Nsajigwa apigilia msumari Tanzania Prisons
Muktasari:
- Katika mechi tisa ilizocheza Prisons msimu huu, imeshinda tano, sare mbili na kupoteza mbili, ikiwa nafasi ya tatu na pointi 17, nyuma ya vinara KMC FC yenye pointi 19, huku safu yake ya ushambuliaji ikifunga mabao 14 na kuruhusu sita.
KOCHA Mkuu wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa 'Fuso', amesema licha ya mwenendo mzuri wa kikosi hicho, ila bado wachezaji hawatakiwi kuendelea kubweteka, ili kuendana na ushindani na kutimiza malengo waliyoweka.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nsajigwa amesema kumekuwa na maendeleo mazuri ya mchezaji mmoja mmoja hadi sasa, ingawa, bado wanahitaji kupambana na kuendelea kushikilia nafasi nne za juu katika raundi hii ya kwanza, ili kuendana na malengo yao.
"Malengo yetu ni kuhakikisha mzunguko wa kwanza hatushuki katika nafasi nne za juu, hii itatusaidia kutuwekea mazingira mazuri Ligi itakaposimama, ili tutakapoanza raundi ya pili ambayo ndio ngumu tuendeleze ushindani," amesema Nsajigwa.
Kocha huyo aliyeichezea Prisons, Yanga na timu ya taifa ya Taifa Stars, kwa msimu wa 2025-2026, alikiongoza kikosi hicho cha maafande kumaliza nafasi ya 13 na pointi 32, katika Ligi Kuu Bara, jambo lililochangia kiasi kikubwa kushuka daraja. Maafande wa Tanzania Prisons walishuka daraja kupitia Play-Off, baada ya kumaliza nafasi ya 13 na pointi zao 32, huku ikicheza na kikosi cha Mbeya City kilichomaliza kikishika nafasi ya 14 na pointi 30 na kutolewa kwa jumla ya mabao 2-0.
Baada ya hapo, timu hiyo ikacheza Play-Off nyingine ya kujinasua na janga la kushuka daraja dhidi ya Polisi Tanzania iliyoitoa Mbeya Kwanza kwa jumla ya mabao 7-1, kisha safari ya Prisons ikaishia hapo kwa kuchapwa jumla ya mabao 4-1.
Katika mechi tisa ilizocheza Prisons msimu huu, imeshinda tano, sare mbili na kupoteza mbili, ikiwa nafasi ya tatu na pointi 17, nyuma ya vinara KMC FC yenye pointi 19, huku safu yake ya ushambuliaji ikifunga mabao 14 na kuruhusu sita.