Prime
Mpango wa Barker kuifanya Simba tishio Afrika
ACHANA na matokeo ya mchezo wa jana, Jumanne, ambao Simba ilicheza dhidi ya Jamus SC katika michuano ya CECAFA Kagame Cup, kwa sababu nyuma ya pazia kuna mambo makubwa ambayo kocha Steve Barker anaonekana kuyafanyia kazi katika wiki ya kwanza ya maandalizi ya msimu mpya.
Kambi ya Kigali, Rwanda, imekuwa zaidi ya sehemu ya kushiriki mashindano hayo kwa Simba. Kwa Barker ni darasa la kuimarisha kikosi cha timu hiyo kuelekea msimu wa 2026/27.
Huu ni msimu wa pili wa kocha huyo raia wa Afrika Kusini akiwa ndani ya Simba. Baada ya msimu uliopita wa kujenga msingi, sasa anaonekana kuhamia hatua nyingine kutengeneza timu yenye uwezo mkubwa zaidi wa kupambana kwenye mashindano ya ndani na Afrika.
Msimu uliopita Barker aliiongoza Simba kutwaa Kombe la Muungano baada ya kuifunga Yanga, kubeba Kombe la CRDB mbele ya Azam FC na kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara, pointi mbili nyuma ya mabingwa Yanga.
Lakini eneo moja ambalo bado linahitaji majibu ni katika michuano ya kimataifa, baada ya Simba kuishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Ndiyo maana maandalizi ya Kigali yanaonekana kuwa ya kimkakati zaidi.
MFUMO KWANZA
Jambo la kwanza ambalo Barker anaonekana kulipa uzito ni kujenga utambulisho wa timu.
Katika mazoezi ya Simba Kigali, kocha huyo amekuwa akisisitiza namna timu inavyotakiwa kucheza ikiwa na mpira, inapopoteza mpira na namna wachezaji wanavyopaswa kusaidiana ndani ya mfumo.
Kwa Barker, wachezaji wapya hawatapata nafasi kulingana na ukubwa wa majina yao na kile walichofanya msimu uliopita huko ambapo wametoka, bali wanapaswa kuelewa falsafa ya timu kuanzia kambini.
Simba ya msimu ujao inahitaji kuwa timu ambayo kila mchezaji anayefika anaelewa anachotakiwa kufanya bila kujali jina lake.
WACHEZAJI WAPYA
Dirisha hili Simba imelenga kuongeza nguvu katika maeneo ambayo yalionekana kuwatatiza msimu uliopita.
Ujio wa Nathaniel Chilambo, Ibraheem Jabaar, Keletso Makgalwa, Kelvin Nashon, Bakari Msimu na Ibrahim Doumbia umeongeza ushindani ndani ya kikosi.
Lakini kazi kubwa ya Barker si kusajili, bali ni kuunganisha wachezaji hao. Jabaar ana faida ya kumfahamu Barker kutokana na kufanya naye kazi Stellenbosch huku Makgalwa akitarajiwa kuongeza kasi na ubunifu pembeni, wakati Doumbia akipewa jukumu la kuongeza makali pale mbele.
USHINDANI WA NAFASI
Simba ya msimu uliopita ilikuwa na kikosi chenye ushindani, lakini Barker anaonekana kutaka kuongeza kiwango hicho zaidi.
Kwa wachezaji wapya kuingia, kila mmoja aliyepo kikosini anahitaji kupigania nafasi yake kila siku.
Hili linaweza kuwa jambo muhimu kwa Simba kutokana na msimu mrefu unaosubiriwa wenye mashindano ya ligi, Kombe la Shirikisho Afrika na mashindano mengine.
HESABU KIMATAIFA
Hili linaweza kuwa eneo kubwa zaidi kwenye mipango ya Barker. Simba imeshindwa kuvuka hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, hivyo safari hii haitaki kurudia makosa hayo.
Kambi ya Kigali na michuano ya Kagame imekuwa sehemu ya kupima ubora wa kikosi kabla ya kuingia kwenye vita kubwa zaidi za CAF.
Barker anafahamu kuwa mafanikio ya Simba hayatapimwa Tanzania pekee, bali namna itakavyopambana dhidi ya timu kubwa za Afrika.
MCHANGUO MENGI
Mchezo wa kwanza dhidi ya Mogadishu City ulionyesha kuwa Barker bado anaendelea kujaribu muundo wa timu.
Baadhi ya wachezaji wapya walipewa nafasi na kuonyesha kuwa wanakitu.
Kocha wa Mogadishu City, Dadir Amin Ali, alikiri Simba ilikuwa na ubora hasa eneo la kiungo. Pia aliwataja wachezaji walioingia kipindi cha pili, akiwemo Keletso Makgalwa na Ibrahim Doumbia, kuwa waliongeza kasi na nguvu kwenye mchezo.
Hilo linaonyesha Barker anataka kuwa na kikosi ambacho kinaweza kubadilisha mchezo wakati wowote kutokana na upana wa kikosi ambacho anahitaji.
MSIKIE KOCHA
Barker alisema maandalizi ya Kigali hayalengi kuangalia matokeo pekee, bali kujenga timu ambayo itaelewana kabla ya msimu kuanza.
“Maandalizi yanaendelea vizuri. Tunataka kila mchezaji aelewe mfumo wetu wa uchezaji, namna tunavyotaka kujilinda, kushambulia na kubadilika haraka tunapopoteza mpira. Hiki ni kipindi cha kujenga timu, si kuangalia matokeo pekee,” alisema Barker.
Kuhusu wachezaji wapya, kocha huyo alisema wameongeza ubora na ushindani ndani ya kikosi.
“Tulihitaji kuongeza ubora katika baadhi ya maeneo. Wachezaji wapya wana uwezo tofauti na kila mmoja ataleta kitu kipya ndani ya timu. Ushindani wa nafasi utakuwa mkubwa na hilo litatusaidia kuongeza kiwango cha timu,” alisema.
Kwa Barker, safari ya kuijenga Simba mpya bado inaendelea. Kigali ni mwanzo wa mchakato huo lakini kipimo halisi kitakuwa katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Agosti 12.