Prime
Mzigo wa Kariakoo Dabi umerudi

Muktasari:
- Vigogo wa Simba na Yanga waliitwa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma kuzungumza na Rais, Samia Suluhu Hassan na muda mchache Bodi ya Ligi ilitoa taarifa kwamba mechi hiyo itapigwa Juni 25, tofauti na msimamo iliyokuwa nayo kwamba itachezwa Jumapili.
MZIGO umerudi. Ndivyo unavyoweza kusema kwa ishu ya Dabi baada ya sasa kutangazwa itapigwa Juni 25 na si keshokutwa Jumapili kama ilivyokuwa awali.
Vigogo wa Simba na Yanga waliitwa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma kuzungumza na Rais, Samia Suluhu Hassan na muda mchache Bodi ya Ligi ilitoa taarifa kwamba mechi hiyo itapigwa Juni 25, tofauti na msimamo iliyokuwa nayo kwamba itachezwa Jumapili.
Taarifa hiyo mpya imemaliza sintofahamu iliyokuwapo awali juu ya mechi hiyo namba 184 ambayo iliahirishwa Machi 8.
Hii ina maana kwamba pambano hilo la watani sasa ndilo litakalofungia msimu kama ilivyokuwa Septemba 26, 1992 na Mei 6, 2012.
Katika mechi ya 1992, Yanga ilisusa kwenda uwanjani kuvaana na Simba kwa vile ilishatwaa ubingwa na hivyo kukubali kupoteza mechi mezani kwa Mnyama kupewa pointi mbili na mabao mawili, kisha Yanga kutozwa faini ya Sh 250,000 zilizolipwa na aliyekuwa moja wa wafadhili wa klabu hiyo, Murtaza Dewji.
Kwa mechi ya 2012, Simba ilishabeba ubingwa mapema na hivyo mechi hiyo ilikuwa ya kusherehesha pati tu na Yanga kupigwa mabao 5-0.
Awali ratiba ilionyesha kuwa Ligi ya msimu huu ingemalizika Juni 22 kabla ya kuchezwa mechi za play-off za kusaka timu ya mwisho ya kupanda au kushuka daraja kwa msimu ujao wa Ligi.
Timu hizo sasa zitamaliza mechi zao mbili za Juni 18 na 22 kabla ya kumalizana wenyewe, Simba ikianza na KenGold kisha kumalizana na Kagera Sugar ambazo zote zimeshashuka daraja.
Kwa Yanga itacheza kwanza na Tanzania Prisons kisha kumalizana na Dodoma Jiji, ndipo sasa zitaenda kukutana Kwa Mkapa.
Licha ya kwamba kilichozungumzwa kati ya mabosi hao wa Simba na Yanga na Rais Samia, ni siri, lakini taarifa ya Bodi ya Ligi kwamba mchezo huo utapigwa Juni 25 na kuzitakia timu zote maandalizi ya pambano hilo litakalopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ina maana ule utata wa mchezo huo umeisha.
Yanga ilithibitisha mechi hiyo kupigwa Juni 25 na kuweka slogani ya Hii haina kipengele, ikipigwa Saa 11:00 jioni.
Kabla ya taarifa mpya, Bodi ilikomaa kwamba mchezo ungepigwa Jumapili kama ilivyokuwa ikisimamia Simba, huku Yanga yenyewe ikisisitiza isingecheza tena hadi itakaposikilizwa mambo yao manne waliyotaka ikiwamo kujiuzulu kwa baadhi ya watu.
HALI ILIVYOKUWA: Ngoma ilioonekana kuwa ngumu juu ya mechi hiyo namba 184 wa kiporo kati ya wenyeji Yanga dhidi ya Simba baada ya kila upande kusimamia msimamo iliyonayo, huku utata zaidi ukiwa ni ukimya uliopo juu ya maandalizi yake tofauti na mazoea kunapokuwepo pambano kama hilo.
Licha ya Bodi ya Ligi kusisitiza mchezo huo upo kama ulivyopangwa, huku Simba nayo ikiweka bayana itapeleka timu kesho Kwa Mkapa, lakini hali ni tete mtaani kwa mashabiki wakihofia isije yakawakuta kama ilivyokuwa Machi 8 walipoibukia uwanjani kisha mechi kupigwa kalenda.
Utata uliokuwa unaendelea juu ya mchezo huo ni mkanganyiko wa taarifa muhimu za mchezo huo huku upande mwingine ukionyesha, kulikuwa na mchakato wa kuahirishwa kwa mechi hiyo ili upigwe siku nyingine, lakini wengine wakisisitiza mechi ipo hata kama Yanga haitaenda uwanjani.
Awali mechi hiyo ilikuwa ipigwe Machi 8,2025 lakini ikaharishwa kutokana na kadhia ya Simba ambao ni timu mgeni kuzuiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Mkapa Machi 7 na wanaodaiwa kuwa ni makomandoo wa Yanga.
Sakata hilo likailazimu Bodi ya Ligi Tanzania kuuahirisha mchezo siku ya mchezo saa chache kabla ya mechi hiyo kuanza.
