Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Panga la Zahera labakisha hawa tu

Muktasari:

  • Chanzo cha ndani cha Yanga kimelidokeza Mwanaspoti kuwa, hadi sasa ni nyota hao tu ndiyo wenye uhakika wa kusalia kwa mujibu wa ripoti ya Kocha Zahera, huku ikielezwa mbali na viwango, lakini pia mikataba waliyonayo ndiyo iliyowabeba.

MPAKA sasa Yanga imeshawasaini majembe mapya wanne kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao kwa msimu ujao wa mashindano, lakini usichokijua ni kwamba Kocha Mwinyi Zahera ametembeza panga na kula vichwa kama vyote na ni nyota tisa tu ndiyo wenye uhakika wa kubaki Jangwani.

Mabosi wa Yanga wamewasainisha nyota wanne wa kigeni akiwamo Patrick Sibomana, Issa Bigirimana ambao ni mawinga, beki Lamine Moro na kiungo Abdul-Aziz Makame waliosaini mikataba ya miaka miwili kila mmoja kama ilivyokuwa kwa Papy Kabamba Tshishimbi aliyeongezewa mkataba klabuni hapo.

Sasa kama hujui ni kwamba, Yanga iliyomaliza msimu wa pili mfululizo mikono mitupu ilikuwa ikiundwa na kikosi cha wachezaji 28, ila kwa mujibu wa taarifa za ndani za timu hiyo ni nyota tisa tu wenye uhakika wa kuwepo msimu ujao akiwamo Kelvin Yondani.

Mbali na beki huyo mkongwe, wengine wenye uhakika wa maisha Yanga ya Mwinyi Zahera ni Juma Abdul, Paul Godfrey ‘Boxer’, Andrew Vincent ‘Dante’, makipa Ramadhan Kabwili na Klaus Kindoki na viungo Rafael Daud na Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Chanzo cha ndani cha Yanga kimelidokeza Mwanaspoti kuwa, hadi sasa ni nyota hao tu ndiyo wenye uhakika wa kusalia kwa mujibu wa ripoti ya Kocha Zahera, huku ikielezwa mbali na viwango, lakini pia mikataba waliyonayo ndiyo iliyowabeba.

“Hao ndiyo ambao wana uhakika, huku wengine kama Haji Mwinyi na Gadiel Michael, wakijadiliwa. Mwinyi anajadiliwa kutokana na kuonyesha kiwango cha hali juu katika mechi za mwisho wa msimu akichukua nafasi ya Gadiel Michael ambaye ni majeruhi,” chanzo kilisema na kuongeza Gadiel anajadiliwa kwa vile ameonyesha kiwango kabla ya kuumia na mkataba wake umemalizika, hivyo inahitajika yeye ama Mwinyi asalie kikosini.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa, Pius Buswita, Amissi Tambwe, Thabani Kamusoko, Beno Kakolanya, Said Makapu, Said Mussa, Matheo Anthony na Juma Mahadhi, Pato Ngonyani aliyepo kwa mkopo African Lyon huku mkataba wake ukimalizika na Burhan Akilimali ndiyo basi tena Jangwani, kwani hawapo kwenye mipango ya Zahera.

Huku Mrisho Ngasa, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Deus Kaseke, Jaffar Mohamed ambaye bado ana mkataba wamependekezwa kutolewa kwa mkopo na Mohamed Issa ‘Banka’ ambaye hajautumikia vyema mkataba wake kwani alikuwa kifungoni.

“Juu ya Yusuf Mhilu aliyepo kwa mkopo Ndanda ameonyesha kupandisha kiwango, ila mwalimu hajafurahishwa na kiwango chake akitaka abaki huko kama watamhitaji au wamtafutie timu nyingine, huku Maka Edward aliyegoma kutolewa kwa mkopo katika dirisha dogo ameshushwa timu ya vijana.

MSIKIE MWAKALEBELA

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alipoulizwa juu ya taarifa hiyo alisema mara baada ya kupata ripoti ya mwalimu wataweka wazi majina yote na wana mpango wa kuwafanyia sherehe ya kuwaaga nyota watakaowatema.

Hata hivyo, Kocha Zahera alishanukuliwa juu ya mpango wake wa kuwatema wachezaji 19 wa kikosi cha sasa, baada ya kuwasilisha ripoti yake kwa mabosi wake, lakini Mwakalebela alisema jana:

“Timu yetu imecheza kwa kuungaunga msimu huu ni vyema kuwapongeza nyota wetu waliotufikisha hapa tulipo. Tarehe ya kuwaaga nyota hao itatangazwa mara baada ya uongozi kukabidhiwa ripoti ya mwalimu ili kufahamu ni nyota gani hatutakuwa nao.”