Serengeti Boys yapoteza kishujaa mbele ya Brazil, nafasi bado ipo
Muktasari:
- Bao pekee la Brazil lilifungwa dakika ya 15 na Richard Wendel baada ya shuti la Eduardo Conceicao kuzuiwa, mpira ukamwangukia Wendel aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kufunga. Brazil ilitumia nafasi hiyo kupata ushindi na kujihakikishia tiketi ya kufuzu hatua ya 32 bora ikiwa na pointi sita baada ya kushinda michezo yake miwili ya mwanzo.
SERENGETI Boys imepokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Brazil katika mchezo wa pili wa Kundi I wa Kombe la Dunia la FIFA chini ya miaka 17 linaloendelea Qatar 2026, lakini pamoja na matokeo hayo, vijana hao wa Tanzania wameonyesha uwezo wa kupambana na moja ya timu zenye historia kubwa katika michuano hiyo.
Bao pekee la Brazil lilifungwa dakika ya 15 na Richard Wendel baada ya shuti la Eduardo Conceicao kuzuiwa, mpira ukamwangukia Wendel aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kufunga. Brazil ilitumia nafasi hiyo kupata ushindi na kujihakikishia tiketi ya kufuzu hatua ya 32 bora ikiwa na pointi sita baada ya kushinda michezo yake miwili ya mwanzo.
Pamoja na kupoteza mchezo huo, Serengeti Boys ilionyesha mchezo mzuri dhidi ya Brazil. Kipa Haji Abdalah alikuwa miongoni mwa wachezaji walioipa Tanzania matumaini ya kusawazisha matokeo baada ya kufanya baadhi ya michomo muhimu iliyozuia Brazil kuongeza mabao.
Hata hivyo, matokeo hayo yameifanya Tanzania kubaki na pointi moja baada ya michezo miwili, ikishika nafasi ya tatu kwenye kundi hilo ikiwa na tofauti ya mabao.
Bado kundi lipi wazi kwani Brazil pekee hadi sasa ndio imefuzu Ireland ina pointi tatu, Tanzania na Costa Rica zikikusanya moja.
Pointi hiyo moja bado inaipa nafasi ya kufuzu
na matumaini hayo yapo kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Jamhuri ya Ireland itakayopigwa Novemba 27 saa 11 jioni.
Mchezo huo sasa ni kama fainali kwa vijana hao, kwani ushindi utawapa pointi nne na kuwaweka kwenye nafasi nzuri ya kumaliza ndani ya timu mbili za juu katika kundi hilo, kutegemea matokeo ya Brazil dhidi ya Costa Rica. Tanzania inahitaji kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika mechi zilizopita, hasa kutumia nafasi za kufunga na kuwa makini katika ulinzi ili kuepuka kuruhusu mabao ya mapema.
Kwa upande wa nafasi ya kufuzu, mfumo wa mashindano unaipa Tanzania matumaini zaidi. Timu mbili za juu kutoka kila kundi zinaingia moja kwa moja hatua ya 32 bora, huku timu nane bora zilizomaliza nafasi ya tatu zikikamilisha idadi ya timu 32 zitakazoendelea. Hivyo, hata kama Tanzania haitamaliza nafasi mbili za juu, bado inaweza kufuzu kupitia nafasi ya tatu.