‘Fupa gumu’ linalomsubiri mrithi wa Edna Lema Yanga
Muktasari:
- Kocha huyo alitimka kikosini hapo baada ya kupoteza kwenye mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba Queens walipopoteza kwa mabao 3-0.
Baada ya kuondoka kwa aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga Princess, Edna Lema kuna mfupa mgumu unaomsubiri kocha mpya atakayechukua mikoba yake.
Kocha huyo alitimka kikosini hapo baada ya kupoteza kwenye mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba Queens walipopoteza kwa mabao 3-0. Pamoja na mabadiliko ya benchi la ufundi, kocha mpya atakayefundisha timu hiyo anapaswa kujiandaa kukabiliana na mfupa mgumu wa kuirejesha timu hiyo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) na kuvunja utawala wa wapinzani wao wakubwa, Simba Queens na JKT Queens.
Edna Lema aliondoka Yanga Princess akiacha alama kubwa ya nidhamu, ushindani na misingi imara ya kiufundi.
Mwanaspoti imekuchambulia changamoto inayomsubiri kocha mpya atakayeifundisha Yanga Princess.
UBINGWA
Hii ndio changamoto kubwa zaidi, mashabiki wa Yanga wana matamanio makubwa ya kuona timu yao ya kike inabeba taji la Ligi Kuu ya Wanawake.
Timu ya wanaume imekuwa ikishinda mataji tofauti na kufanya vizuri kimataifa lakini kwa upande wa wanawake ni kama donda ndugu lililoshindwa kupata dawa. Hivyo kibarua cha kwanza kwa kocha mpya wa Yanga itakuwa kurudisha imani kwa mashabiki kwa kuwapatia kile ambacho wametamani kuona kubeba taji la ligi ambalo limekuwa likinyakuliwa na wapinzani wao Simba Queens na JKT Queens.
KUVUNJA UTAWALA SIMBA, JKT
Moja ya changamoto ngumu zaidi kuliko yote utakaomkabili kocha mpya ni kumaliza ukame wa mataji na kuvunja utawala wa Simba Queens pamoja na JKT Queens ambazo zimekuwa zikitawala Ligi Kuu ya Wanawake kwa miaka mingi.
Yanga Princess imewekeza fedha nyingi katika usajili wa wachezaji wa ndani na wa kigeni, lakini bado haijafanikiwa kubeba taji la ligi kuu tangu timu hiyo ilipoanza kushiriki ligi mwaka 2018. Hii ndio changamoto kubwa ya Yanga Princess mashabiki wana hamu ya kuona timu hiyo ikitwaa ubingwa na kupata tiketi ya kushiriki Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kama ilivyo kwa watani zao Simba na JKT Queens.
MATOKEO
Yanga ni klabu kubwa yenye presha kubwa kutoka kwa mashabiki. Tofauti na klabu nyingine ambazo kocha anaweza kupewa muda wa kujenga timu kwa miaka miwili au mitatu, Yanga Princess haitakuwa na muda huo.
Kocha mpya anatakiwa kutambua kwamba kila mechi kwake itakuwa kama fainali. Kupoteza au kutoka sare katika mechi mbili mfululizo kutamweka kwenye presha kubwa ya mashabiki wanaotaka kuona matokeo ya haraka. Kuondoka kwa Edna Lema kunaongeza uzito pia kwa sababu mashabiki watakuwa wakilinganisha mbinu na matokeo ya kocha mpya na yale ya kocha aliyetimka.
KUUNGANISHA TIMU
Kila msimu unapomalizika au kuanza, Yanga Princess imekuwa ikifanya mabadiliko kwenye kikosi chake kwa kuingiza nyota wapya wa kigeni na wa ndani.
Changamoto ya kwanza kabisa kiufundi kwa kocha mpya itakuwa ni kuunganisha vipaji hivi mbalimbali na kutengeneza timu moja inayoelewana.
Kuwa na wachezaji wenye majina makubwa ni jambo moja, lakini kuwafanya wacheze kama timu yenye mbinu moja na maelewano uwanjani ni kazi nyingine kabisa.
Edna Lema alifanikiwa kujenga nidhamu ya kikosini, hivyo kocha mpya anapaswa kuhakikisha haharibu mshikamano huo huku akiingiza mfumo wake mpya wa uchezaji.
MABEKI, USHAMBULIAJI
Moja ya maeneo yaliyokuwa yakilalamikiwa na wadau wa soka.msimu uliopita ni ukosefu wa umakini katika safu ya mabeki wakati wa mechi kubwa dhidi ya timu kama Simba Queens au JKT Queens. Kocha mpya anatakiwa kutafuta suluhu ya haraka ya kuhakikisha safu yake ya ulinzi hairuhusu mabao kwenye mechi za ushindani wa juu, huku pia akiongeza makali kwenye safu ya ushambuliaji ili kutumia vyema nafasi zinazotengenezwa.
SAIKOLOJIA
Yanga Princess imekuwa ikionyesha kiwango kizuri dhidi ya timu za saizi ya kati na ndogo, lakini mara kadhaa imekuwa ikipoteza upepo inapokutana na wapinzani wao wa jadi, Simba Queens.
Kocha mpya ana kazi ya ziada ya kuwajenga wachezaji wake kisaikolojia ili wawe na utulivu, kujiamini katika mechi hizo kubwa. Dabi za Kariakoo kwa wanawake zimekuwa na presha kubwa, na matokeo ya mechi hizo mara nyingi hutoa mwelekeo wa bingwa atakavyokuwa.
Ikiwa kocha mpya atafanikiwa kutafuna mfupa huo mgumu kwa kupanga mbinu sahihi, kuweka nidhamu ya hali ya juu kikosini bila shaka Msimu huu unaweza kuwa wa kihistoria kwa Wana yanga.