Simba yashindwa kutamba nyumbani CAFCL
Muktasari:
- Matokea hayo ya Simba yameendeleza mwanzo mbaya wa timu za Tanzania katika mashindano ya kimataifa wiki hii baada ya Yanga, Azam FC na Singida Black Stars kupoteza mechi zao za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho msimu huu wa 2026-2027.
VINARA wa Ligi Kuu Bara, Simba imeshindwa kushikiria bomba kwa dakika 90, baada ya kuiruhusu Orland Pirates kutoka nyuma kwa mabao 2-0 kipindi cha kwanza hadi kumalizika mechi kwa sare ya 2-2 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Matokea hayo ya Simba yameendeleza mwanzo mbaya wa timu za Tanzania katika mashindano ya kimataifa wiki hii baada ya Yanga, Azam FC na Singida Black Stars kupoteza mechi zao za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho msimu huu wa 2026-2027.
Licha ya sare hiyo, Simba imesahihisha makosa iliyofanya msimu uliopita katika michuano hiyo, kwani ilianza kwa kichapo cha bao 1-0 nyumbani dhidi ya Petro de Luanda ya Angola.
Simba ambayo huu ni msimu wa tisa kushiriki hatua ya makundi ya mashindano ya CAF ngazi ya klabu tangu mfumo wa Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho ulipobadilishwa, imekuwa na matokeo mchanganyiko katika michezo yake ya kwanza, huku rekodi zikionyesha kuanza kwa matokeo mazuri si dhamana ya kumaliza vizuri hatua hiyo.
Katika mechi yake ya kwanza ya hatua ya makundi msimu huu, Simba ilikuwa na mwanzo mzuri dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini, lakini ilishindwa kulinda uongozi wa mabao mawili na kulazimika kugawana pointi katika mchezo huo.
Wekundu wa Msimbazi walianza kushambulia mapema kwa kupata bao la kwanza dakika ya 10 kupitia Libasse Gueye aliyemalizia pasi ya Anicet Oura.
Dakika ya 41, Simba ilipata bao la pili kupitia Antony Mligo aliyefuatilia mpira uliomponyoka kipa wa Orlando Pirates, Sipho Justin Chaine baada ya kudaka kona iliyochongwa na Gueye.
Hata hivyo, Orlando Pirates ilirejea kipindi cha pili kwa kasi na kuanza kulishambulia lango la Simba. Dakika ya 53, Tshepang Moremi aliifungia timu hiyo bao la kwanza kabla ya Simphiwe Selepe kusawazisha dakika ya 63, matokeo yaliyobadilisha kabisa mwelekeo wa mchezo.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kuendeleza rekodi yake ya kutokuwa na mwanzo wenye matokeo yanayofanana kila inaposhiriki hatua hiyo, kwani katika misimu iliyopita imewahi kuanza kwa ushindi, sare na hata vipigo, huku mwisho wa safari ukitofautiana.
Misimu minne Simba imeanza hatua ya makundi kwa ushindi ambayo ni 2018-2019, 2020-2021, 2021-2022 na 2024-2025, huku ikipoteza mara tatu msimu wa 2003, 2022-2023 na 2025-2026. Sare mbili msimu wa 2023-2024 na 2026-2027.
SINGIDA YALALA UGENINI
Wakati huohuo, Singida Black Stars imepoteza ugenini kwa mabao 2-0 dhidi ya AS Maniema na kuifanya kuanza kwa kichapo hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika.
Wenyeji walitumia vizuri kipindi cha kwanza kufunga mabao dakika ya 39 kupitia Edouard Tumbola akimalizia pasi ya Onoya Sangana na dakika ya 45, Beni Namboka alipohitimisha ushindi huo kwa pasi ya Obed Mbala.
Mapema Ijumaa, Azam ilipokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Ahli Tripoli huku Jumamosi Yanga ikifungwa bao 1-0 na MC Alger. Macho ya mashabiki yatakuwa mwishoni mwa wiki hii kuona zitafanya nini katika mechi zao za pili za hatua ya makundi.
Katika Ligi ya Mabingwa, Simba watakuwa ugenini kucheza dhidi ya Colombe, wakati Yanga waifuata Club Africans wakati katika Kombe la Shirikisho Azam atakuwa Afrika Kusini kucheza dhidi ya Durban City.