Kipimo kizito Msimbazi, JKT Tanzania yapania
Muktasari:
- Simba itaingia kwenye mchezo huo ambao utachezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo huko Mbweni ikiwa na rekodi ya kuvutia baada ya kushinda mechi zote 10 ilizocheza, ikikusanya pointi 30 kati ya 30 na kuongoza ligi.
HEKAHEKA za Ligi Kuu Bara zinaendelea tena leo, Jumamosi kwa michezo mitatu kupigwa huku macho ya mashabiki wengi yakielekezwa kwenye mchezo kati ya JKT Tanzania na Simba huku wageni hao wakiwa na dhamira ya kuendeleza ubabe wao na kusaka ushindi wa 11 mfululizo tangu kuanza kwa msimu huu.
Simba itaingia kwenye mchezo huo ambao utachezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo huko Mbweni ikiwa na rekodi ya kuvutia baada ya kushinda mechi zote 10 ilizocheza, ikikusanya pointi 30 kati ya 30 na kuongoza ligi.
Mafanikio hayo yanaonyesha uimara wa kikosi cha kocha Steve Barker katika kupata matokeo mazuri tangu mwishoni mwa msimu uliopita huku ushindi wa leo ukiwa na maana zaidi ya pointi tatu kwa sababu utaendeleza rekodi yake ya kutopoteza wala kutoka sare tangu kuanza kwa msimu wa 2026/27.
Hata hivyo, safari ya Simba kuelekea ushindi huo wa 11 haitakuwa ya rahisi, ikizingatiwa kuwa JKT Tanzania imekuwa na mwanzo mzuri unaoiweka nafasi ya nne ikiwa na pointi 17. Tofauti ya pointi 13 kati ya timu hizo inaonyesha utofauti uliopo kwenye msimamo, lakini haiondoi ushindani unaoweza kujitokeza uwanjani, hasa kwa JKT ambayo itakuwa na faida ya kucheza nyumbani.
Historia ya michezo baina yao inaipa Simba faida. Katika mechi 12 zilizopita, Wekundu wa Msimbazi wameshinda mara 11 huku JKT Tanzania ikiambulia ushindi mmoja pekee, bila timu hizo kutoka sare. Katika michezo hiyo, Simba imefunga mabao 21 dhidi ya matatu ya JKT.
Ushindi pekee wa JKT Tanzania katika rekodi hiyo ulipatikana Februari 7, 2020, ilipoifunga Simba bao 1-0. Tangu wakati huo, Simba imekuwa ikitawala dhidi yao, ikishinda michezo yote iliyofuata.
Hata katika mikutano mitano ya mwisho kwenye ligi, JKT imeshindwa kupata hata pointi moja, huku Simba ikishinda kwa mabao 1-0 katika michezo mitatu na 2-1 katika mwingine, jambo linaloonyesha kuwa imekuwa na uwezo wa kupata matokeo mazuri dhidi ya maafande hao.
Pamoja na historia hiyo, JKT Tanzania haitaingia kinyonge kwenye mchezo huu. Katika michezo yake mitano ya mwisho ya ligi, imeshinda mitatu, kutoa suluhu moja na kupoteza mmoja, ikifunga mabao sita na kuruhusu manne.
Ushindi dhidi ya Fountain Gate wa mabao 2-1, Mbeya City 2-1 na Kagera Sugar 1-0 unaonyesha kuwa timu hiyo ina uwezo wa kupata matokeo inapokuwa na mpangilio mzuri huku suluhu dhidi ya Dodoma Jiji ikionyesha pia kuwa inaweza kuwa na uimara wa kujilinda.
Changamoto kwa JKT imekuwa kutokuwa na mwendelezo wa matokeo mazuri. Baada ya kushinda dhidi ya Kagera Sugar, ilishindwa kupata ushindi dhidi ya Dodoma Jiji kabla ya kupoteza nyumbani kwa mabao 2-1 dhidi ya Azam.
Katika eneo la ushambuliaji, JKT italazimika kuwa na mipango zaidi ya kutegemea mashambulizi ya kushtukiza. Ili kuipa Simba wakati mgumu, itahitaji kutumia vizuri mipira inayopatikana katika maeneo ya pembeni, kuongeza kasi ya kupeleka mashambulizi mbele na kuhakikisha inakuwa na wachezaji wa kutosha katika eneo la mwisho. Hata hivyo, itahitaji kufanya hivyo bila kuacha nafasi kubwa nyuma, kwa sababu Simba imeonyesha uwezo wa kubadilisha haraka hali ya mchezo na kutumia mianya inayojitokeza katika safu za ulinzi za wapinzani.
Kwa upande wa Simba, ubora wake umeonekana zaidi katika uwezo wa kufunga mabao na kupata matokeo katika mazingira tofauti. Katika mechi zake tatu za mwisho za ligi, imefunga mabao 10 na kuruhusu matatu, ikishinda Mashujaa kwa mabao 6-1, Fountain Gate 1-0 na Namungo 3-2.
Katika mashindano yote, Simba imekuwa na mwendelezo mzuri zaidi. Katika michezo yake miwili ya mwisho ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya 15 de Agosto, ilishinda kwa jumla ya mabao 9-1, ikipata ushindi wa 6-1 ugenini na 3-0 nyumbani.
Ukiunganisha matokeo hayo na michezo yake mitatu ya mwisho ya ligi, Simba imefunga mabao 19 na kuruhusu manne katika mechi hizo tano, jambo linaloonyesha ubora wa safu yake ya ushambuliaji na uwezo wa kupata matokeo katika mashindano tofauti.
Pamoja na ubora huo, safu ya ulinzi ya Simba ina eneo ambalo JKT inaweza kulitumia. Kuruhusu mabao mawili katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Namungo na bao moja katika ushindi wa 6-1 dhidi ya Mashujaa na 15 de Agosto kunaonyesha kuwa haijawa ikimaliza kila mchezo bila kuruhusu wapinzani kufunga.
WASIKIE MAKOCHA
Kocha wa Simba, Steve Barker, alikiri ugumu wa mchezo huo na kusema timu yake inahitaji kuendeleza kiwango ilichoonyesha kabla ya mapumziko ya ligi.
“Ni mechi ngumu na muhimu kwetu kwa sababu tunahitaji kuendelea kuonyesha kiwango chetu. Tumetoka kwenye mapumziko, hivyo tulikuwa na muda wa kufanyia kazi mambo kadhaa na tulikuwa na mechi za kirafiki ambazo naamini zimetujenga,” amesema na kuongeza;
“Nawakaribisha mashabiki wa Simba kwa ajili ya kuisapoti timu yao kabla ya kugeukia mashindano ya kimataifa ambapo tutaanza maandalizi ya kukabiliana na Orlando, ushindi utatufanya kuwa na morali zaidi kuelekea mechi hiyo.”
Kwa upande wake, kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, amesema wanatambua ukubwa wa kazi iliyopo mbele yao kutokana na ubora wa Simba, lakini wamejiandaa kukabiliana na changamoto hiyo.
“Hii ni mechi ngumu kama ambavyo imekuwa siku zote dhidi ya timu ambazo zimekuwa katika nafasi za juu. Sisi kama timu tumejiandaa na tunaamini tutakuwa na wakati mzuri, kwa sababu tunahitaji kufanya vizuri na kuendelea kusogea kwenye nafasi za juu,” amesema Ahmad.
Katika michezo mingine ya leo, Dodoma Jiji itakuwa mwenyeji wa Fountain Gate huku Pamba Jiji ikiikaribisha Coastal Union.