Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ni balaa niliwehuka nikapelekwa kwa sangoma

Muktasari:

  • Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, Sekilojo akiwa na umri mdogo tu aliingia katika kaburi kupokea mwili wa rafiki yake.

SAFARI ya kwenda kumzika Lawrence ilianzia Hospitali ya Makandana Tukuyu kwenda Kyela.

Mzee Jose Mwakasala ndiye aliyekuwa na kisanga kikubwa. Vipi kama Baba yake Lawrence angegoma kupokea mwili wa mwanae ambaye hakumruhusu kucheza soka Mbeya mjini?

“Tulipofika tulipokewa vema. Taarifa za msiba zilishafika. Tulikwenda na baadhi ya wazee kwa ajili ya kumsaidia Mzee Mwakasala ambaye ndiye ambaye alikuwa katika hali ngumu zaidi. Bahati nzuri baba yake, Lawrence akaelewa tukio zima, akamwachia Mungu.”

Anasimulia Sekilojo.

Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, Sekilojo akiwa na umri mdogo tu aliingia katika kaburi kupokea mwili wa rafiki yake.

Ni kitu ambacho hawezi kusahau. Kupokea kaburini mwili wa mtu ambaye alikuwa analala naye chumba kimoja akiwa mzima wa afya siku chache tu zilizopita.

“Katika watu waliochaguliwa kuingia ndani ya kaburi mimi nilikuwa mmojawapo. Nilikuwa mdogo na nilikuwa nina wasiwasi mwingi.

Kama unavyojua Kaka yangu alikuwa amehama Mbeya. Nilimuwaza Mama, nikamuwaza kaka nikawawaza ndugu zangu wengine. Kilichonitisha zaidi ni kwamba wa timu yetu ambao bado walikuwa imani za kishirikina walidai kwamba mimi ndio ilibidi nife uwanjani.”

Anasimulia Sekilojo: “Unajua pale uwanjani katika zile dakika za mwanzo mimi nilipepesuka kwa kawaida tu lakini sikuanguka.

Watu wanadai kwamba kama ningeanguka mimi basi nisingeamka kama Lawarence. Sikujali sana uvumi huo kwa sababu nilikuwa siamini. Mimi ni Msabato safi na nimekulia katika mazingira ya dini.

“Niliporudi Mbeya sikuweza kulala tena katika kile chumba ambacho nilikuwa nalala na Lawrence. Mzee Mwakasala akanichukua nikaenda nyumbani kwake akawa ananichukulia kama mwanae wa kumzaa.

Alikuwa na watoto wake wengine lakini mimi ndiye ambaye alinipenda zaidi. Kuna watu wengi Mbeya walikuwa wanaamini mimi ni mtoto wa Mzee Mwakasala.”

Siku kadhaa baada ya maziko ya Lawrence, masahibu yakaanza kumkumbuka Sekilojo. Mambo ya ajabu yalikuwa yanamtokea katika ndoto lakini mchana alihisi kwamba kuna milio ilikuwa inatoka katika sehemu yake ya nyuma ya kichwa na alishindwa hata kutembea.

“Kuna wakati nilikuwa nahisi kuna vitu vinagonga kama kengele kisogoni kwangu. Nashindwa kunyanyuka na kutembea. Nawaita dada zangu (watoto wa Mwakasala) wanishike mikono.

Mmoja ananishika mkono wa kulia mwingine ananishika mkono wa kushoto. Hapo ndio naweza kutulia.”

Anasema: “Wakati huo nilikuwa siwezi kucheza mpira. Usiku nilikuwa nashindwa kulala. Baadaye ikagundulika ilitokana na mimi kukaa sana peke yangu na kumuwaza Lawrence.

Sikuwa na tatizo jingine lolote. Walinipeleka kwa Mganga wa kiienyeji na kwa sababu sikuwa na imani na mambo hayo wala haikusaidia. Mganga alisema nimetupiwa jinni. Ulikuwa ni uongo. Nilikuwa na matatizo ya kisaikolojia tu.” anasimulia Sekilojo.

“Baadaye nikaanza kufanya mazoezi. Kila nilipokuwa nafanya mazoezi ndivyo tatizo hilo lilivyotoweka. Ni kwa sababu nilianza kuwa bize na vitu vingine kwahiyo mawazo ya kifo cha Lawrence yakaanza kuondoka taratibu.”

Umaarufu wa Sekilojo uliandelea kutambaa katika vitongoj vya Mbeya na hatimaye mwaka 1989 alionwa na klabu ya Tawala ya Mbeya. Klabu hiyo ilikuwa chini ya ofisi ya Mkuu wa mkoa.

“Uzuri wa timu hii ni kwamba ulikuwa ukicheza unapata ajira. Hapo hapo timu yetu ya Mbeya Kids (ngorongoro) ikafifia kutokana na Mzee Mwakasala kushindwa kuihudumia kama awali kutokana na timu hiyo kuanza kusafiri nje ya mkoa wa Mbeya kwa michuano ya kanda.”

Maisha ya zamani yanabakia kuwa maisha ya zamani tu. Hauwezi kuamini kuwa Sekilojo aliajiriwa kama Mhasibu msaidizi wa Ardhi mkoa wa Mbeya bila ya kuwa na Elimu hiyo. Ilikuwa njia ya kushawishi wanasoka mahiri wasaini klabu hiyo ya tawala.

Baada ya kipaji chake kuzidi kung’ara, hatimaye macho ya Tukuyu Stars yalimuona Sekilojo. Mwaka 1990 alitua Tukuyu Stars na kukuta wachezaji wenye majina makubwa. Baadhi aliwakuta wengine aliingia nao.

“Kikosi chetu kilikuwa kimekamilika. Nakumbuka tulikuwa na akina Jimmy Morerd, Ali Kimwaga, Steven Mussa (Marehemu), Michael Kidilu, Joshua Kilale, Ephraim Kayeta, Moses Kanyiki na wengineo wengi. Timu ilikuwa imekamilika.” Anasema Sekilojo.

Na sasa Sekilojo alikuwa ameingia katika changamoto ya soka. Alianza kucheza soka la kikubwa zaidi.

Alilazimika kusahau soka la Mbeya Kids na Tawala na kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza. Ni katika msimu wake wa kwanza anakumbuka kuna kitu kilitokea kati yake na kiungo mahiri wa Pamba ya Mwanza, Khalfani Ngassa ambaye ni Baba wa staa wa sasa wa soka, Mrisho Khalfani Ngassa.

Ni kitu gani kilitokea baina yao? Fuatilia simulizi hizi za makala za staa wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Sekilojo Chambua aliyefanya mahojiano na mwandishi Edo Kumwembe jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini Desemba mwaka jana.