Neria kumsindikiza Mtukudzi kaburini
Muktasari:
Wimbo wao wa kwanza Dzandimomotera ulifanya vizuri na ukafuatiwa na albamu ya kwanza ya Tuku, ambayo pia ilikupata mafanikio makubwa. Kama haitoshi Mtukudzi pia alikuwa na mchango katika Kundi la Afrika Kusini la Mahube.
ULIWAHI kuiona filamu ya Neria iliyotamba miaka ya 90? Unaukumbuka Wimbo wa Neria uliobeba jina la filamu hiyo?
Kama ndio, basi yule mtunzi wa wimbo huo, Oliver Mtukudzi juzi Jumatano amefariki dunia katika hospitali moja ya binafsi jijini Harare kule Zimbabwe.
Filamu ya Neria ya mwaka 1993 ilitungwa na Mwandishi wa Vitabu, Tsitsi Dangarembga. Kwa kifupi, filamu hiyo ilimhusu mwanamke ambaye mume wake alifariki dunia kwa ajali. Kaka wa mumewe alimrithi mwanamke huyo aliyekuwa na watoto na kutumia vibaya mali zilizochumwa na mdogo wake. Filamu hiyo ilipata umaarufu mkubwa na ilivutia zaidi kutokana na ‘sound track’ ya Wimbo wa Neria wa Oliver Mtukudzi.
Gwiji huyo wa muziki wa Afro Jazz aliyefahamika kwa jina la ‘Tuku’ alikuwa mpiga gitaa mahiri amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 66 na kabla kifo chake alikuwa akipigania uhai wake kwa zaidi ya mwezi.
Hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na familia yake kuhusiana ugonjwa uliosababisha kifo chake, ingawaje habari zisizo rasmi zinadai ugonjwa wa moyo ndio uliomuondoa duniani.
Ujanani Mtukudzi aliyekulia katika Kitongoji cha Highfield, katika getto jirani kabisa na Mji Mkuu, Harare alianza kazi ya muziki mwaka 1977 alipojiunga na Bendi ya Wagon Wheels, akiwa na Thomas Mapfumo na mpiga gitaa mahiri James Chimombe.
Wimbo wao wa kwanza Dzandimomotera ulifanya vizuri na ukafuatiwa na albamu ya kwanza ya Tuku, ambayo pia ilikupata mafanikio makubwa. Kama haitoshi Mtukudzi pia alikuwa na mchango katika Kundi la Afrika Kusini la Mahube.
Sauti yake ilikuwa maarufu na ilitambulika kwa kila aliyeisikia kuwa inatokea Zimbabwe na ilifanikiwa kuvuka mipaka ya Afrika. Akiwa mmoja wa washiriki wa Kundi la Zimbabwe la KoreKore, sambamba na Nzou Samanyanga aliimba nyimbo zake kwa Lugha ya Taifa ya Kishona, Ndebele na Kiingereza. Pia, Mtukudzi alichanganya vionjo vingine vya kiasili na kuufanya muziki wake utambulike kama kwa staili ya Muziki wa Tuku.
Unaweza kushangaa, lakini ndivyo ilivyokuwa, wimbo wake wa Neria ulikuwa kama Wimbo wa Taifa la Zimbabwe. Kila lilipotokea tukio kubwa, Mtukudzi aliitwa kuimba wimbo huo. Februari 21, mwaka jana katika mazishi ya kiongozi wa chama cha upinzani, Morgan Tsvangirai aliimba na kupokewa kwa majonzi na maelfu ya Wazimbabwe waliohudhuria mazishi hayo.
Mtukudzi ambaye alikuwa balozi wa UNICEF Kanda ya Kusini mwa Afrika, mfanyabiashara, mwanasiasa na mtetezi wa haki za binaadamu, alipata mapokezi makubwa katika ziara zake za Uingereza, Marekani na Canada alipoenda kuitumbuiza na kupokewa na umati wa mashabiki.
Pamoja na umri kumtupa, Mtukudzi katika maisha yake, amefanikiwa kutoa album 58 na kupata zaidi ya tuzo zaidi ya 25 katika kila nyanja ya muzuki wake.
Mbali na Neria pia Mtukudzi alishiriki katika filamu nyingine kama vile Jit mwaka 1990. Shanda mwaka 2002 na 2004) Sarawoga, 2009, 2012 Nzou NeMhuru Mudanga ambayo alikuwa akishirikiana na mwanaye wiki chake kabla ya kifo chake.
Mtukudzi ni baba wa watoto watano na wajukuu wawili. Watoto wake wawili ni wanamuziki. Mtoto wake, Sam Mtukudzi alirithi kazi ya baba yake, alifariki kwa ajili ya gari Machi 2010 na mwaka 2013, baba yake alitoa albamu aliyoiita ‘Sarawoga’.
Mtukudzi alizaliwa katika familia ya watoto sita, mazishi yake yatafanyika jijini Harare hivi karibuni.
Tarehe kamili ya mazishi yake haijatajwa lakini yanatarajiwa kuhudhuriwa na maelfu ya wadau wa muziki, wanasiasa na wanyonge wa Zimbabwe. Bila shaka Wimbo wa Neria utamsindikiza kaburini na kuimbwa na waombolezaji. Mtukudzi ni kama shujaa aliyepotea ghafla.