Nabi aishika pabaya Simba
YANGA juzi ilikuwa uwanja wa nyumbani ikipambana na Kagera Sugar ikiendelea kupunguza hatua ya kufuata taji lao la pili la ubingwa mfululizo na baada ya kumaliza mechi hiyo, akili ya kocha wao Nasreddine Nabi ni kuelekea mchezo dhidi ya watani wao Simba.
Nabi ambaye juzi alirudi kazini tangu arejee kutoka nchini kwao ameliambia Mwanaspoti kuwa wala hawana presha yoyote kuelekea mchezo dhidi ya Simba Aprili 16, pale Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Nabi alisema ingawa wanatambua kwamba mchezo huo utakuwa mgumu wakiheshimu Simba lakini kikosi chake kitashuka uwanjani siku ya mchezo na sapraizi nzuri kwa mashabiki wao na wanaamini kuwa wao ni bora kwa kuwa wanaifahamu Simba.
Kocha huyo ameringia uzoefu wa wachezaji wake akisema wanajua thamani ya mechi kama hiyo kwa mashabiki wao na kwamba wataingia katika maandalizi wakijikita kujiandaa vizuri na mchezo huo na watu wasiwe na hofu.
"Tunawaheshimu Simba ni timu yenye mabadiliko lakini hatuwezi kuwa na presha hata kidogo, tutakwenda kuandaa timu ambayo itakuja uwanjani kucheza kwa ubora mkubwa kwenye mechi hii kubwa, tunawajua vizuri sana," alisema Nabi ambaye tangu aanze kazi Yanga Novemba 25,2021, ndani ya mechi 8 za mashindano yote dhidi ya Simba ameshinda 4 akipoteza 1 na kutoa sare 3.
"Kitu bora kwetu wachezaji ambao walikuwa majeruhi wamerejea wengi kitu ambacho kitatupa nafasi pana ya kuchagua nani anaweza kuwa ndani ya kikosi kuelekea mchezo huo.
Nabi alisema malengo yao makubwa katika mchezo huo ni kutamani ushindi ili waendelee kuusogelea ubingwa wa pili mfululizo kwa timu yake ambayo ipo katika msimu bora.
"Malengo yetu ni kuendelea kushinda, tunahitaji ushindi ili kuendelea kuweka hai malengo yetu ya kuchukua ubingwa wakati kama huu ni vyema kuongeza pointi na sio kupunguza.
"Narudia tunaiheshimu Simba na hautakuwa mchezo rahisi lakini niseme Yanga itaingia uwanjani kucheza kwa ubora mkubwa kwa ujazo wa mchezo mkubwa kama huo ili tupate ushindi, jambo la msingi kwetu ni kushinda."