaocheza katika baadhi ya klabu kubwa za Ulaya, jambo alilodai linaonyesha tofauti ya viwango vya ushindani.
Amesema Tanzania bado inategemea kwa kiasi kikubwa wachezaji wanaocheza ndani ya nchi, huku mataifa mengine yakiwa na wachezaji wengi wanaoshiriki ligi za juu barani Ulaya.
“Sisi bado tunawategemea wachezaji wetu wa Yanga, Simba na Azam, unataka Mudathir anayecheza Yanga afanane na mchezaji anayecheza Torino?” Alihoji.
Edo pia ametaja Guinea-Bissau kama mfano wa timu ambayo huenda ikaonekana ya kawaida kwa mtazamo wa baadhi ya mashabiki, lakini ina wachezaji wengi wanaocheza katika ligi za Ulaya.
“Hiyo Guinea-Bissau tunayoiona timu ya kawaida, asilimia 90 ya wachezaji wake wanacheza klabu za Ligi Kuu Ulaya, kwa nini isimfunge Nigeria?” Alihoji.
Hata hivyo, aliyekuwa mshambuliaji na kocha wa Stars, Abdallah ‘King’ Kibadeni, anaona timu ilizokutana nazo Stars si za kutisha, ingawa kiwango kilichoonyeshwa kinaonyesha bado kuna kazi ya kufanya.
Kwa upande wa Musa Hassani ‘Mgosi’, alisema si wakati wa kulaumiana, akitaka Serikali, TFF na Gamondi pamoja na wachezaji kupewa nafasi ya kutekeleza mipango yao kuelekea AFCON.
“Hakuna sababu ya kumlaumu mtu yeyote kuhusiana na matokeo ya timu hiyo. Serikali, TFF, Gamondi na wachezaji waachwe wafanyie kazi mpango kazi walionao kuelekea Afcon ijayo,” alisema Mgosi.Amesema anapotazama mwenendo wa Stars katika mashindano mbalimbali, ikiwemo AFCON iliyopita iliyofanyika Morocco na FIFA Series, anaona matokeo yake yanaridhisha, hasa kutokana na aina ya timu ambazo Tanzania imekutana nazo.
“Kwa kuangalia mwenendo wa Stars katika michuano mbalimbali ikiwemo Afcon iliyopita iliyofanyika nchini Morocco na FIFA Series, matokeo yake yanaridhisha hasa kwa kuwa imekutana na timu nyingine zenye historia kubwa katika soka,” alisema.
Mgosi pia amesema haamini kama Stars ingefanya vizuri zaidi iwapo ingekuwa chini ya kocha mwingine tofauti na Gamondi.
“Siamini kama Stars ingefanya vizuri zaidi kama ingekuwa inafundishwa na kocha mwingine yoyote tofauti na hiki kilichofanywa na Gamondi, tuache timu itengenezwe muda bado upo,” alisema.
Mjadala kuhusu hali ya Stars pia umeibua rekodi ya kocha mkuu Miguel Gamondi tangu alipoanza kuiongoza timu hiyo.
Gamondi aliyejiunga na Stars kwa mara ya kwanza Novemba 4, 2025, akikaimu nafasi iliyoachwa na Hemed Suleiman ‘Morocco’ kisha kukabidhiwa kikosi hicho rasmi Februari 16, 2026, ameiongoza katika jumla ya mechi tisa, ambapo kati ya hizo ameshinda moja, sare tatu na kupoteza tano.
Stars katika kipindi hicho imefunga mabao 13, huku idadi ya mabao iliyofungwa ikiwa pia 13. Hata hivyo, Gamondi ana uzoefu wa mashindano ya AFCON akiwa ameiongoza Stars kufika hatua ya 16 bora ya AFCON 2025, jambo ambalo TFF ililitaja wakati wa kumthibitisha rasmi Februari 2026.
Kocha huyo raia wa Argentina, alianza safari yake ndani ya Stars kwa kipigo cha mabao 4-3 dhidi ya Kuwait, Novemba 15, 2025, kabla ya Stars kufungwa 2-1 na Nigeria katika AFCON 2025. Stars ilipata sare mbili mfululizo dhidi ya Uganda na Tunisia, zote zikiwa za bao 1-1.