Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serengeti boys yaondolewa kiume kombe la dunia, Mourinho akishuhudia jukwaani

Muktasari:

Serengeti Boys imeondolewa mashindanoni mbele ya kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho ambaye alikuwa jukwaani akishuhudia mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Aspire Academy Field 1.

Safari ya Serengeti Boys katika fainali za Kombe la Dunia la FIFA U-17 linaloendelea  Qatar 2026 imeishia hatua ya makundi baada ya leo Novemba 27, 2026 kuchapwa mabao 3-1 na Jamhuri ya Ireland katika mchezo wa mwisho wa Kundi I, matokeo yaliyoiwezesha timu hiyo kuungana na Brazil kufuzu hatua ya mtoano ya 32 bora.

Serengeti Boys imeondolewa mashindanoni mbele ya kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho ambaye alikuwa jukwaani akishuhudia mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Aspire Academy Field 1.

Serengeti Boys iliyoingia kwenye mechi hiyo ikiwa na matumaini ya kutumia nafasi ya mwisho kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu, ilijikuta ikianza vibaya baada ya Cillian Murphy kufunga bao la kwanza dakika ya sita, kabla ya Luqman Mbalasalu kurejesha matumaini kwa Watanzania kwa kusawazisha dakika ya 18.

Hata hivyo, furaha ya Tanzania haikudumu kwa muda mrefu, kwani Murphy alifunga bao lake la pili dakika ya 26 na kuirejesha Ireland mbele kwa mabao 2-1, kabla ya Desmond Armstrong kuongeza la tatu dakika ya 31 na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa na faida ya mabao mawili.

Matokeo hayo yalihitimisha nafasi Tanzania ambayo ilihitaji ushindi ili kuongeza matumaini ya kusonga mbele, lakini licha ya juhudi za kutafuta mabao ya kurejea mchezoni.

Katika mechi zake mbili zilizopita, Serengeti Boys ilianza kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Costa Rica Novemba 21, 2026 kabla ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Brazil Novemba 24, 2026. Hivyo, katika michezo yake mitatu ya Kundi I, Tanzania imekusanya pointi moja tu, ikifunga mabao matatu na kuruhusu mabao sita.

Wakati Tanzania ikiaga mashindano, Brazil nayo ilimaliza kazi yake kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Costa Rica, matokeo yaliyoifanya imalize hatua ya makundi ikiwa na pointi tisa na kufuzu kama kinara wa Kundi I. Ireland imefuata ikiwa na pointi sita baada ya kushinda michezo miwili na kupoteza mmoja, huku Tanzania na Costa Rica zikibaki na pointi moja kila moja.

Mfumo wa mashindano hayo una timu 48 zilizogawanywa katika makundi 12, ambapo timu mbili za juu kutoka kila kundi zinafuzu moja kwa moja hatua ya 32 bora, huku nafasi nyingine nane zikichukuliwa na timu bora zilizomaliza nafasi ya tatu. Timu hizo hupangwa kwa kuzingatia pointi, tofauti ya mabao, idadi ya mabao yaliyofungwa, nidhamu na droo endapo vigezo vingine vitashindwa kutenganisha timu.

Kwa Tanzania haina matumaini ya kutumia nafasi hiyo kutokana na pointi moja iliyoikusanya. Hata Vietnam iliyomaliza nafasi ya tatu Kundi G ikiwa na pointi moja na tofauti ya mabao -3, imefunga mabao matano, mawili zaidi ya Tanzania, hivyo Serengeti Boys inakuwa nyuma yake kwenye kigezo cha mabao yaliyofungwa. Hiyo inamaanisha safari ya vijana hao imeishia hatua ya makundi, huku Brazil na Ireland zikiendelea na vita ya kuwania taji hilo.

UGANDA, MALI ZAFUZU

Wakati Serengeti Boys ikiaga mashindano, mataifa mengine ya Afrika yameendelea kupeperusha bendera ya bara hilo baada ya Uganda, Mali, Misri, Msumbiji, Senegal, Ivory Coast na Morocco kufuzu hatua ya mtoano moja kwa moja.

Uganda imekuwa miongoni mwa zilizovutia zaidi baada ya kuichapa New Caledonia mabao 6-0, ushindi ulioipa nafasi ya pili Kundi B ikiwa na pointi sita, huku nahodha Owen Mukisa akifunga hat-trick na Joseph Dorongin, Isima Magala na Junior Ofoyrwth wakiongeza mabao mengine. Ushindi huo uliifanya ipite Ecuador kwa tofauti ya mabao na kuungana na Korea Kusini katika hatua inayofuata.

Mali nayo imeonyesha ubora kwa kumaliza kinara wa Kundi G ikiwa na pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu, ikiwemo ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Vietnam kupitia Sanaba Keita na Djigui Koita. Senegal imefuzu baada ya kumaliza nafasi ya pili Kundi F, ikitoka sare ya bao 1-1 na Tajikistan katika mchezo wa mwisho, wakati Misri ilipata tiketi kwa kuichapa Panama mabao 4-1 na kumaliza ya pili Kundi A. Msumbiji ilijihakikishia nafasi ya mtoano baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Australia na kumaliza ya tatu Kundi C, huku Ivory Coast ikiichapa Jamaica 3-1 na Morocco nayo ikafuzu kupitia matokeo yake ya awali. Hivyo, Afrika imepata wawakilishi saba katika hatua hiyo, huku Serengeti Boys ikiwa miongoni mwa timu zilizoishia hatua hiyo.