Rekodi ngumu inayozisubiri Simba, Yanga CAF
Muktasari:
- Simba na Yanga zimejikuta zikiangukia katika makundi yenye shauku ya visasi katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu wa 2026-2027, kutokana na droo iliyopangwa, japo moja ya jambo gumu ni kuandika rekodi mpya katika Michuano ya kimataifa.
DROO ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imewekwa hadharani juzi jijini Cairo, Misri, huku timu za Simba na Yanga ambazo ndio wawakilishi wa Tanzania zikijua rasmi wapinzani watakaokutana nao.
Simba na Yanga zimejikuta zikiangukia katika makundi yenye shauku ya visasi katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu wa 2026-2027, kutokana na droo iliyopangwa, japo moja ya jambo gumu ni kuandika rekodi mpya katika Michuano ya kimataifa.
Katika droo ya mashindano hayo iliyofanyika Oktoba 28, 2026, Yanga imepangwa kundi B, huku watani zao wa jadi, Simba ikiangukia kundi C.
Katika kundi B, Yanga imepangwa na Zamalek SC ya Misri, MC Alger ya Algeria na Club Africain ya Tunisia ambapo timu zote zimewahi kukutana miaka ya nyuma katika michuano ya kimataifa kwa maana ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa ni mechi za visasi.
Kwa upande wa Simba, imepangwa kundi C na timu za RS Berkane ya Morocco, Orlando Pirates FC ya Afrika Kusini ambazo zote zimeshawahi pia kukutana kwa nyakati tofauti na Colombe Sportive ya Cameroon ambayo ndio mara yao ya kwanza.
Wakati mashabiki wakiona Simba ina kundi jepesi zaidi linaloweza kuifikisha hadi fainali, ila rekodi zinaonyesha katika misimu sita ya Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika ni kundi A, B na C yametoa bingwa mmoja mmoja tu, huku kundi D, likitoa mabingwa watatu.
Kwa maana hiyo, kundi B na C ambalo Yanga na Simba zipo, kwa misimu sita iliyopita mabingwa wamepatikana mara moja moja tu, jambo linaloonyesha wawakilishi hao pekee wa Tanzania wana kazi ya kuandika rekodi mpya katika michuano hiyo.
Msimu wa 2020-2021, bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa ni timu ya Al Ahly ya Misri iliyoifunga Kaizer Chiefs FC ya Afrika Kusini mabao 3-0.
Kwa msimu huo, Al Ahly ilikuwa kundi A, ikimaliza nafasi ya pili na pointi 11, nyuma ya vinara, Simba iliyoongoza na pointi 13, huku AS Vita Club ya DR Congo ikiwa ya tatu na pointi saba na Al Merrikh SC ya Sudan ikiburuza mkiani na pointi zake mbili tu.
Msimu wa 2021-2022, Wydad Casablanca ya Morocco ilitwaa ubingwa kwa kuifunga Al Ahly ya Misri mabao 2-0, huku ikitokea kundi la D.
Katika msimu huo, Wydad iliongoza kundi D na pointi 15, ikifuatiwa na Petro De Luanda ya Angola iliyokuwa na pointi 11, huku Zamalek SC ya Misri ikiwa ya tatu na pointi nne na Sagrada Esperanca ya Angola ikiburuza mkiani, baada ya kukusanya pointi zake mbili.
Msimu wa 2022-2023, bingwa ni Al Ahly ya Misri iliyoifunga Wydad Casablanca ya Morocco kwa jumla ya mabao 3-2, hivyo, kuivua ubingwa huo iliouchukua msimu wake wa 2021-2022.
Katika msimu huo, Al Ahly ilikuwa kundi B, ikimaliza nafasi ya pili na pointi 10, sawa na za Al-Hilal Omdurman ya Sudan iliyomaliza ya tatu, nyuma ya vinara, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyokuwa na pointi 14, huku Coton Sport kutoka Cameroon ikiburuza mkia bila ya pointi zozote.
Msimu wa 2023-2024, Al Ahly ikatetea taji hilo baada ya kuifunga Esperance de Tunis ya Tunisia kwa jumla ya bao 1-0, ikitokea kundi la D.
Katika kundi hilo la D, Al Ahly iliongoza na pointi 12, ikifuatiwa na Yanga iliyokuwa ya pili na pointi nane sawa na za CR Belouizdad ya Algeria iliyomaliza ya tatu, huku Medeama SC ya Ghana ikiburuza mkia na pointi nne.
Msimu wa 2024-2025, Pyramids FC ya Misri ilitwaa taji hilo baada ya kuifunga Mamelodi Sundowns FC ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-2, huku kikosi hicho kikitokea kundi la D.