Patachimbika hapa

Wachezaji wa Yanga wakiwa mazoezini.
MWANDISHI WETU WAKATI pambano la Simba na Yanga likiwa linaanza leo Jumamosi, utakuwa tayari unajua matokeo ya mechi ya Manchester United dhidi ya Everton katika mechi ya Ligi Kuu England ambayo itakuwa tayari imekwisha. Lakini wakati wanaume hao wa Msimbazi na Jangwani wakianza pambano lao saa 10:00 jioni, itakuwa ni dakika ya 60 katika pambano la Chelsea na Arsenal katika Uwanja wa Stamford Bridge, jijini London. Sahau mechi hizo za majuu, jiandae kuangalia miamba miwili ya soka Tanzania ikiumana katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara. Neno rahisi unaweza kusema ‘Patachimbika hapa’. Kwa kawaida mapigo ya moyo ya binadamu huendana na kasi ya sekunde katika dakika, lakini kwa Watanzania wengi leo Jumamosi mapigo hayo yataongezeka kasi hiyo mara mbili. Simba inaingia uwanjani ikiwa inaongoza msimamo wa ligi hiyo kwa kuwa na pointi 27 wakati Yanga ikishika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 21. Yanga, ambayo imemtimua kocha wake Mganda, Sam Timbe na kumrejesha Kosta Papic wa Serbia, itataka kulipa kisasi kwa wapinzani wake baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 katika mchezo wa Ngao ya Hisani miezi miwili iliyopita. Kazi kubwa uwanjani itakuwa ni sehemu ya kati, kwani Yanga itakuwa ikiundwa na Juma Seif ‘Kijiko’ na Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ watakaopambana na viungo wa Simba; Jerry Santo, Patrick Mafisango na Shomari Kapombe. Raha hiyo haiwezi kuwa hapo tu, kwani mabeki wa Yanga; Godfrey Taita, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Chacha Marwa/Bakari Mbegu watakuwa na kazi nzito kukabiliana na mstari wa mbele wa Simba unaotengenezwa na Haruna Moshi ‘Boban’, Emmanuel Okwi na Felix Sunzu. Mabeki wa Yanga hawana budi kuwalinda vizuri, Sunzu na Okwi, ambao katika mechi iliyopita ndiyo walipeleka kilio katika makao makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Jangwani, Dar es Salaam. Hata hivyo mabeki wa Simba; Said Nasor Chollo, Juma Jabu, Juma Nyosso na Victor Costa, hawatalala kwani inabidi kuwachunga vizuri; Davies Mwape, Kenneth Asamoah na Hamisi Kiiza. Simba itamkosa beki wake wa kushoto, Amir Maftah, ambaye ni majeruhi, lakini wachezaji wengine wote wapo fiti. Yanga nayo itawakosa Stephano Mwasika na Shadrack Nsajigwa, lakini Davies Mwape amerejea baada ya kupona maumivu yake. Timu zote mbili zimefunga mabao 18, lakini ukuta wa Simba ukiwa umeruhusu mabao manne tu dhidi ya 10 ya Yanga. Mwamuzi wa pambano hilo ni Oden Mbaga ambaye anatambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).