Baraza aibuka na matumaini mapya Pamba Jiji
Muktasari:
- Timu hiyo ambayo msimu uliopita ilionyesha kiwango bora na kumaliza nafasi ya saba kwa pointi 36, msimu huu hali imeonekana tete na kufanya presha kuwa kali ndani na nje ya uwanja.
WAKATI Pamba Jiji ikisota na matokeo yasiyoridhisha, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Francis Baraza ametaja sababu za anguko, huku akitoa matumaini mapya akizipigia hesabu mechi nne za mzunguko wa kwanza.
Timu hiyo ambayo msimu uliopita ilionyesha kiwango bora na kumaliza nafasi ya saba kwa pointi 36, msimu huu hali imeonekana tete na kufanya presha kuwa kali ndani na nje ya uwanja.
Katika michezo 11 hadi sasa, timu hiyo ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza, imevuna pointi sita na kuwa nafasi ya 14 ikibakiza mechi nne kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Baraza raia wa Kenya amesema matokeo hayo aliyatarajia kutokana na pigo walilokutana nalo la kuondokewa na nyota wengi waliokuwa kikosi cha kuanza, lakini majeruhi kwa mastaa wake nayo imekuwa tatizo lingine.
Amesema sababu nyingine ni usajili wa nyota wengi (23) wapya ambao alitumia muda mwingi kutengeneza muunganiko akitoa matumaini tangu mchezo wao na Geita Gold waliposhinda 4-0, yapo mabadiliko kikosini.
“Kuna wachezaji wengine hadi sasa hawajaonja ladha ya mpira wa Ligi Kuu wakiendelea na majeraha, lakini nashukuru kwa sasa naona mabadiliko tangu tumerejea kambini kuendelea na maandalizi”
“Matumaini na matarajio yangu ni kuona mechi nne zijazo kufunga mzunguko wa kwanza tunataka pointi 12 ambazo zitatuondoa nafasi za chini na kukaa juu, hili linawezekana kwakuwa muunganiko umeonekana,” amesema Baraza.
Kocha huyo ameongeza, licha ya matokeo hayo kumuumiza, lakini hajakata tamaa kwa namna yoyote na baada ya michezo minne, mzunguko wa pili utakuwa wa mafanikio makubwa kwake.
“Niwaombe mashabiki na wadau waendelee kuwa watulivu, timu inaendelea kusukwa na baada ya mechi nne zijazo tukianza na Coastal Union, Namungo, Mbeya City na Kagera Sugar, tutakuwa pazuri” amesema kocha huyo.