Neema Kusekwa: Mgore, Manula wampa maujanja
Muktasari:
- Katika mahojiano baina yake na Mwanaspoti, Neema anasema wazazi wake walihitaji aweke nguvu zaidi kwenye elimu, lakini alitafuta njia mbadala ya kuhakikisha anapambania kipaji chake.
BIDII na kipaji cha golikipa wa Mashujaa Queens, Neema Mustafa Kusekwa, ndivyo vilivyobadilisha mtazamo wa wazazi wake kuanza kuamini katika kazi anayofanya ya mpira wa miguu.
Katika mahojiano baina yake na Mwanaspoti, Neema anasema wazazi wake walihitaji aweke nguvu zaidi kwenye elimu, lakini alitafuta njia mbadala ya kuhakikisha anapambania kipaji chake.
“Baba yangu alikuwa amenilipia masomo ya ziada baada ya kutoka shule, nilichokuwa nakifanya katika begi nililobebea daftari, nilikuwa naweka na nguo za mazoezi, hivyo kila siku nilikuwa napita viwanja kucheza na watoto wa kiume,” anasema Neema na kuongeza;
“Baadaye baba yangu alikuja kugundua napitia kufanya mazoezi, tena bila viatu, ikabidi aanze kunisapoti kwa kuninunulia viatu vya mazoezi na kunipeleka mazoezi ya maveterani yeye alikuwa anacheza beki.”
Anasema kitu kilichokuwa kinamvutia katika mazoezi hayo, alikuwa anamuona aliyekuwa winga wa Yanga, Dickson Ambundo akicheza na tayari alikuwa amefanikiwa.
“Nyumbani kwa kina Ambundo ni jirani na kwetu, nikawa naamini kama kaka zangu wa mtaani wameanza kupata maisha kupitia soka na mimi naweza,” anasema.
Anasema safari yake ya kucheza mpira wa miguu, ilianzia katika kituo cha Marsh Queens ya Mwanza mwaka 2021.
“Nilikuwa najituma kwa bidii, ili kuwaonyesha wazazi wangu sikukosea kuchagua kipaji changu, kiwango changu kikawa kinakuwa siku hadi siku, hiyo timu ya kituo ilikuwa inacheza Ligi ya Mkoa ambako ndiko nilikoonekana na timu zingine,” anabainisha.
Anasema baada ya kutoka Marsh Queens alikwenda kujiunga na kituo cha Mshikamano Queens ambacho kipo Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam, baada ya kufanya vizuri alionekana na timu ya Ruangwa Queens msimu uliopita wa 2025-2026.
“Kabla ya kwenda kujiunga na Ruangwa Queens, tayari nilikuwa nafuatiliwa na Mashujaa kwani kuna kipindi tulicheza nao mechi ya kirafiki nikiwa na Mshikamano, kocha wa makipa wa timu hiyo Mustafa Mabruck, alinifuata na kuniambia mimi ni golikipa mzuri natakiwa kujituma kwa bidii,” anasema Neema na kuongeza;
“Usajili wa msimu huu viongozi wa Mashujaa walinipigia simu na kuhitaji huduma yangu, nafarijika kuwa hapa kwani tunapata sapoti ya hali ya juu.”
DAU LA USAJILI
Anasema kwa mara ya kwanza pesa ndefu ya usajili aliyoipata ilikuwa Sh.3.5 milioni, ambapo Sh.2m alimpatia baba yake mzazi, aliyemnunulia kiwanja na kumuanzia msingi wa nyumba.
“Pesa nyingine iliyokuwa imebakia ilikuwa ya matumizi yangu pia niliwasaidia wachezaji wenzangu ambao bado hawajatoka kuwanunulia viatu, ili kuwapa moyo wa kupambana,” anasema Neema ambaye ndoto yake kubwa ni kucheza Twiga Stars na nje ya nchi. Anasema golikipa aliyewahi kumfuata na kumwambia ana kipaji cha juu ni wa TRA United, Daniel Mgore.
“Mgore ni kipa ninayemtazama kama mfano, lakini wengine ni Aishi Manula wa Azam, Djigui Diarra wa Yanga, napenda wanavyojiamini, wanavyozungumza na mabeki, akili kubwa ya kuokoa hatari, ukiachana hao kwa upande wa wanawake ni Najiat Abass anajituma, akifungwa unamuona anaumia, anastahili nafasi anayopata kucheza timu ya Twiga Stars.”
Anaongeza: “Kwa wachezaji wa ndani nampenda Maxi Nzengeli, Dickson Ambundo, Dickson Job kwani wana nidhamu kubwa uwanjani.”
NENO KWA WAZAZI
Anasema kuna vikwazo vikubwa kwa wasichana wanaocheza mpira wa miguu, lakini ombi lake kwa wazazi wawaruhusu watoto wao kupambania vipaji walivyo navyo.
“Wazazi wanaona msichana akicheza mpira wa miguu anakwenda kuwa mhuni, wanapaswa kujua kwa sasa soka ni ajira na limeanza kulipa.”