Hersi atangaza Yanga kumuuza Okello
Muktasari:
- Okello alikuwa akiwaniwa kwa nguvu na klabu mbili za Morocco wakiwemo Wydad Athletic na AS FAR Rabat zikiweka fedha ndefu.
Yanga hatimaye imethibitisha rasmi kwamba imemuuza kiungo wake Allan Okello ambaye sasa atakwenda nchini Morocco huku pia ikifahamika kuwa Ile Ngao iliyoibiwa imerudishwa.
Okello alikuwa akiwaniwa kwa nguvu na klabu mbili za Morocco wakiwemo Wydad Athletic na AS FAR Rabat zikiweka fedha ndefu.
Akitangaza mbele ya mashabiki wa klabu hiyo Rais wa Yanga injinia Hersi Said amesema klabu hiyo imemuuza rasmi Okello.
"Niwatangazie rasmi Wananchi, tumefikia makubaliano ya kumuuza rasmi kiungo wetu mpendwa Allan Okello kwa msimu huu unaoanza," amesema Hersi.
"Nataka niwaambie jambo moja licha ya kwamba tumemuuza Okello lakini hapa kwake ni nyumbani, atarudi wakati wowote tukitaka kumrudisha au akitaka kurudi."
Okello ameitumikia Yanga kwa nusu msimu akiibuka mfungaji bora wa timu hiyo msimu uliopita, akifunga mabao 14, akiwa alitua akitokea Vipers ya Uganda.
Ingawa Hersi hakutaja timu ambayo imemnunua Okello lakini Mwanaspoti lifahamu kwamba kiungo huyo ameuzwa AS FAR Rabat ambayo kwa sasa inafundishwa na kocha wa zamani wa Yanga Pedro Goncalves.
Wakati Yanga ikitangaza maamuzi hayo kiungo huyo alikuwa Mkoani Lindi ambako kikosi cha timu hiyo kilikuwa kikianza msimu mpya wa Ligi Kuu Bara kikiwa ni mgeni wa Namungo.
Aidha Yanga imethibitisha kwamba Ile Ngao ya Jamii ambayo ilitangazwa imeibiwa, imefanikiwa kurudishwa klabuni hapo.
Meneja wa Habari wa Yanga Ally Kamwe amesema:" Niwatangazie Wananchi Ile Ngao yetu ambayo tulitangaza imeibiwa, imerudishwa rasmi na sasa ipo klabuni kwetu, " amesema Kamwe huku mashabiki wakishangilia kauli hiyo.