MUHAMMAD ALI : Aliteswa na ubaguzi wa rangi duniani
Muktasari:
Ali aliibiwa baiskeli na kuripoti polisi, akiwa kituoni alikutana na askari, Joe Martin na kumwambia anataka ampige mwizi aliyeiba baiskeli yake.
AKIWA na miaka 12, Muhammad Ali wakati huo akijulikana kwa jina la Cassius Clay, alishawishika kujifunza ngumi kupitia mkasa wa aina yake.
Ali aliibiwa baiskeli na kuripoti polisi, akiwa kituoni alikutana na askari, Joe Martin na kumwambia anataka ampige mwizi aliyeiba baiskeli yake.
Martin akamwambia: “Sawa lakini lazima ujifunze kupigana kabla ya kufikiria kukabiliana na watu.
Martin ambaye mbali ya kuwa ofisa polisi, pia alikuwa akitoa mafunzo ya ngumi katika gym yake.
Inadaiwa huo ulikuwa mwanzo wa Ali kuingia katika ngumi akianzia kwenye gym ya Martin, akaingia katika ngumi za ridhaa na mara ya kwanza alipigana na kushinda mwaka 1954.
Aliendelea na ngumi hizo akiiwakilisha Marekani katika Michezo ya Olimpiki na mingineyo kabla ya kugeukia ngumi za kulipwa zilizompa umaarufu zaidi.
Mbali na tukio la kuibiwa baiskeli, katika maisha yake ya utotoni Ali pia alikumbana na adha za ubaguzi wa rangi.
Mwaka 1964, akiwa na miaka 22, aliamua kujiunga na Umoja wa Waislamu na hatimaye akabadili jina na kujiita Cassius X lakini baadaye akaamua kujiita Muhammad Ali akitoka katika Ukristo wa dhehebu la Orthdox na kuwa Muislam.
Tangu hapo Ali akawa anajulikana zaidi kwa mambo mawili, mwanamichezo na muumini wa Dini ya Kiislam aliyechukizwa na ubaguzi wa rangi na manyanyaso yote ya binadamu dhidi ya binadamu mwenzake.
Katika harakati zake za kupambana na mambo hayo, Ali hakusita kutoa matamshi makali yaliyowakera watawala na mojawapo la kukumbukwa ni wakati wa vita ya Marekani dhidi ya Vietnam.
Ali aliifananisha vita hivyo na mchezo dhidi ya watu weusi: “Wazungu weupe wanawapeleka watu weusi kupigana na watu wa ‘njano’ (Wavietnam) ili kuilinda nchi ambayo waliiba kwa Red Indians.”
Ali alikataa kuchezeshwa mchezo huo, alikataa kusajiliwa kwenye Jeshi la Marekani, akashitakiwa kwa usaliti ingawa bado aliendelea kusisitiza kwamba hana ugomvi na watu wa Vietnam.
Pia, alinyang’anywa leseni yake ya ngumi na kushindwa kupigana kati ya mwaka 1967 hadi 1970 kabla ya kurudishiwa leseni yake mwaka 1971.
Akiwa amenyang’anywa leseni Ali alizunguka sehemu mbalimbali hasa vyuoni akiwashawishi Wamarekani kutounga mkono vita dhidi ya Vietnam huku akiwahimiza Wamarekani Weusi kujivunia weusi wao na haki zao.
Mwandishi wa mmoja wa michezo, Dabe Zirin alimzungumzia Ali kuhusu sakata hilo akisema: “Miaka ya 1960 kulikuwa na harakati za kijamii za aina mbili, mapambano ya kupinga vita dhidi ya Vietnam na mapambano ya Wamarekani Weusi kujikomboa, na hapo unaye mwanamichezo maarufu duniani ambaye ameuweka mguu wake katika mapambano yote hayo mawili.
Katika vita yake dhidi ya manyanyaso, Ali akiwa Beirut mwaka 1974 alitembelea kambi ya wakimbizi wa Palestina na kusema: “Natangaza kuwaunga mkono Wapalestina katika mapambano ya kukomboa ardhi yao.”
Katika vita vya ubaguzi wa rangi Ali pia anakumbukwa zaidi katika tukio lake tata la mwaka 1960 baada ya kushinda medali ya dhahabu kwenye Michezo ya Olimpiki ya Roma, Italia.
Baada ya kurudi Marekani, Ali au Cassius Clay, wakati huo akiwa na miaka 18 akiwa katika mgahawa mmoja kwenye hafla ya chakula cha jioni wahudumu walikataa kumpa chakula kwa sababu ya kuwa Mmarekani mweusi.
Jambo hilo lilimkera mno na kwa hasira aliamua kuitupa medali yake ya dhahabu kwenye Mto Ohio akidai kwamba hangependa kuvaa medali katika nchi ambayo anakataliwa hata kupewa huduma ya chakula.
Hayo ni ndiyo yaliyomtambulisha Ali nje ya ulingo wa masumbwi, kwamba wakati mashabiki wakilia kuondokewa na gwiji wa masumbwi na wengine kuamua kuweka glovu kwenye kaburi lake, nje ya hilo dunia pia iliheshimu misimamo yake dhidi ya ubaguzi wa rangi na manyanyaso mengineyo.
Katika maisha yake yote hadi anafariki akiwa na miaka 74 kama kuna kitu kilichomnyima usingizi basi kitu hicho ni ubaguzi wa rangi na dhulma za aina yoyote.
Kabla ya kifo, Ali aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi ya Parkinson pamoja na matatizo ya kupumua alikuwa akiishi na mkewe Yolanda waliyefunga ndoa mwaka 1986 na kupata mtoto mmoja wa kiume Asaad, ingawa ana watoto wengine wanane kwa wake wa awali akiwamo mwanadada Laila Ali ambaye alifuata nyayo za baba yake kwenye ngumi.
Kwa kuwa Michezo ya Olimpiki inafanyika Agosti mwaka huu nchini Brazil, wanamichezo duniani kote wanasubiri kwa hamu kuona Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) itampa heshima gani Ali baada ya kifo chake.
Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwanaspoti au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz