FVS yaliliwa Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- Usaidizi wa Video katika Mpira wa Miguu (FVS) inatumika Ligi Kuu Bara msimu huu 2026-2027 na inatajwa kuwa msaada mkubwa wa kuamua matukio yenye utata.
MFADHILI Mkuu wa Black Sailors, Juma Awadhi Khatib amelishauri Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) kuweka kifaa kisaidizi kwa waamuzi (FVS) ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
Usaidizi wa Video katika Mpira wa Miguu (FVS) inatumika Ligi Kuu Bara msimu huu 2026-2027 na inatajwa kuwa msaada mkubwa wa kuamua matukio yenye utata.
Kiongozi huyo alisema ili kuiboresha zaidi Ligi Kuu ya Zanzibar, ni vyema shirikisho hilo kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia, ikiwemo kuangalia namna ya kuweka kifaa hicho.
Alifafanua kifaa hicho kitawasaidia waamuzi kufanya uamuzi sahihi wakati wa michezo na kuondoa sintofahamu inayojitokeza kwa baadhi ya matukio.
"Hatua hii inaweza kusaidia kupunguza malalamiko kutoka kwa klabu na kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa mashindano ya ZFF," alisema kiongozi huyo.
Mbali na hilo, Juma alilishauri ZFF kuweka utaratibu wa kuzikutanisha klabu, kamati ya waamuzi na wasimamizi wa mashindano, kwa lengo la kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili ligi hiyo.
Alisema utaratibu huo utasaidia kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa wadau wa soka, huku wakiwa na lengo moja la kukuza na kuendeleza mpira wa miguu Zanzibar.
Sambamba na hilo, alilipongeza Shirikisho hilo kwa namna inavyoendelea kusimamia ligi na kuahidi Black Sailors itaongeza hamasa kwa mashabiki kufika uwanjani.