Prime
Okello amuibua kocha Yanga
KIUNGO Allan Okello amerejea kwao Uganda kufanya maandalizi ya kujiunga na klabu yake mpya AS FAR Rabat ya Morocco lakini kocha wake mpya akachekelea usajili huo akidai amepata silaha ya maangamizi.
Yanga imefikia makubaliano na AS FAR Rabat kwa kumuuza Okello kwa dau la Dola 1.2 Milioni (Tsh 3.1 Bilioni), baada ya Waarabu hao kuwashinda wenzao wa Wydad Athletic ambao nao walikuwa wanamwania nyota huyo.
Okello baada ya dili hilo kukamilika, Yanga haikumtumia kwenye mchezo wa ligi uliopita dhidi ya Namungo ugenini, ikishinda 3-1 huku kiungo huyo akiwekwa jukwani ambapo jana akaelekea kwao kufanya maandalizi ya kwenda Morocco.
Okello msimu uliopita alifanikiwa kuifungia Yanga jumla ya mabao 14 na asisti nane akifanikiwa kuhusika kwenye jumla ya mabao 22 akifanikiwa kuwa mfungaji bora wa timu hiyo, akitumia miezi sita tu kuweka rekodi hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kocha wa AS FAR Rabat Pedro Goncalves amesema uongozi wa klabu yake umeshamjulisha juu ya kufanikiwa kumpata kiungo huyo akisema anasubiri kuungana naye ndani ya kikosi chake.
Pedro ambaye alifanya kazi na Okello kwa miezi sita wakiwa Yanga amesema Okello ni kiungo mzuri ambaye anajua namna ya kuwatengenezea nafasi washambuliaji ambapo kikosi chake kitakuwa kimepata kiungo waliyekuwa wanamtaka.
Kocha huyo raia wa Ureno amesema msimu ujao AS FAR Rabat ina malengo makubwa ya kufanya makubwa ambapo Okello ni mmoja wa mastaa bora ambao wameongezwa kwenye kikosi chake, wakitaka kuchukua ubingwa wa nchini humo na kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Nimejulishwa tayari na uongozi wa klabu kwamba kuna hatua nzuri kumpata Okello, nadhani utakuwa usajili mkubwa kumpata mchezaji bora kama huyu mwenye uwezo wa kutengeneza nafasi nyingi,”amesema Pedro.
“Kabla ya kufika hapa nilikuwa na Okello, kila mmoja hapo anajua namna alivyo na ubunifu mkubwa akiwa anacheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho, kuna wachezaji wengi wazuri wameongezwa hapa nadhani tutakuwa na timu imara zaidi.
“Ushindani hapa Morocco ni wa kiwango cha juu sana, unahitaji wachezaji ambao akili yao inawaza kwa haraka, unapotaka kuchukua ubingwa wa Morocco au kufika mbali kwenye mashindano ya Afrika ni lazima uwe na kikosi imara, hiki ndicho tunachopambana kufanya sasa.”