Ninju atia neno, ashusha presha Kombe la Dunia U17
Muktasari:
- Ninju alisema wachezaji walipambana dakika zote 90 za mchezo, wakijaribu kufuata mpango wa benchi la ufundi, lakini katika soka matokeo yana pande tatu ambazo ni ushindi, sare na kipigo.
BEKI wa Timu ya Taifa ya vijana U-17 (Serengeti Boys), Abubakar Nizar Othman ‘Ninju’ amesema kikosi hicho kilijitahidi kutekeleza maelekezo ya kocha kwa asilimia 100 katika mchezo dhidi ya Brazil, lakini kilishindwa kutumia nafasi ilizozipata akiamini wana nafasi ya kufanya vizuri.
Ninju alisema wachezaji walipambana dakika zote 90 za mchezo, wakijaribu kufuata mpango wa benchi la ufundi, lakini katika soka matokeo yana pande tatu ambazo ni ushindi, sare na kipigo.
“Tulijaribu kufanya kile ambacho kocha alituagiza kuanzia mwanzo hadi mwisho, lakini hatukuweza kufunga mabao. Tulitoa kila kitu kwa asilimia 100. Haikuwa matokeo mazuri kwetu, lakini huo ndiyo mpira, kuna ushindi, sare na mshindwa,” alisema Ninju.
Kwa upande wake, kocha wa Serengeti Boys, Elieneza Nsanganzelu, alisema timu hiyo ilijaribu kuhimili ubora wa kiufundi wa Brazil, lakini ilikosa baadhi ya mambo madogo yaliyosababisha kuruhusu bao lililoamua mchezo huo. Hata hivyo, amesema anaamini kikosi hicho kitafanya vizuri zaidi katika mchezo ujao.
“Nadhani wameona kile tunachoweza kufanya. Unajua kiwango cha Brazil na kiwango chetu. Tulijaribu kuzuia uwezo wao wa kiufundi. Bila shaka tulikosa baadhi ya vitu vidogo na kuruhusu bao moja, lakini nina uhakika katika mchezo wa mwisho tutafanya vizuri zaidi,” alisema Nsanganzelu.
Kauli hizo zimekuja baada ya Serengeti Boys kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka Brazil katika mchezo wa Kundi I uliochezwa Novemba 24, licha ya kuonyesha upinzani dhidi ya moja ya mataifa yenye historia kubwa katika soka duniani.