Baraza: Ushindi utatupunguzia presha
Muktasari:
- Baraza aliliambia Mwanaspoti matumaini hayo baada ya kikosi chake kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya TRA United Septemba 13, 2026, matokeo yaliyokuwa muhimu kwa timu hiyo iliyokuwa ikipitia mwanzo mgumu wa msimu.
KOCHA wa Pamba Jiji, Francis Baraza, anaamini ushindi wa kwanza wa timu hiyo katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2026/27 utapunguza presha kwa wachezaji wake na kuwapa nguvu ya kuendeleza matokeo mazuri.
Baraza aliliambia Mwanaspoti matumaini hayo baada ya kikosi chake kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya TRA United Septemba 13, 2026, matokeo yaliyokuwa muhimu kwa timu hiyo iliyokuwa ikipitia mwanzo mgumu wa msimu.
Akizungumzia ushindi huo, Baraza amesema wachezaji wake walikuwa wamejipanga kufanya vizuri kwa sababu hawakuamini kama walistahili kuendelea kupoteza mechi nyingi kama ilivyokuwa ikitokea mwanzoni mwa ligi. “Baada ya ushindi huu wa kwanza, naamini presha itapungua kwa wachezaji wangu na tutaendeleza moto huu katika michezo inayofuata,” amesema Baraza.
Kocha huyo amesema maandalizi ya mchezo huo yalilenga kupata matokeo mazuri ili kubadilisha mwenendo wa timu na kuanza kujenga matumaini mapya kwa wachezaji.
“Tulikuwa tumejipanga kufanya makubwa kwa sababu tuliona hatustahili kuendelea kupata matokeo ya kupoteza mechi nyingi. Tulihitaji ushindi ili kurejesha hali nzuri ndani ya kikosi,” amesema Baraza.
Mwanzo wa Pamba Jiji msimu huu ulikuwa mgumu, kwani katika mechi sita za mwanzo ilipata sare moja na kupoteza tano bila kushinda mchezo wowote.
Katika michezo hiyo, timu hiyo ilifunga mabao manne na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 13, matokeo yaliyoifanya kukusanya pointi moja pekee na kushika nafasi ya mwisho katika msimamo wa ligi baada ya mechi hizo sita.
Hali hiyo ilikuwa tofauti na msimu uliopita, ambapo Pamba Jiji ilikusanya pointi tisa katika mechi sita za mwanzo kwa kupata ushindi mara mbili, sare tatu na kupoteza mchezo mmoja.