Mzunguko wa pili Ligi Kuu Wanawake kuanza leo
Muktasari:
- Mechi hizo zinatarajiwa kuanza kwa kasi, huku vigogo wakisaka kuendelea kupambania taji hilo linalotetewa na JKT Queens, ilhali wakiwapo wengine wanaopigania kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja.
MZUNGUKO wa pili wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) unarejea leo baada ya mapumziko ya mwezi mmoja wa kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na lile la Afrika (CAF) kwa mashindano ya wanawake, ambapo zinapigwa mechi sita kwenye viwanja tofauti.
Mechi hizo zinatarajiwa kuanza kwa kasi, huku vigogo wakisaka kuendelea kupambania taji hilo linalotetewa na JKT Queens, ilhali wakiwapo wengine wanaopigania kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja.
Simba Queens inaongoza ikiwa na pointi 31 baada ya michezo 11, ikifuatiwa na Yanga Princess yenye pointi 30, jambo linaloashiria ushindani katika mbio za ubingwa, huku JKT ikiwa nazo 26.
Katika mechi za mzunguko wa pili, vinara Simba Queens watakuwa na kibarua kizito dhidi ya Bilo Queens, ambao wanashika mkiani, mechi itakayopigwa Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.
Ni mechi ambayo Simba itataka kushinda ili kujiimarisha zaidi kileleni, lakini Bilo kuitumia ili kufufua matumaini yao ya kusalia Ligi Kuu.
Mechi nyingine itapigwa Uwanja wa Azam Complex, Yanga Princess ikiikaribisha Ruangwa Queens katika mechi inayotarajiwa kuwa na ushindani, hasa ikizingatiwa Ruangwa wanahitaji pointi kujinasua kutoka nafasi za chini.
Mabingwa watetezi JKT Queens wanacha kujiuliza kwa Bunda Queens; mechi itapigwa Karume, Mwanza, na JKT wanahitaji kushinda ili kupunguza gepu la msimamo, huku Bunda wakisaka pointi ili kusogea juu.
Alliance Girls, iliyopo nafasi ya nne na pointi 19, itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Fountain Gate Princess, iliyopo nafasi ya tano na pointi 17; mechi ambayo inaweza kubadilisha kabisa nafasi za katikati ya msimamo kutokana na tofauti ya pointi mbili baina yao.
Mechi nyingine itakuwa ni ile ya Geita Queens iliyopo nafasi ya tisa na pointi tisa itavaana na Ceasiaa Queens iliyopo nafasi ya 10 ikiwa na alama nane, huku Mashujaa Queens ikivaana na Tausi FC.
Kocha wa Ceasiaa, Ezekiel Chobanka, amesema mechi hiyo itakuwa ngumu kwa upande wao kutokana na ushindani wa Geita waliouonyesha msimu huu.
“Timu zote zinafuatana kwenye msimamo wa ligi; hii ina maana kuna ushindani mkubwa. Tunajua ni mechi ya nyumbani, hivyo tunapaswa kushinda na kuzibakiza pointi tatu.”
Mshambuliaji wa Yanga, Jeanine Mukandayisenga, amesema wamejipanga kuhakikisha wanafanya vizuri ili kuendelea kusogea kwenye nafasi za juu.
“Ligi ni ngumu; kama wachezaji tumejiandaa kuhakikisha tunafanya vizuri na kuisaidia timu kutimiza malengo ya msimu huu ya kuchukua ubingwa.