Singida BS yaishushia kipigo Azam FC Ligi Kuu
Muktasari:
- Ushindi wa mabao 4-2 wa Singida Black Stars ilioupata uwanjani hapo umeifanya ivunje rekodi iliyoanza kuwekwa na Mbeya City, Novemba 7, 2013 na kisha Namungo FC, Oktoba 27, 2023.
SINGIDA Black Stars imevunja rekodi ya Namungo FC na Mbeya City katika Ligi Kuu ya NBC kwa kuwa timu iliyofunga idadi kubwa zaidi ya mabao dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Azam Complex leo Ijumaa, Novemba 21, 2026.
Ushindi wa mabao 4-2 wa Singida Black Stars ilioupata uwanjani hapo umeifanya ivunje rekodi iliyoanza kuwekwa na Mbeya City, Novemba 7, 2013 na kisha Namungo FC, Oktoba 27, 2023.
Katika mechi dhidi ya Mbeya City, Novemba 7, 2013, timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3 na katika mechi ya Oktoba 27, 2023, Namungo FC iliichapa Azam FC mabao 3-1 katika uwanja huo wa Azam Complex.
Kwenye mechi ya leo, Azam FC ndio ilitangulia kupata bao katika dakika ya 27 kupitia Feisal Salum kwa mkwaju wa penalti na kisha Zidane Sereri akaongeza la pili katika dakika ya 29.
Emmanuel Keyekeh aliifungia Singida Black Stars bao la kwanza katika dakika ya 40 na timu hizo kwenda mapumziko huku Azam ikiongoza kwa mabao 2-1.
Kipindi cha pili kilionekana kuwa kigumu zaidi kwa Azam FC kwani ilifanya makosa mengi yaliyowagharimu katika mchezo huo.
Singida Black Stars iliyoingia katika kipindi cha pili ikiwa kama mbogo aliyejeruhiwa, ilipata bao la kusawazisha kupitia James Mwashinga katika dakika ya 60.
Aliyeimaliza Azam katika mechi ya leo ni Jonathan Sowah ambaye alipachika mabao mawili katika dakika ya 68 na 72 ambayo yaliamua matokeo ya mchezo huo.
Singida Black Stars ingeweza kuondoka na ushindi mnono wa mabao matano iwapo ingepata mkwaju wa penalti ambao Keyekeh alipiga na kukosa baada ya kupanguliwa na kipa wa Azam FC, Zuberi Foba katika dakika ya 65.
Kichapo cha leo kimeifanya Azam FC kubaki katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi na pointi zake 23.
Singida Black Stars imepanda hadi katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikifikisha pointi 17.