Simba hakuna kuremba

Muktasari:
- Wakati wachezaji wakielekea kwenye ukaguzi kabla ya kupanda ndege, Bocco alisema malengo yao ni kufanya vizuri hata kama baadhi ya nyota hawatakuwepo.
JESHI la Kocha Patrick Aussems limepaa jana jioni kwenda nchini Algeria kwa ajili ya kusaka ushindi ambao, unaweza kuipeleka Simba kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kikosi cha Simba kimeondoka kikiwa na wachezaji 20 pamoja na viongozi wakiongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Crescentius Magori lakini, kikimkosa straika wake matata Mganda, Emmanuel Okwi, ambaye hakuwa katika orodha ya wachezaji waliondoka kwenda kuikabili JS Saoura hapo Machi 9.
Okwi alikosekana katika mechi ya Ligi Kuu Bara, ambayo Simba walishinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Stand United, mabao yote yakifungwa na nahodha John Bocco.
Suala la Okwi kutosafiri na timu limeanza kuzua minong’ono, watu wanajiuliza imekuwaje? Na viongozi wa Simba akiwemo Kocha Msaidizi, Dennis Kitambi, alipoulizwa sababu ya straika huyo kuachwa, alisema hawezi kuzungumzia.
Hata Okwi mwenyewe alipotafutwa ili kujua sababu za kuachwa, alimtaka Mwandishi kuwauliza viongozi wa Simba kwa kuwa, lipo nje ya uwezo wake hivyo hawezi kulizungumzia.
Katika mchezo wa kwanza, Okwi alikuwa mwiba kwa mabeki wa JS Saoura, akitengeneza mabao mawili kwa Meddie Kagere huku mwenyewe akipachika moja na kuipa Simba ushindi wa mabao 3-0.
Wakati wachezaji wakielekea kwenye ukaguzi kabla ya kupanda ndege, Bocco alisema malengo yao ni kufanya vizuri hata kama baadhi ya nyota hawatakuwepo.
Alisema hilo la kukosekana kwa baadhi ya wachezaji halipo chini yangu kwani, kila mchezaji ambaye atapata nafasi ya kucheza atatimiza majukumu yake.
“Wachezaji tumepata muda wa kujiandaa vizuri na kwenda kushindana katika mechi na JS Saoura malengo yetu yakiwa ni kufanya vizuri.
“Tunafahamu tunakwenda kucheza na timu ambayo itakuwa imebadilika na si ile ambayo tulicheza nayo katika mechi ya kwanza hapa nyumbani.
“Wachezaji wote wana morali kubwa tunaomba Watanzania watuombee ili tufanye vizuri na kutimiza lile ambalo lipo katika mioyo yetu,” alisema Bocco.
Wachezaji 20, walioondoka ni Aishi Manual, Zana Coulibaly, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Mohammed Hussein, Pascal Wawa, Poul Bukaba, James Kotei, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga, Cletus Chama, Rashid Juma, Abdul Selemani, Bocco, Maddie Kagere, Adam Salamba.
Wengine Deo Munishi, Mohammed Ibrahim na kiungo fundi Haruna Niyonzima.
Mwanzo wa safari
Mwanaspoti ambalo lilitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 7:30 mchana lilimkuta Mjumbe wa Bodi, Mwina Kaduguda akiwa anasubiri msafara. Dakika 15 baadaye, alifika Magori ambaye alikuwa amevalia jinzi ya bluu, sweta la rangi nyeusi na koti la suti la rangi ya bluu huku akiwa na begi lake la kuburuza.
Saa 8:00 mchana gari ndogo ya kubebea wachezaji wa Simba aina ya Toyota Hiace lilifika huku likiwa na daktari Yassin Gembe, Mtunza Vifaa Hamis Mtambo, Meneja Patrick Rweyemamu, Mpishi Samuel Cyprian pamoja na mabegi ya wachezaji.
Saa 8:17 mchana kikosi cha Simba ndio kiliwasili uwanjani hapo na wa kwanza kushuka alikuwa Patrick Aussems na alifuatiwa na kocha msaidizi Denis Kitambi.
Wachezaji hawakushuka haraka, walikaa kwenye gari zaidi ya dakika 20, ndipo walishuka na wa kwanza kushuka alikuwa ni kiungo Mzamiru Yassin.
HOTELI YA MAANA
Msafara wa Simba ulitarajiwa kupitia Dubai na imeelezwa kuwa wakitua Algeria watafikia katika hoteli ya maana.
Imeelezwa kuwa kabla ya kwenda JS Saoura watakaa Algers kwa siku mbili kabla ya kuwafuata wapinzani wao siku moja kabla ya mchezo.
Simba watafikia katika hoteli ya kifahari ya Grouz mjini Algers.
Siku hizo mbili ambazo Simba watakuwa hapo watafanya mazoezi ya mwisho ili kuzoea mazingira na hali ya hewa ya nchini humo.
SIMBA KUTUMIA JAMHURI
Mara baada ya kumaliza majukumu ya michezo ya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika Simba wakirudi watatumia Uwanja wa Jamuhuri Morogoro.
Baada ya Uwanja wa Taifa kufungwa kwa ajili ya matengenezo maalumu uongozi wa Simba ulipewa nafasi ya kutafuta uwanja, ambao watautumia katika mechi zao za nyumbani na sasa wamechagua.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Kaduguda alisema uongozi umeupitisha uwanja huo kwa mechi zao za nyumbani za Ligi Kuu Bara mpaka hapa matengenezo na matumizi ya Uwanja wa Taifa yatakapokamilika.