Kocha Rwanda aukubali mziki wa Tanzania
Muktasari:
- Rwanda ilianza kwa kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Tanzania kwenye mechi ya kundi A ambayo ina timu Ethiopia.
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Rwanda U-20 amekiri kuwa Tanzania ilikuwa bora kwenye kila eneo na kwamba makosa waliyoyafanya kipindi cha kwanza yaliwavuruga kwa kiasi kikubwa.
Rwanda ilianza kwa kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Tanzania kwenye mechi ya kundi A ambayo ina timu Ethiopia.
Kocha huyo amesema Tanzania ilicheza kwa utulivu na mshikamano mkubwa, kiasi cha kuonekana kama kikosi ambacho kimekaa pamoja kwa muda mrefu.
Akizungumzia mchezo huo, kocha huyo alisema kipindi cha kwanza kilikuwa kigumu kwao kutokana na makosa waliyofanya wenyewe, hali iliyowapa Tanzania nafasi ya kutengeneza mashambulizi na kufunga mabao matatu.
Kocha huyo alisema mwanzo mbaya uliigharimu Rwanda, kwani walishindwa kuwa na utulivu na kufanya maamuzi sahihi wakati wa kuzuia mashambulizi ya Tanzania.
“Tumefanya makosa na Tanzania wakatuadhibu hatuna namna zaidi ya kushinda mechi ijayo dhidi ya Ethiopia,”
Baada ya kuona mambo yamekuwa magumu kipindi cha kwanza, benchi la Rwanda lilifanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kubana eneo la katikati ya ulinzi na kiungo.
Eneo hilo ndilo ambalo Tanzania ilikuwa ikilitumia kupitisha mipira na kujenga mashambulizi, hivyo Rwanda ilijaribu kulifunga ili kupunguza nafasi za wapinzani wao.
Mbinu hiyo ilisaidia Rwanda kurejea kwenye mchezo na kupunguza kasi ya mashambulizi ya Tanzania, tofauti na ilivyokuwa katika kipindi cha kwanza.
Pamoja na kubadilika kwa mchezo, Rwanda ilipata nafasi kadhaa za kufunga kipindi cha pili, lakini washambuliaji wake walishindwa kuzitumia.
Kocha huyo alisema tatizo kubwa lilikuwa kwenye umaliziaji, kwani nafasi walizozipata hazikuzaa mabao.