Sababu nne kwa nini Alikiba Simba Day
Muktasari:
- Sasa katika tamasha hilo ambalo Simba imekuwa ikilifanya kila mwaka, huambatana na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wa muziki, vichekesho, maigizo na sanaa nyingine.
KESHO ndiyo kilele cha Simba Day na mashabiki, viongozi, wachezaji na benchi la ufundi wanakusanyika pamoja kusherehekea siku hiyo muhimu ya kuanza msimu mpya wa mashindano wa 2026/27.
Sasa katika tamasha hilo ambalo Simba imekuwa ikilifanya kila mwaka, huambatana na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wa muziki, vichekesho, maigizo na sanaa nyingine.
Simba Day 2026 msanii Alikiba ndiye staa mkuu atakayepafomu kwenye tamasha hilo ambalo ni la 17 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009.
Tamasha hilo limegeuka kuwa moja ya matukio makubwa ya michezo na burudani nchini. Mwaka huu macho yatakuwa kwa Alikiba, msanii mkuu wa usiku huo, baada ya Mbosso kuacha alama kubwa kwenye tamasha la mwaka jana.
Alikiba anatarajiwa kupafomu kwa mara nyingine kwenye tamasha hilo na kuna baadhi ya maswali yamekuwa yakiulizwa kwa nini yeye na si mwingine.
Jibu linaweza kuanzia kwenye historia yake ya muda mrefu kwenye muziki wa Tanzania na Afrika Mashariki.
Alikiba ni miongoni mwa wasanii waliojenga himaya kubwa ya mashabiki kwa zaidi ya miaka 10 akivuka mipaka ya kizazi kutokana na nyimbo zake zilizokubalika kwa watu wa rika tofauti. Hilo linampa nafasi ya kipekee kwenye tamasha kubwa linalokusanya mashabiki wa aina mbalimbali.
HISTORIA YA SIMBA DAY
Tangu ilipoanzishwa mwaka 2009, Simba Day imeendelea kukua na kubadilika kutoka tukio la kawaida la utambulisho wa kikosi hadi kuwa tamasha kubwa linalounganisha michezo na burudani.
Kila mwaka maelfu ya mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi hukusanyika kushuhudia utambulisho wa wachezaji wapya, benchi la ufundi na jezi za msimu mpya, huku burudani kutoka kwa wasanii maarufu ikiwa sehemu ya kivutio kikubwa cha siku hiyo.
Kadiri miaka ilivyopita, tamasha hilo limekuwa likivuka mipaka ya soka na kuwa jukwaa linalowakutanisha wadau wa michezo, burudani na familia za mashabiki wa Simba.
Hali hiyo imeifanya Simba Day kuwa moja ya matukio yanayosubiriwa kwa hamu kila mwaka kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa mashindano.
Ndiyo maana uchaguzi wa msanii mkuu umekuwa ukipewa uzito mkubwa na uongozi wa klabu.
Msanii anayepanda kwenye jukwaa la Simba Day anatakiwa kuwa na uwezo wa kubeba hadhira ya maelfu ya watu kwa saa kadhaa, kuimba moja kwa moja bila kuyumba na kuacha kumbukumbu itakayozungumzwa hata baada ya tamasha kumalizika.
Baada ya Mbosso kuonyesha kiwango kilichowavutia wengi katika Simba Day ya mwaka jana, macho ya mashabiki sasa yanaelekezwa kwa Ali Kiba.
Wengi wanaamini uzoefu wake wa miaka mingi, nyimbo zake zinazojulikana karibu kila kona ya Afrika Mashariki na uwezo wake wa kutawala jukwaa vinaweza kuifanya Simba Day 2026 kuwa moja ya matamasha yatakayobaki kwenye kumbukumbu za mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi kwa muda mrefu.
UHUSIANO
Moja ya sababu inayomfanya Alikiba kuwa chaguo la kwanza kwa Simba Day ni uhusiano wake wa karibu na klabu hiyo.
Msanii huyo amekuwa akijulikana kwa muda mrefu kama mmoja wa mashabiki maarufu wa Simba, jambo linaloifanya nafasi yake kwenye jukwaa hilo ionekane kuwa na maana zaidi kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi.
Pia amekuwa akishiriki kwenye matukio tofauti ya klabu hiyo, sababu ambayo inambeba mkali huyo kwa kiasi kikubwa.
Lakini zaidi ya mapenzi yake kwa Simba, Alikiba ana historia ya mashabiki wa Mnyama kupitia muziki. Wimbo wake ‘Mnyama’ umekuwa ukiteka hisia za mashabiki wa Simba na kuwa moja ya nyimbo zilizopokelewa kwa nguvu na wapenzi wa klabu hiyo.
FINALE IMECHANGIA
Miongoni mwa kolabo zilizofanya vizuri mwanzoni mwa mwaka huu ni pamoja na Finale, ngoma ya Bien aliomshirikisha King Kiba ikiwa imefanya vizuri kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
Ushirikiano huo umeongeza kuaminika kwa kiasi kikubwa na Simba tangu kutolewa Machi mwaka huu, wimbo huo umepokelewa vizuri ndani na nje ya Afrika Mashariki, ukiongoza chati mbalimbali za muziki na kukusanya mamilioni ya watazamaji kwenye YouTube ndani ya muda mfupi.
Bien mwenyewe ameeleza Finale ndiyo wimbo wake uliofanya vizuri zaidi tangu aanze kazi ya muziki kama msanii wa kujitegemea, akimpa sifa Alikiba kwa mchango wake mkubwa katika mafanikio hayo.
Hilo linazoweza kuwa moja ya sababu zilimfanya Ali Kiba kuwa chaguo la Simba Day 2026 kutokana na mwendelezo wa mafanikio yake kwenye muziki, hasa kupitia kolabo yake na mwanamuziki wa Kenya, Bien, katika wimbo Finale.
UWEZO WA KUPIGA ‘LIVE’
Mbali na historia yake kwenye muziki na umaarufu alioutengeneza kwa miaka mingi, uwezo wa Alikiba kuimba moja kwa moja (live) unaonekana kuwa miongoni mwa sababu zinazomfanya awe chaguo kubwa kwenye jukwaa la Simba Day.
Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, amekuwa akionyesha uwezo huo kwenye matamasha mbalimbali ya ndani na nje ya Tanzania, jambo lililomtengezea sifa ya kuwa mmoja wa wasanii wanaoweza kubeba jukwaa kwa sauti halisi na kuwafanya mashabiki waimbe naye kutoka mwanzo hadi mwisho wa onyesho.
Kwa tamasha kubwa kama Simba Day, linalotarajiwa kukutanisha maelfu ya mashabiki Uwanja wa Uhuru, uwezo wa kuwasiliana na hadhira ni jambo muhimu.
Alikiba ameonyesha mara kadhaa uwezo wa kuiongoza hadhira, kuibadilisha hali ya jukwaa na kuwashirikisha mashabiki kupitia nyimbo zake maarufu.
Hilo linaongeza imani kwamba anaweza kuifanya Simba Day 2026 kuwa moja ya matamasha yatakayokumbukwa, si kwa ukubwa wa jina lake pekee, bali kwa ubora wa maonesho yake ya moja kwa moja.