Kasi ya Yanga yamchanganya kocha Gaborone United
Muktasari:
- Kauli ya kocha huyo aliitoa muda mchache baada ya kumalizika mchezo huo, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na Yanga kushinda mabao 2-1 na kufuzu hatua ya pili kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya ugenini kutoka 1-1.
KOCHA Mkuu wa Gaborone United ya Botswana, Sean Connor amesema kasi ya Yanga dakika 15 za mwanzo katika mechi ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliwavurugia hesabu zao, jambo lililosababisha wachezaji kuanza kwa kusuasua.
Kauli ya kocha huyo aliitoa muda mchache baada ya kumalizika mchezo huo, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na Yanga kushinda mabao 2-1 na kufuzu hatua ya pili kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya ugenini kutoka 1-1.
Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, kocha huyo raia wa Ireland ya Kaskazini, amesema kasi kubwa ya ghafla iliyoonyeshwa na Yanga dakika 15 hadi 20 za mwanzo, zilichangia kuvuruga kabisa mbinu zake alizokusudia kutumia.
“Tulitambua wazi wapinzani wetu watashambulia kwa nguvu sana kwa sababu wako nyumbani, ila hatukutegemea wangeanza kwa kasi dakika 15 hadi 20 za kwanza, kisaikolojia ilitunyima utulivu na kufanya makosa yaliyotugharimu mapema,” amesema Connor.
Amesema mashambulizi ya haraka ya Yanga yaliwanyima uhuru wachezaji wa timu hiyo kutokana na mwenendo wa makosa ya kujirudia yaliyowapa faida wapinzani wao, jambo lililosababisha kupata bao la mapema lililozidi kuwavuruga kimbinu.
“Kipindi cha pili kilikuwa kizuri kwetu tofauti na cha kwanza, ila tayari tulikuwa tumeshazidiwa kwa sababu wapinzani wetu muda huo wanacheza kimbinu kwa kuzuia na kushambulia kwa kushtukiza, nawapongeza wachezaji kwa walichokionyesha.”
Aidha, kocha huyo amesema walichofanikiwa wapinzani wao ni kutumia faida ya nyumbani tofauti na wao walivyocheza kwao Botswana, ingawa kila hatua wanazidi kujifunza namna bora ya kupambana na timu zenye wachezaji bora kama ilivyo Yanga.