Morocco alia na mechi ya Yanga
KOCHA Mkuu wa TRA United, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amesema kuahirishwa kwa mechi ya yao dhidi ya Yanga iliyopangwa kuchezwa leo imetibua mipango yake, kwa sababu walikuwa tayari wamejipanga ila kwa sasa atakaa tena kwa muda mrefu.
Mechi hiyo iliyopangwa kuchezwa leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri, Abeid, jijini, Arusha imesogezwa mbele hadi Oktoba 24, 2026, ili kutoa nafasi kwa Yanga kujiandaa na pambano la Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya CFFA FC ya Madagascar.
Akizungumza na Mwanaspoti, Morocco amesema kukaa wiki mbili bila ya kucheza mechi yoyote ya ushindani imeharibu mipango yake, kwa sababu baada ya kupoteza dhidi ya Namungo FC kwa bao 1-0, Oktoba 8, 2026, walihitaji kusawazisha makosa yao.
“Tunaiheshimu Yanga lakini tulihitaji kucheza nao, kutoka Oktoba 8 hadi 24 ni sawa na takribani wiki mbili za kukaa bila kupata ushindani, kwetu itatuathiri kwa sababu wenzetu watakuwa wanaendelea na programu kama kawaida,” amesema Morocco.