OLE WAKO
Ernest Boakye
MWANDISHI WETU,TANGA SIKU za kiungo wa Yanga, Ernest Boakye sasa zinahesabika, benchi la ufundi la klabu hiyo limechoshwa na tabia zake huku kocha Kosta Papic akimwambia; "Ole wako." Na yeye amejibu; "Mkinilazimisha kucheza naondoka, siwezi kufia uwanjani, najali afya na maisha yangu." Ndio maana kwa hasira, benchi hilo la ufundi chini ya Kocha Kosta Papic limemrudisha kiungo huyo wa Ghana kutoka Tanga kuja jijini Dar es Salaam ikiwa ni saa chache kabla ya mechi yao dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani. “Asubuhi ya siku ya mechi (juzi Jumapili) alinifuata akasema tumbo linamuuma hivyo hawezi kucheza, nikamwambia apande basi aende hospitali jijini Dar es Salaam, nataka ripoti ya daktari vinginevyo nitamchukulia hatua kali,” alisema Papic. Kocha huyo wa Serbia alisema si mara ya kwanza kwa kiungo huyo kusingizia anaumwa, amekuwa akifanya hivyo katika mechi mbalimbali ikiwamo mechi dhidi ya Simba. “Sijui anataka nini, amezoea kulalamika tu, ni mlalamishi muda wote, mara hiki ,mara kile. Sasa anasema anaumwa, nimemwambia aende Dar es Salaam, ole wake ripoti ya daktari ionyeshe yupo fiti,” alionya Papic. “Tumemrudisha Dar es Salaam kutokana na utovu wa nidhamu, uongozi utakutana kwa ajili ya kuliongelea jambo hilo,” alisema Katibu wa Yanga, Lawrence Mwalusako huku habari zikidai kuwa uongozi umechukizwa kwa madai kuwa staa huyo na anadeka mno. Mwanaspoti ilizungumza na Boakye jana akiwa njiani kuelekea hospitali na alisema; “Nilikuwa naumwa na nilitoa taarifa kwa uongozi, siko tayari kupoteza maisha yangu kwa ajili ya kazi, nipo tayari kurudi nyumbani lakini si kulazimishwa kucheza." "Nilikuwa nasumbuliwa na matatizo ya mkojo nimepimwa nimeambiwa nipumzike, nimewapa taarifa viongozi wanasema nadeka, nashangaa sasa. Siwezi kusema uongo nimekuja hapa kucheza mpira. "Kama Yanga wanaona nimedanganya, niko tayari kurudi kwetu Ghana,"alisema mchezaji huyo huku akionekana kukerwa na hali hiyo. Kutokana na kutokuwapo kwa Ernest Boakye, katika mchezo ambao walitoka suluhu dhidi ya Azam, sehemu ya kiungo ya Yanga ilikuwa chini ya Athuman Idd ‘Chuji’, Godfrey Bonny, Nurdin Bakari na Abdi Kassim, ambao walicheza vizuri katika nafasi hiyo na kuwafanya Azam FC kushindwa kucheza mpira wao wa kawaida. Katika mechi hiyo mjini Tanga, Azam walijaribu kucheza vizuri kipindi cha kwanza kabla ya kupotea kipindi cha pili na kuwafanya Yanga kutawala, ingawa timu zote hazikutengeneza nafasi za kufunga mabao. Hata hivyo, kwa upande wa Yanga, ukilinganisha na mechi tatu zilizopita, ilionyesha mpira mzuri na wa nguvu huku wachezaji wake wakionekana kuwa na ari zaidi.