Nado aendeleza moto, Azam ikiitandika Mbeya City 4-0
Muktasari:
- Nado alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 45 akimalizia pasi ya Abdulrafiu Taiwo, akiifanya Azam kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
WINGA wa Azam FC, Idd Seleman 'Nado', ameendelea kuonyesha ubora wake baada ya kuitanguliza timu hiyo kwa bao la kipindi cha kwanza dhidi ya Mbeya City, kabla ya matajiri hao wa Chamazi kuongeza mengine kipindi cha pili na kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa leo Oktoba 28, 2026 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Nado alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 45 akimalizia pasi ya Abdulrafiu Taiwo, akiifanya Azam kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kabla ya mapumziko, takwimu zilionyesha kuwa wenyeji Azam walitawala mechi hiyo wakimiliki mpira kwa asilimia 66 dhidi ya 34 za Mbeya City, huku wakipiga mashuti manne yaliyolenga lango na kupata kona mbili.
Kipindi cha pili kilivyoanza Azam iliendeleza mashambulizi, huku Mbeya City ikishindwa kupata njia ya kuzuia kasi ya wenyeji.
Dakika ya 62, kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliiandikia Azam bao la pili na kuifanya timu hiyo kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kudhibiti mchezo. Kwa Fei Toto, bao hilo lilikuwa la nne msimu huu.
Dakika ya 71, Hassan Mubiru aliiongezea timu hiyo bao la tatu akitumia pasi ya Fei Toto na lile la nne likifungwa na Kipre Junior dakika ya 90, akimalizia pasi ya Mubiru.
Nado, bao hilo linamfanya afikishe mabao mawili msimu huu katika ligi akicheza mechi tano kati ya tisa, akiendelea kuwa miongoni mwa wachezaji muhimu katika mashambulizi ya Azam.
Pia nyota huyo alifunga mabao mawili katika ushindi wa jumla wa 2-1 dhidi ya ZED FC ya Misri ulioifanya Azam kufuzu Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi kwa msimu wa pili mfululizo.
Ushindi dhidi ya Mbeya City unaifanya Azam kufikisha pointi 20 katika mechi tisa za ligi ikishinda sita, sare mbili na kupoteza moja ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo.
Upande wa Mbeya City, imebaki nafasi ya kumi ikiwa na pointi kumi katika mechi tisa ilizocheza, imeshinda tatu, sare moja na kupoteza tano.