Prime
Namba sita wa Yanga huyu hapa!
Muktasari:
- Aucho alitambulishwa rasmi Yanga Agosti 9, 2021, akisajiliwa kama mchezaji huru kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Misr El Makkasa ya Misri.
MZIMU wa kiungo mkabaji Khalid Aucho umeendelea kuitafuna Yanga kimyakimya, huku klabu hiyo ikihangaika msimu mzima kuziba pengo la Mganda huyo bila mafanikio, licha ya kufanya usajili kadhaa. Swali ni, je, msimu ujao itafanikiwa kupata mrithi sahihi?
Aucho alitambulishwa rasmi Yanga Agosti 9, 2021, akisajiliwa kama mchezaji huru kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Misr El Makkasa ya Misri.
Aliitumikia Yanga kwa takribani misimu minne mfululizo kuanzia 2021/22 hadi mwisho wa msimu wa 2024/25. Akiwa klabuni hapo, alikuwa mhimili muhimu wa safu ya kiungo, akichangia Yanga kutwaa mataji manne ya Ligi Kuu ya NBC, Kombe la FA na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup) mwaka 2023.
Aliondoka Yanga Julai 2025 baada ya mkataba wake kumalizika na kujiunga na Singida Black Stars, ambako amecheza kwa msimu mmoja hadi sasa.
PENGO HALIJAZIBWA
Katika jitihada za kuziba nafasi yake, Yanga ilimsajili Moussa Balla Conté katika dirisha kubwa la usajili akitokea CS Sfaxien ya Tunisia. Hata hivyo, hakuweza kudumu kwa muda mrefu baada ya kushindwa kuonyesha kiwango kilichotarajiwa ndani ya miezi sita.
Katika dirisha dogo la Januari 2026, Conté alihamia Raja Casablanca ya Morocco, lakini hata huko hakufanikiwa kuwashawishi viongozi wa klabu hiyo.
Yanga pia ilimsajili Mohamed Damaro, ambaye alitambulishwa rasmi Desemba 31, 2025, akitokea Singida Black Stars. Alisajiliwa kama mchezaji wa ndani licha ya kuwa raia wa Guinea.
Hata hivyo, hakuna kati yao aliyefikia kiwango na mchango wa Aucho, ambaye alikuwa akicheza kwa ubora na nidhamu kubwa iliyoisaidia Yanga kufikia malengo yake. Ndiyo maana hadi sasa klabu hiyo inaendelea kutafuta mbadala wa uhakika.
KAZI IKO HAPA
Viungo kadhaa wanatajwa kuwindwa na Yanga kuelekea msimu wa 2026/27. Lakini, kwa kuzingatia rekodi zao, ni nani anayefaa kuwa mrithi wa Aucho usishangae akatoka nje ya listi hii?
MORICE CHUKWU
Kiungo huyo wa Nigeria ana uwezo wa kucheza pia kama beki. Alijiunga na Singida Black Stars misimu mitatu iliyopita na kufanya kazi chini ya makocha mbalimbali, akiwemo Miguel Gamondi. Katika kipindi hicho aliwahi kutolewa kwa mkopo Ihefu (sasa Fountain Gate) na Tabora United.
Baada ya kumaliza mkataba wake na Singida Black Stars, sasa ni mchezaji huru. Pia anatajwa kuwa mmoja wa viungo wachache waliowahi kumweka Aucho benchi walipokuwa pamoja Singida.
Faida nyingine ni uzoefu wake mkubwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara, jambo linalomfanya kutohitaji muda mrefu wa kuzoea mazingira iwapo atasajiliwa na Yanga.
MOHAMED ZOUGRANA
Mohamed Zougrana ni miongoni mwa majina yanayotajwa sana katika tetesi za usajili wa Yanga. Kwa sasa anachezea MC Alger ya Algeria, ambapo bado ana mkataba wa mwaka mmoja.
Ni kiungo mkabaji mwenye uwezo mkubwa, lakini iwapo Yanga itamhitaji italazimika kufanya mazungumzo na klabu yake, pamoja na kumpa muda wa kuzoea mazingira ya soka la Tanzania.
JAMES AKAMINKO
Kiungo huyo wa kimataifa wa Ghana pia anatajwa katika mipango ya Yanga kuelekea msimu mpya.
Akaminko alimaliza mkataba wake wa takribani miaka minne na Azam FC Julai 5, 2026, hivyo kwa sasa anapatikana kama mchezaji huru. Faida yake kubwa ni kuifahamu vizuri Ligi Kuu Tanzania Bara.
ALPHONCE MABULA
Kiungo wa Taifa Stars mwenye umri wa miaka 22 amekuwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na Şamaxı FK ya Azerbaijan kumalizika Juni 30, 2026.
Mabula ndiye mchezaji pekee wa ndani anayetajwa kwenye nafasi hiyo. Usajili wake unaweza kuipa Yanga nafasi ya kuendelea kutumia vizuri idadi ya wachezaji wa kigeni, huku ikipata kiungo mwenye uwezo.
SEYDOU SACKO
Kiungo wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast naye anahusishwa na Yanga. Taarifa zinaeleza kuwa Yanga inachuana na Esperance de Tunis ya Tunisia katika mbio za kuwania saini yake.
UPANDE WA MASTAA
Akizungumza na Mwanaspoti, Morice Chukwu amesema hawezi kuzungumzia taarifa za kuhusishwa kwake na Yanga kwa sasa. “Siwezi kusema lolote kwa sasa. Nipo Nigeria na nimemaliza mkataba na Singida Black Stars. Bado sijajua nitajiunga na timu gani msimu ujao. Majibu yatapatikana wakati ukifika.”
Mtu wa karibu wa James Akaminko amesema: “Akaminko alikuwa kwenye mazungumzo na Simba hapo awali, lakini yalikwama. Kuhusu Yanga, hata mchezaji mwenyewe hana taarifa rasmi.”
WASIKIE WADAU
Mchezaji wa zamani wa Simba, Dua Said, amesema Yanga inahitaji kiungo mwenye uzoefu kutokana na ugumu wa ratiba ya msimu ujao.
“Viongozi wa Yanga wanafahamu vizuri soka na ubora wa wachezaji. Wakifanya maamuzi sahihi, wanaweza kupata mchezaji atakayemsaidia kocha kuwa na chaguo nyingi zaidi,” amesema.
“Mabula akiwa pamoja na kiungo mmoja wa kigeni, ushindani utaongezeka. Pia Duke atapata wachezaji watakaomsaidia msimu ujao. Hii ni hatua muhimu kwa Yanga, hivyo wanapaswa kufanya maamuzi sahihi.”