Taifa Stars kujiuliza kwa Harambee Stars
Mwandishi Wetu TIMU ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' leo itakuwa na jukumu moja la kuhakikisha inapata ushindi kwenye mchezo wake wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Kenya kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Mechi hiyo inayotambuliwa na kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ina taswira kuu mbili kwa vikosi vya timu hizo. Mosi, kupima uwezo wa vikosi vya timu hizo kabla ya mashindano ya Chalenji yatakayorindima jijini Kampala, Uganda kuanzia Novemba 24 hadi Desemba 8, pili kusaka kupanda kwenye vigezo vya ubora wa viwango vya Fifa. Kwa mujibu wa viwango hivyo, Tanzania ndiyo inayoshika mkia katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki ikiwa nafasi ya 134, Kenya 130, Burundi 128, Rwanda 122 na Uganda nafasi ya 86. Hii ni mechi ya kumi kwa nchi hizo kucheza katika jiji la Mwanza na mara ya mwisho zilikutana mwaka 2009, Kenya ilishinda 2-1. Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen ataingia kwenye mchezo huo akiwa na rekodi ya kushinda mechi moja na Gambia 2-1, akafungwa na Ivory Coast 2-0, akitoa sare tatu dhidi ya Msumbiji (1-1), Malawi (1-1) na Botswana (3-3) tangu alipochukua jukumu hilo kutoka kwa Jan Poulsen. "Tunataka kushinda mechi hii kama njia ya kutuongezea morali kabla ya kuelekea Uganda kushiriki mashindano ya Chalenji, uwezo wa kutimiza hilo upo kwani ndani ya muda huu mfupi wa mazoezi wachezaji wameonekana kuimarika," alisema Kim. Hata hivyo Kim leo atakuwa na kazi kubwa ya kuwatengeneza kisaikolojia wachezaji wake ili kuwarudisha mchezoni kutokana na baadhi yao kukumbwa na kashfa ya kupokea hongo na kupanga matokeo katika michezo ya Ligi Kuu. Nahodha Juma Kaseja wa Simba na msaidizi wake Aggrey Morris wa Azam walilazimika kuzikosa mechi za mwisho za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kutokana na kushutumiwa kupokea hongo na kucheza chini ya kiwango. Kaseja na Mrisho Ngassa walidaiwa kuchukua hongo na kucheza chini ya kiwango katika mechi ya Simba iliyofungwa 2-0 na Mtibwa Sugar, Morogoro. Huku uongozi wa Azam ukiwapeleka kwenye mikono ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mabeki wake Aggrey Morris, Erasto Nyoni na kipa Deogratius Munishi kwa madai ya kupokea hongo kwenye dhidi ya Yanga na pia katika mechi dhidi ya Simba. Meneja wa Taifa Stars, Taso Mukebezi akizungumzia suala hilo alisema suala la wachezaji kutuhumiwa kupokea hongo katika klabu zao halihusiani na timu ya taifa. "Tunajua kuwa wanashutumiwa, lakini hiyo haiwezi kumzuia kocha Kim kuwatumia wachezaji hawa kwenye mchezo huu pamoja na Kombe la Chalenji," Mukebezi aliimbia Redio One jana. Wadhamini wa Taifa Stars, Kilimanjaro Premium Lager nao waliwataka wachezaji kuonyesha nidhamu ya hali ya juu wakiwa kambini Mwanza na kuhakikisha wanapata ushindi mechi dhidi ya Harambee Stars pamoja na Kombe la Chalenji. Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe ilisema wao kama wadhamini wana imani na timu ya taifa na kocha wake Kim Poulsen. ìMechi zilizochezwa mpaka sasa hivi tangu tumechukua udhamini zinaridhisha kwa kuwa tumeona kiwango cha timu kikikua siku hadi siku, tuna imani mechi ya Jumatano dhidi ya Harambee Stars tutashinda,î alisema Kavishe. Safu ya ushambuliaji wa Stars itaongozwa na washambuliaji wa TP Mazembe, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaotikisa kwa sasa barani Afrika kwa upachikaji mabao pamoja na John Bocco. Samata amefunga mabao sita kwenye Ligi ya Mabingwa na kuisaidia Mazembe kucheza nusu fainali ya mashindano hayo, lakini ameshindwa kuhamisha mafanikio yake hayo kwa timu ya taifa. Katika mchezo huo kocha Kim anatarajia kuwatumia vijana wengi zaidi ili kuwapa uzoefu chipukizi hao ambao ni Simon Msuva na Frank Domayo aliowapandisha kutoka katika timu ya vijana walio na miaka 20. "Miezi sita iliyopita nilichagua vijana kama Domayo na Msuva, watu walishangaa kutokana na uteuzi wangu, lakini vijana hao leo hii wanacheza mpira wa uhakika, hivyo vijana niliowateua nina hakika watafanya vema katika mechi zinazotukabili na watakuwa hazina ya nchi hii siku zijazo hivyo tuwape nafasi ya kulitumikia Taifa lao,"alisema Poulsen. Wakati huohuo, ndoto za wakazi wa Mwanza kumuona kiungo wa kimataifa wa Kenya na klabu ya Celtic, Victor Wanyama zimeyeyuka baada ya mchezaji huyo kushindwa kuungana na wenzake kutokana na kusumbuliwa na mafua. "Tulikuwa na saa 48 za kujiandaa kwa mchezo huu hivyo Wanyama na kipa Arnold Origi wameshindwa kuwahi kambini, kwa hiyo hawatakuwapo," alisema kocha Henri Michel wa Harambee Stars. Alisema,"ni matumaini yetu tutapata matokeo mazuri Tanzania, tumeshindwa kuwalazimisha Wanyama na Origi kuja hata kama hii ni mechi ya kalenda ya Fifa, kwa sababu tunataka kutengeneza uhusiano mzuri na klabu zao ili hapo baadaye tutapowahitaji kwa mechi muhimu zaidi waweze kuja." Michel alisema," lengo langu ni kuhakikisha Kenya inafuzu mashindano yajayo ya Afrika baada ya mashindano yatakayofanyika Afrika Kusini, hivyo ni lazima tuhakikishe tunapata matokeo mazuri kuanzia sasa."