Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serengeti Boys na dakika 90 za kuandika historia mpya Qatar

SERENGETI Pict

Muktasari:

  • Serengeti Boys hadi sasa iko nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi hilo ikiwa imekusanya pointi moja iliyoipata kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Costa Rica, kisha ikapokea kipigo chembamba cha bao 1–0 mbele ya mabingwa mara nne wa michuano hiyo Brazil.

NI leo siku ya kihistoria kwa vijana wa Tanzania U-17, Serengeti Boys ambao watakuwa Uwanja wa Aspire Zone saa 11 kamili jioni, kuminyana na Jamhuri ya Ireland katika mechi ya mwisho ya kundi I itakayoamua hatma ya kufuzu hatua ya 32 bora.

Hii si mechi ya kukamilisha ratiba; ni dakika tisini za kutafuta ushindi utakaoipa tiketi ya kihistoria ya kucheza hatua ya 32 Bora kwa mara ya kwanza.

Serengeti Boys hadi sasa iko nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi hilo ikiwa imekusanya pointi moja iliyoipata kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Costa Rica, kisha ikapokea kipigo chembamba cha bao 1–0 mbele ya mabingwa mara nne wa michuano hiyo Brazil.

Sasa pointi hiyo ina faida kubwa kwenye kundi hilo kama Serengeti itaondoka na ushindi katika mechi hiyo ambayo inatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa.


SERE 01

TAKWIMU ZA MECHI MBILI

Lipo somo kubwa ambalo benchi la ufundi chini ya kocha Elieneza Nsanganzelu linapaswa kulifanyia kazi kabla ya kipenga cha kwanza dhidi ya Ireland. Katika mechi mbili, Tanzania imetengeneza jumla ya mashuti 38, mashuti 25 dhidi ya Costa Rica na 13 dhidi ya Brazil.

Hii ni idadi kubwa inayothibitisha kuwa vijana hao wana uwezo wa kufika kwenye lango la mpinzani. Tatizo liko kwenye umaliziaji: kati ya mashuti hayo 38, ni mashuti saba yaliyolenga lango, huku mashuti 25 yakitoka nje.

Safu ya mabeki imeonyesha ukomavu wa hali ya juu ikishatulia. Mabao yote matatu tuliyofungwa katika mashindano hayo yalifungwa ndani ya dakika 15 za kwanza, dakika ya nane na 15 dhidi ya Costa Rica, na dakika ya 15 dhidi ya Brazil.

Baada ya hapo, ukuta wa Hussein Ally Mbegu, Kassim Selemani, Elick Yusuph na Idrisa Kilendemo, ulilindwa vyema na mikono salama ya kipa Haji Ally Abdalah aliyeokoa michomo minne mikali dhidi ya Brazil, haukuruhusu bao lolote kwa dakika 150 mfululizo.

Hii ina maana kuwa Serengeti ikivuka robo saa ya kwanza salama dhidi ya Ireland, mchezo unakuwa upo mikononi mwao.


SERE 02

IRELAND WANAPIGIKA VIPI?

Je, Ireland wanapigika vipi? Ukizitazama mechi zao mbili walipofungwa 2–1 na Brazil kisha kushinda 2–0 dhidi ya Costa Rica  utagundua kuwa Ireland ni timu inayopenda kucheza kwa mipira ya moja kwa moja  katika mfumo wa 4-4-2.

Wanapokutana na timu inayomiliki mpira kwa pasi fupi fupi kama walivyofanya Brazil, Ireland hupoteza mwelekeo walikuwa na umiliki wa asilimia 41 tu na pasi zao zilipotea kwa asilimia 26.

Hapa ndipo Issa Mussa Chole na Sadam Hamis wanapopaswa kuonyesha ubora wao. Tanzania ina wastani wa umiliki wa mpira wa asilimia 53.5 katika mashindano hayo, ukiwanyima Ireland mpira katikati ya uwanja, watachoka na kufungua njia za pembeni ambako Brazil iliwaadhibu mara mbili.

SERE 04
SERE 04

Aidha, ufunguo mwingine wa ushindi ni kuwakata makali nyota wao wawili: Cillian Murphy na Ryan Sheridan. Mabao yote matatu ambayo Ireland imefunga  yamepitia miguuni mwao  Murphy akitoa pasi za mabao mawili na kufunga moja, huku Sheridan akifunga moja na kutoa pasi moja. Viungo wakabaji wakiwaweka wawili hawa kwenye mfuko na kuzuia pasi za kupenya katikati ya mistari, Ireland itabaki ikipiga mipira mirefu isiyo na macho.

Kisha, kazi ibaki kwa Faraji Kayanda, Razaki Mbegelendi na Abel Samson kuimaliza kazi mbele ya lango. Kayanda tayari ameshaonyesha kuwa ana uwezo wa kuamua mechi kubwa baada ya kufunga mabao mawili dhidi ya Costa Rica.

Ushindi wowote dhidi ya Ireland unafikisha pointi nne, na kuifanya Serengeti kusogea juu ya Ireland wenye pointi tatu, na kufungua mlango mpana wa kuingia 32 Bora, aidha kama washindi wa pili wa kundi au kupitia mlango wa timu nane bora zilizoshika nafasi ya tatu.

Tayari vijana hao wamethibitisha kuwa wana vipaji, wana pumzi na wana uzalendo. Kilichobaki leo ni utulivu mbele ya lango na umakini wa dakika zote 90.


SERE 03

MECHI ZINGINE

Mbali na mchezo wa Serengeti Boys dhidi ya Ireland, mechi nyingine saba za hatua ya makundi ya Kombe la Dunia zitaikutanisha Costa Rica dhidi ya Brazil linalotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa. Costa Rica iliyopo mkiani na pointi moja ina kibarua dhidi ya Brazil ambayo tayari imefuzu hatua ya 32 bora.

Katika mechi nyingine, Honduras itakutana na Japan, huku Colombia ikiwania pointi dhidi ya Serbia.Katika kundi J, Algeria itapambana na Jamhuri ya Dominican, wakati Chile itakuwa na kibarua dhidi ya Montenegro.

Mechi nyingine zitakuwa kati ya Venezuela na Mexico, huku Romania ikiikabili Cameroon katika kundi K. Michezo hiyo itakuwa muhimu kwa timu hizo katika kuwania nafasi za kufuzu hatua inayofuata ya mashindano hayo yanayoshirikisha mataifa 48.