Kuahirishwa kwa mchezo huo kukaibua mzozo mpya baada ya Yanga ambao walikuwa timu mwenyeji akiwa amefika mpaka uwanjani kugomea mchezo utakaopangwa.
Yanga imesimama na msimamo huo ikigoma mechi iliyopangwa upya kufanyika Juni 15 Jumapili wiki hii ikisema haiutambui mchezo huo kwa kile ilichodai kutoridhishwa na taratibu za kuindoa mechi ya kwanza huku ikitaka hatua zichukuliwe za kuwawajibisha baadhi ya maafisa wa Bodi ya Ligi (TPLB) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Msimamo huo wa Yanga ndiyo umekuwa kizuizi kikubwa juu ya hatma ya mchezo huo wakidai hawataingia uwanjani endapo hatua hizo walizozitaka kuchukuliwa zifanyiwe kazi.
Wakati Yanga ikisimama na msimamo huo Bodi ya Ligi kupitia kwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Almasi Kasongo alisisitiza kila kitu kuhusu mchezo huo kipo palepale.
Hata hivyo, wakati Kasongo akitoa msimamo huo kulikuwa na mambo matatu yaliyozusha sintofahamu juu ya taratibu zinazokwenda kukamilisha mchezo huo.
Jambo la kwanza ambalo lilikuwa linazusha utata ni juu ya uwanja ambao utafanyika mchezo huo na Maafisa wa Wizara ya Habari, Sanaa na Utamaduni na Michezo walikuwa wakikwepa kutoa msimamo juu ya Uwanja wa Mkapa, ambao awali ulikuwa umefungiwa kabla ya fainali za Kombe la CAF.
Hata hivyo, asubuhi Simba ambao ni timu mwenyeji ikaweka wazi barua kutoka wizara hiyo, ikionyesha waliomba nafasi ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa waliyoiandika Juni 9 na kukubaliwa kwa majibu yalitolewa juzi Juni 12.
Katika barua hiyo yenye kumbukumbu namba BA 280/300/03/10 ikisainiwa na Boniface Tamba kwa niaba ya Katibu Mkuu imewataarifu Simba kuwa kupitia barua yao yenye kumbukumbu namba SSC/WUSM/09/06/2025/01 juu ya maombi ya kufanya mazoezi uwanjani hapo uwanja upo tayari kwa mchezo huo na hata kufanya mazoezi upo tayari.
Aidha barua hiyo imeieleza Simba inakumbushwa kukamilisha taratibu zote za maandalizi ya mechi ikiwemo kushiriki kikao cha maandalizi ya mchezo (Pre-match meeting ambacho huratibiwa na TPLB huku nakala ya barua hiyo ikitumiwa bodi hiyo.)
Jambo la pili lilikuwa linatatiza juu ya hatma ya mchezo huo ni hatua ya uuzwaji wa tiketi sambamba na hatma ya namna ya uingiaji wa mashabiki ambao walikata tiketi za mchezo wa Machi 8, ukiwa haujatoka ufafanuzi wowote.
MAREFA WALEWALE
Wakati wadau wakijiuliza juu ya maswali hayo TFF kupitia bosi wao mmoja wa juu akaliambia Mwanaspoti, taratibu zote za mchezo huo wa kesho zilikuwa zinakwenda kama ilivyokuwa kwenye mechi ya kwanza.
Kwa mujibu wa taarifa ya Machi 5 iliyotangaza waamuzi wa Machi 8, mwamuzi wa kati alikuwa ni Ahmed Arajiga (Manyara), akisaidiwa na Mohmmed Mkono (Tanga), Kassim Mpanga (Dar es Salaam) na mezani alipaswa kuwa Amina Kyando kutoka Morogoro.
“Kuna vitu waandishi mnachanganya, hamuwasaidii watu, anayetangaza uwanja na taratibu zingine za maandalizi sio timu mwenyeji ni bodi, nikiwauliza kwani bodi ilisema kutakuwa na mabadiliko?” Alihoji bosi huyo wa TFF na kuongeza;
“Mchezo upo palepale, utafanyika kwenye uwanja uleule ambao ulikuwa uchezwe mechi ya kwanza na kuhusu waamuzi watachezesha wale wale waliokuwa wachezeshe mechi ya kwanza kwa hiyo taratibu zipo hivyo hakuna mabadiliko. Hivyo ni wazi hata mechi ya Juni 25 wataendelea kusalia waamuzi haohao wa awali.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa Oktoba 19, 2024, Simba ikiwa wenyeji ilipoteza kwa bao 1-0 lililotokana na kujifunga kwa beki wa kulia, Kelvin Kijili wakati akiokoa mpira wa Maxi Nzengeli.
Hilo lilikuwa pambano la nne mfululizo kwa Simba kupoteza la dabi mbele ya Yanga, huku timu hizo zikiwa zikichuana kileleni kwa sasa zikitofautiana kwa pointi moja.
Yanga ambao ni watetezi kwa msimu wa tatu mfululizo, inaongoza kwa pointi 73 baada ya mechi 28, Simba ikiwa na 72 kwa idadi kama hiyo ya mechi, hivyo mechi hiyo ya Juni 25 inaweza kutumiwa kutangaza bingwa mpya wa msimu huu.