SMZ kuibua sheria za soka la watoto
Muktasari:
- Hatua hiyo ni sehemu ya harakati za siku 16 za kupinga vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto, ikiwa na lengo la kubaini na kutatua changamoto zinazojitokeza katika akademi za soka ili kuhakikisha watoto wanakuwa katika mazingira salama wanaposhiriki michezo.
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMS) kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, imesema itakutana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) pamoja na wadau wanaomiliki akademi za soka kwa ajili ya kutengeneza miongozo na sheria zitakazolinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Hatua hiyo ni sehemu ya harakati za siku 16 za kupinga vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto, ikiwa na lengo la kubaini na kutatua changamoto zinazojitokeza katika akademi za soka ili kuhakikisha watoto wanakuwa katika mazingira salama wanaposhiriki michezo.
Waziri, Dk Saada Mkuya Salum, alieleza hayo wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo uliofanyika katika ukumbi wa Nyumba za Wazee, Sebleni, mjini Unguja.
Amesema hatua hiyo inalenga kuzuia uwezekano wa watoto wanaojihusisha na michezo kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na viongozi au watu wanaosimamia klabu na vituo vya kukuza vipaji.
“Mpango huu utahusisha Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo ili kuweka miongozo na utaratibu utakaowawezesha watoto kushiriki michezo bila kuathiriwa,” amesema.
Dk Saada amesema uamuzi huo umetokana na ongezeko la hamasa kwa watoto wengi Zanzibar kujiunga na michezo mbalimbali, ikiwemo soka, jambo linalohitaji kuwepo kwa mifumo madhubuti ya kuwalinda.
Amesema pamoja na kuendelea kuhamasisha uanzishwaji na uendeshaji wa akademia hizo, Serikali inalenga kuhakikisha vitendo vya udhalilishaji vinazuiwa ili watoto wakue katika mazingira bora na salama.
“Tumeshazungumza na Jeshi la Polisi kupitia madawati yake na mchakato unaendelea. Wale watakaobainika kuwa na hatia watafikishwa katika vyombo vya sheria. Tutaendelea kulihusisha Jeshi la Polisi katika kutekeleza mikakati yetu,” amesema.