Simba yairudisha chimbo JKT Tanzania
Muktasari:
- JKT Tanzania ina takribani siku 15 za kujiandaa na mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, baada ya kupoteza mbele ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Novemba 21, 2026.
KOCHA wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amesema kikosi chake kina maeneo kadhaa yanayohitaji kufanyiwa marekebisho kabla ya kukutana na Mashujaa Desemba 6, 2026 na watatumia muda walioupata baada ya mchezo dhidi ya Simba kuboresha kiwango chao.
JKT Tanzania ina takribani siku 15 za kujiandaa na mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, baada ya kupoteza mbele ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Novemba 21, 2026.
Muda huo utaitumia benchi la ufundi kufanya tathmini ya makosa yaliyojitokeza na kuimarisha kikosi kabla ya kukabiliana na Mashujaa ugenini.
Ahmad amesema licha ya kutopata matokeo waliyokuwa wakiyahitaji dhidi ya Simba, hana sababu ya kuwalaumu wachezaji wake kwa sababu walipambana na kutekeleza maelekezo waliyopewa, jambo lililowawezesha kupata bao.
“Hatuwalaumu vijana wetu kwa matokeo tuliyoyapata dhidi ya Simba kwa sababu wamefanya kazi yao. Ndiyo maana umeona tumefanikiwa kupata bao moja. Walijitahidi kupambana na kufanya kile tulichokuwa tumewaelekeza,” amesema.
Kocha huyo amesema baada ya kucheza na Simba, wamewapa wachezaji mapumziko ya siku mbili kabla ya kurejea mazoezini kuanza maandalizi ya mchezo dhidi ya Mashujaa, ambao amekiri hautakuwa rahisi kutokana na ubora wa wapinzani wao na ukweli kwamba watakuwa ugenini.
“Tumewapa wachezaji mapumziko ya siku mbili. Ingawa mchezo wetu unaofuata ni Desemba 6, bado tuna kazi kubwa ya kufanya kwa sababu tunakwenda kucheza na Mashujaa ugenini,” amesema.
Ameongeza kuwa benchi la ufundi linapanga kutumia muda uliopo kufanya mazoezi Dar es Salaam na kurekebisha upungufu kabla ya kusafiri kwenda Kigoma.
“Mashujaa ni timu ngumu na tunakwenda kucheza ugenini, kwa hiyo tunajua mchezo hautakuwa rahisi. Tutakuwa na maandalizi mazuri na tutafanya mazoezi hapa Dar es Salaam kabla ya kusafiri,” amesema.
Ahmad pia amegusia suala la safari ya kwenda Kigoma, akisema umbali wa eneo hilo ni jambo jingine wanalopaswa kulizingatia katika mipango yao ili kuhakikisha wachezaji wanafika wakiwa tayari kwa mchezo.
“Tunakoenda ni mbali, kwa hiyo lazima tuwe vizuri. Hatutaki kusafiri bila kuwa na maandalizi ya kutosha. Tutatumia muda tulionao hapa Dar kufanya mazoezi na kurekebisha makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo dhidi ya Simba,” amesema.
JKT Tanzania imecheza mechi 12 za Ligi Kuu Bara msimu huu, ikishinda tano, sare mbili na kupoteza tano, huku ikiwa na pointi 17 zinazoiweka nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi. Katika mechi hizo, timu hiyo imefunga mabao 14 na kuruhusu 16.
Mechi dhidi ya Mashujaa itakuwa kibarua kinachofuata kwa JKT Tanzania baada ya pambano lake dhidi ya Singida Black Stars lililokuwa limepangwa kufanyika Novemba 28, 2026 kuahirishwa kutokana na majukumu ya kimataifa ya wapinzani wao.