Sheikhan aahidi makubwa Singida
Muktasari:
- Singida Black Stars, ambayo msimu huu itaiwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, imeweka kambi nchini Rwanda ambako inashiriki michuano ya CECAFA Kagame kama sehemu ya maandalizi ya msimu wa 2026/27.
KIUNGO mpya wa Singida Black Stars, Sheikhan Khamis anaamini timu hiyo ina kila sababu ya kufanya vizuri katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao huku akisisitiza kuwa kwa sasa akili yake yote ipo kuitumikia klabu hiyo baada ya kujiunga kwa mkopo akitokea Yanga.
Singida Black Stars, ambayo msimu huu itaiwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, imeweka kambi nchini Rwanda ambako inashiriki michuano ya CECAFA Kagame kama sehemu ya maandalizi ya msimu wa 2026/27.
Sheikhan alisema michuano hiyo ni fursa muhimu ya kujenga maelewano ndani ya kikosi kabla ya kuanza kwa majukumu makubwa ya ndani na kimataifa, akiamini timu ina uwezo wa kufika mbali ikiwa itaendelea kufanya kazi kwa umoja.
“Kombe la Shirikisho ni mashindano makubwa, lakini tunaamini kila kitu kinawezekana. Kikubwa ni kufuata maelekezo ya benchi la ufundi, kufanya kazi kwa bidii na kupambana kwa ajili ya malengo ya timu,”.
Kiungo huyo alisema tangu alipowasili kambini Kigali amepokelewa vizuri na viongozi pamoja na wachezaji wenzake, jambo lililomsaidia kuanza haraka kuzoea mazingira ya timu hiyo.
“Nashukuru Mungu kwa kunifikisha hapa. Nimepokelewa vizuri sana na kila mmoja ndani ya timu. Kwa sasa akili yangu yote ipo Singida Black Stars na nataka kutoa mchango wangu kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea,” alisema.
Singida Black Stars ilianza vibaya michuano ya Kagame kwa kufungwa mabao 2-0 na Jamus SC, lakini ikafufua matumaini ya kutetea ubingwa baada ya kuichapa Mogadishu City mabao 4-1, matokeo yaliyoiweka kwenye nafasi ya kupigania tiketi ya hatua ya nusu fainali kupitia mchezo wa mwisho dhidi ya Simba.
Mbali na Kombe la Shirikisho Afrika, Singida Black Stars pia itashiriki Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB.