Simba isikubali kuingia mtego wa Rushine
Muktasari:
- Baadhi ya watu wakisema jamaa uwezo wake ni wa kawaida na sio beki mzuri kiasi hicho tofauti na sifa anazopewa na wengi tangu alipoanza kuichezea Simba.
NAONA kuna mjadala unaoendelea mitandaoni na kwenye vijiwe mbalimbali kumuhusu nahodha msaidizi wa Simba, Rushine de Reuck.
Baadhi ya watu wakisema jamaa uwezo wake ni wa kawaida na sio beki mzuri kiasi hicho tofauti na sifa anazopewa na wengi tangu alipoanza kuichezea Simba.
Na wanakuambia kabisa eti De Reuck anafichiwa makosa na beki mwenzake Ismael Toure ambaye kama asipokuwepo, safu ya ulinzi ya Simba inayumba.
Watu kutoa maoni yao sio jambo jambo la kushangaza lakini maoni hayo kufanyiwa au kutofanyiwa kazi na wahusika inabakia kuwa uamuzi binafsi wa wahusika ambao wanalengwa na maoni hayo.
Hapa kijiweni tunaamini Simba wasikubali kuingia katika mtego wa kuaminishwa Rushine ni beki wa kawaida maana wakikubali kufanya hivyo mwishowe watashawishika kumuacha.
Hadi sasa hao wanaotuaminisha De Reuck ana uwezo wa kawaida, hawajatupa uthibitisho wa kitakwimu wa angalau wastani wa makosa ambayo beki huyo wa zamani wa Mamelodi Sundowns anayafanya kwa mchezo.
Na bahati mbaya kwa vile wameamua kumtengenezea kidagaa jamaa, huwezi kuwasikia wakizungumzia maeneo ambayo De Reuck anaonyesha ubora na kuibeba timu yake.
Jamaa ni mtulivu, ni mzuri katika kusoma na kutibua mikimbio ya washambuliaji, ni kiongozi na anaweza kunusa hatari ya shambulizi kabla halijaleta madhara kwa golini kwake.
Mabeki kama Rushine de Reuck ni rahisi kuona hawana faida ukiwa nao kikosini lakini pale wanapoondoka ndipo unapojutia. Simba wasiruhusu hilo.