Simba noma yaamua kumfuata Luis Sauzi
Muktasari:
Hivi unavyosoma Mwanaspoti ni kwamba, Senzo yupo Afrika Kusini ambako pia ni kwao, lakini ikielezwa kubwa lililompeleka huko ni kumalizana na winga huyo aliyewatibulia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kwa bao lao lilowavusha UD Songo kwa faida ya bao la ugenini.
HUENDA Yanga hawakuamini zile taarifa zilizoripitiwa na Mwanaspoti juzi kati juu ya mabosi wa Simba kuingiza mkono kwenye usajili wa winga teleza wa UD Songo, Luis Jose Miquissone.
Lakini, ukweli ni kwamba Wekundu wa Msimbazi wamepania kumteka nahodha huyo wa UD Songo aliyekuwa akicheza kwa mkopo akitokea Mamelodi Sundowns iliyopo Ligi Kuu ya Sauzi (PSL).
Habari ambazo Mwanaspoti imezinyaka mapema jana asubuhi kuwa, mabosi wa Simba juzi usiku walikutana faragha na kumjadili Luis na kuelezana lazima atue Msimbazi hata kama watani wao, Yanga walikuwa kwenye hatua nzuri ya kumalizana naye baada ya kuzungumza naye mapema.
Inaelezwa kilichoamriwa ni Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Senzo Mazingisa kupanda pipa kwenda Afrika Kusini ikiwa ni baada ya kuzungumza naye kwa simu na kumwambia wakutane huko.
Hivi unavyosoma Mwanaspoti ni kwamba, Senzo yupo Afrika Kusini ambako pia ni kwao, lakini ikielezwa kubwa lililompeleka huko ni kumalizana na winga huyo aliyewatibulia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kwa bao lao lilowavusha UD Songo kwa faida ya bao la ugenini.
Katika mechi hiyo ya raundi ya awali, Simba ililazimisha sare ya 1-1 nyumbani baada ya suluhu ya ugenini na kutolewa, ikiwa ni fedheha kwani, kwani msimu uliopita iliishia robo fainali na mechi hiyo ni kati ya sababu zilizotajwa kumtemesha kibarua Kocha Patrick Aussems.
Taarifa zinasema katika kikao hicho kilichoongozwa na Mtendaji Mkuu wa zamani wa Simba, Crescentius Magori na vigogo wengine waliamua kwa pamoja kumuwahi Luis mapema Sauzi na kumalizana naye wakati Yanga wakimsubiri jijini Dar es Salaam aje ili wamsainishe mkataba.
Ikumbukwe kuwa, Simba ndiyo iliyokuwa klabu ya kwanza kutajwa kumtaka winga huyo, ili kuziba nafasi ya Emmanuel Okwi, lakini haikumtilia nguvu hadi Yanga ilipotajwa kuzungumza naye ili awahi mapema pambano la watani litakalopigwa Januari 4.
Simba imeuangalia mpira mwingi wa Luis na ile mikrosi yake, kisha ikaangalia namna Yanga inavyosajili vifaa vya maana, akiwamo Ditram Nchimbi, Tariq Seif na jana ikimalizana na Yikpe Gnamein, wakaona isiwe tabu na wakaamua kupambana kumzuia asitue huko ili aende Msimbazi.
Tangu dirisha dogo lifunguliwe Desemba 16, Simba haijasajili mchezaji yeyote, jambo linaloelezwa mipango yao ni kuvuta mashine mbili, moja winga na mwingine straika kutokana na bajeti yao ya Sh 76.8 zilizotangazwa kwenye Mkutano Mkuu wa Simba uliofanyika hivi karibuni.
Simba inahitaji straika wa kuongeza nguvu kwenye kikosi chake ambapo sasa ina washambuliaji wawili pekee wanaowategemea zaidi Meddie Kagere na John Bocco ambaye alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na majeraha.
Chanzo kutoka ndani ya Simba, kimesema kuna asilimia kubwa ya kumnasa mchezaji huyo hasa baada ya nyota huyo kudaiwa kukata mawasiliano na Yanga kutokana na kuahidiwa donge nono tofauti na lile la watani hao wa jadi.
“Jana (juzi Alhamisi) ndiyo hasa tumekamilisha mipango yote kwa kiwango kikubwa, mtendaji wetu amesafiri kwenda Afrika Kusini hivyo atamaliza hilo ingawa kuna bosi mwingine (jina tunalo) anashirikiana naye kuweka mambo sawa,” kilisema chanzo hicho ambacho ni mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba.
Senzo mwenyewe alipoulizwa akiwa Sauzi, alijibu kwa ufupi; “Nipo nyumbani na familia, mambo mengine ya kazi kama hayo yote uliyoniuliza nitayajibia muda si mrefu nitakaporejea Tanzania.”
Magori alipotafutwa kwa njia ya simu hakupatikana hewani kwani simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi na mwandishi hakuweza kutoa ushirikiano.