Simba, Yanga zamliza nahodha Gaborone United
Muktasari:
- Nyota huyo aliyefunga bao la kufutia machozi katika kichapo cha mabao 2-1 walichopokea kutoka kwa Yanga kwenye mechi ya marudiano ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Septemba 12, 2026, amesema soka la Tanzania linazidi kujitangaza zaidi.
NAHODHA wa Gaborone United, Lebogang Ditsele, amesema kwa misimu miwili mfululizo, timu za Simba na Yanga zimekatisha matumaini yao ya kufika hatua za mbele zaidi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, japo amezisifu kutokana na aina ya uwekezaji walioufanya.
Nyota huyo aliyefunga bao la kufutia machozi katika kichapo cha mabao 2-1 walichopokea kutoka kwa Yanga kwenye mechi ya marudiano ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Septemba 12, 2026, amesema soka la Tanzania linazidi kujitangaza zaidi.
Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Ditsele amesema kwa misimu miwili mfululizo ndoto za Gaborone katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika imekatishwa na Simba na Yanga, ingawa wanaendelea kujifunza ili kujiimarisha.
“Ilikuwa ni ngumu sana kwetu kucheza na timu za Simba na Yanga tena katika hatua hizi za awali za mtoano, wapinzani wetu wametupa funzo la kuamini kila kitu kinawezekana, ndio maana tumeonyesha ushindani ingawa hatujafikia malengo,” amesema.
Kiungo huyo amesema kutolewa hatua za awali ni jambo lililowaumiza kuanzia wachezaji, benchi la ufundi, viongozi wao na mashabiki, japo moja ya jambo wanaloendelea kulifanyia kazi ni namna bora ya kucheza mechi za aina ya mtoano.
Aidha, Ditsele amesema miongoni mwa wachezaji bora waliomvutia katika kikosi cha Yanga ni Maxi Mpia Nzengeli, kutokana na ubora wa nyota huyo hasa wakati wa kujua jinsi nzuri ya kusoma mchezo na kuchezesha timu hususani ikiwa inashambulia.
“Maxi ni mchezaji mzuri sana na naweza kusema ndiye aliyechangia kutuvuruga, alikuwa anafika kila eneo na hata akiwa na mpira alijua ni sehemu gani muhimu ya kuupeleka kwa wakati, kwangu nimevutiwa na kipaji chake alichonacho,” amesema.
Msimu wa 2025-2026, Gaborone iliishia pia hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchapwa na Simba 2-1, ikichapwa nyumbani bao 1-0, Septemba 20, 2025, kisha ugenini ikatoka sare ya 1-1, Septemba 28, 2025.
Ndoto ya kikosi hicho ikaendelea tena kudidimizwa na timu za Tanzania na safari hii msimu wa 2026-2027, imetolewa na Yanga hatua ya awali, ikitoka sare ya bao 1-1, Septemba 5, 2026, na marudiano ikachapwa 2-1.