Morocco: TRA United tupo tayari
Muktasari:
- Morocco, aliyejiunga na TRA Septemba 10, 2026 akichukua nafasi ya Mrundi Etienne Ndayiragije, aliliambia Mwanaspoti kuwa kambi ya zaidi ya wiki moja Zanzibar imemsaidia kukifanyia kazi kikosi hicho, hasa katika kuboresha muunganiko wa safu ya ulinzi na ushambuliaji.
TRA United imeingia mapumziko ya Ligi Kuu Bara ikiwa na sura mpya baada ya kumpa mikoba Kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’, ambaye sasa anasema kikosi chake kipo tayari kurejea kwenye mashindano na kupigania malengo yake, akiamini mchanganyiko wa vijana na wachezaji wenye uzoefu unaweza kuipa timu hiyo nguvu ya kufanya vizuri.
Morocco, aliyejiunga na TRA Septemba 10, 2026 akichukua nafasi ya Mrundi Etienne Ndayiragije, aliliambia Mwanaspoti kuwa kambi ya zaidi ya wiki moja Zanzibar imemsaidia kukifanyia kazi kikosi hicho, hasa katika kuboresha muunganiko wa safu ya ulinzi na ushambuliaji.
“Kikosi chetu sasa kipo tayari kwenye mashindano ya Ligi. Tuna kikosi kipana ambacho kina mchanganyiko mzuri wa vijana na wachezaji wenye uzoefu, na ninachoamini ni kwamba kutokana na njaa waliyonayo ya mafanikio, wataweza kuipigania timu kufikia malengo yake,” amesema Morocco.
Kocha huyo amesema bado amekuwa akisisitiza nidhamu ya kiuchezaji na namna ya kupunguza mabao wanayoruhusu, baada ya TRA kuonyesha uwezo wa kufunga lakini pia kuyumba katika ulinzi.
“Bado tunafanya kazi ya kupata muunganiko mzuri wa kiuchezaji kati ya safu yetu ya kujilinda na ushambuliaji. Tunafunga mabao, lakini tunaruhusu pia, hivyo hilo ni eneo ambalo tumekuwa tukilifanyia kazi mazoezini na maendeleo yetu ni mazuri.”
TRA ilianza msimu kwa kusuasua, ikicheza mechi tano bila ushindi kabla ya Morocco kuwasili, hali iliyosababisha uongozi kuachana na Ndayiragije.
Baada ya kuchukua timu, Morocco alianza kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Pamba Jiji Septemba 13 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, ukiwa ushindi wa kwanza wa TRA msimu huu na pia ushindi wake wa kwanza tangu apewe jukumu hilo.
Morocco anaingia kwenye hatua inayofuata akiwa na uzoefu wa kufanya kazi katika soka la Tanzania, akiwa amewahi kuinoa Simba, Namungo FC, KMKM na Geita Gold, huku pia akiwa sehemu ya benchi la Taifa Stars kabla ya kuwa kocha mkuu wa timu hiyo.
Akiwa Taifa Stars, alipata nafasi ya kushiriki katika michuano ya AFCON mara tatu mfululizo, akiwa katika nafasi tofauti za benchi la ufundi.